January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ndugai Spika Bunge la 11, Mwakyembe atajwa Uwaziri Mkuu

Spread the love

WAKATI Bunge la 11 likiwa limekwishapata Spika, Job Ndugai, jina la Dk. Harrison Mwakyembe limeendelea kupewa nafasi ya kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tano inayotarajiwa kutangazwa hivi karibuni. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Ndugai ambaye alikuwa naibu spika wa Bunge la 10, amefanikiwa kushinda kiti cha Spika katika Bunge la 11 baada ya kushinda kura 254 ambazo ni sawa na asilimia 70 ya kura zote. Kinachosubiriwa sasa ni uteuzi wa Waziri Mkuu wa Serikali ya awamu ya tano ambapo Dk. Mwakyembe akitajwa.

Wakizungumza na MwanaHALISI Online, baadhi ya wananchi wamesema kutokana na Taifa lilipofikia, linahitaji waziri mkuu ambaye atafanya kazi bila ya kupokea maelekezo kutoka kwa baadhi ya vigogo.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Chausta, Amina Mcheka, amesema kutokana na Mwakyembe kutajwa kwenye mitandao ya kijamii mbalimbali, anaona anafaa kuwa kuwa waziri mkuu.

Amesema, serikali ijayo inahitaji waziri mkuu ambaye ataendana hali halisi ya jiografia ya nchi, kwa ajili ya kukimbizana na umasikini wa watanzania.

Amina, amesema kuwa na mtu anayefaa kuwa waziri mkuu katika serikali ijayo ni Dk. Mwakyembe kutokana na wananchi kuamini kuwa ni mchapa kazi, ambaye hana hana maamuzi ya woga katika kutetea masilahi ya wananchi.

“Siyo kama mawaziri wakuu waliyopita hawakufanya kitu, bali hivi sasa tunahitaji waziri mkuu ambaye atafanya kazi kwa ufanisi na atakayendana na kauli mbiu ya Rais inayosema Hapa Kazi Tu,” amesema Amina.

Amina, amesema anatambua kuwa nafasi ya uwaziri mkuu inatokana na kuteuliwa bado anaamini mawazo ya wananchi yananafasi kutokana na kufahamu utendaji wa baadhi ya viongozi serikalini.

Hatibu Yahya, amesema, licha ya Dk. Mwakyembe kuwa chaguo la baadhi ya wananchi bado haamini kama Adad Rajab ambaye ni Mbunge wa Muheza atapenya kwenye nafasi hiyo ingawa akipewa anaweza.

“Unajua kama angekuwa amefanya kazi ya uwaziri kwa vipindi vyote viwili nadhani hicho kingekuwa kigezo kizuri, ambacho kingemuongezea uwezekano wakupata nafasi hiyo,” amesema Yahya.

Amesema nafasi kubwa ambayo inamfaa Adad katika Baraza la Mawaziri lijalo ni ile ya Mambo ya Nchi za Nje, kwani hiyo inatokana na uzoefu wake wa kufanyakazi za ubalozi nchi za nje.

Naye Mchungaji Wiliam Mwamalanga, amesema kuwa taifa linahitaji waziri mkuu mwenye hekima ya mungu ya uongozi ambaye atamsaidia Rais kuiangalia jamii ya watu wa kipato cha chini kabisa.

“Tunataka waziri mkuu ambaye ataondoa makundi ya uhasama na kuleta utulivu ndani ya nchi kama atapatikana ambaye hana maadili kuna hatari nchi itawaka moto jambo ambalo hatuliombei,” amesema Mchungaji Mwamalanga.

Mchungaji Mwamalanga, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu wa Madhehebu ya dini ya Kiislam na Kikristu, amesema pia awe mtu asiyekurupuka.

“Tunataka waziri mkuu asiyekurupuka, atakayekuza uhuru wa wa habari, atakayeisimamia serikali na kurudisha maadili ya umma na kuiweka serikali mikononi mwa wananchi ukilinganisha,” amesema Mchungaji Mwamalanga.

Alisema katakuwa hana maadili atakuwa ni waziri mkuu ambaye ataimarisha makundi ya mafisadi ambayo yataharibu nchi, kwa sababu mafisadi hao wataongeza gepu la waliyonacho na wasiyonacho.

Hata hivyo, Dk. Mwakyembe juzi, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa kisheria uwaziri mkuu hauji kwa mtu kupitia kwenye mitandao ya kijamii kama wananchi wanavyofikiria.

Mmoja wa wananchi, Dk. Rex Kidyalla amesema kamwe haiwezekani kupatikana waziri mkuu wa tofauti na serikali ya CCM kwani vongozi wanaotokana na chama hicho wote wana akili zinazofanana.

“Unajua watanzania hatuchagui viongozi na wala hatuchagui viongozi ikumbukwe kuwa nchi hii wanaochagua viongozi ni watu watatu tu, mmoja ni Ally Hassan Mwinyi, Benjamini Mkapa na Jakaya Kikwete, kwa mfumo huo hata sisi wananchi tukiwa na mapenzi ya kumtaka waziri mkuu ambaye anaweza kufanya kazi za wananchi haiwezekani kumpata.

“Hadi sasa ni wazi kwamba viongozi wengi wanachaguliwa na viongozi wa ngazi ya juu kwa maana hiyo inaonesha wazi kuna mtu ambaye ameshapangwa kwa ajili ya kushika nafasi hiyo ambaye tayari atakuwa Waziri Mkuu hata kama tutapiga kelele haitasaidia,” amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha wafanyakazi wa taasisi za elimu (THTU), Dodoma Nashon Maisori amesema kwa sasa taifa linahitaji waziri mkuu mwenye uthubutu, uadilifu,nuzoefu na awe kiongozi mwenye hekima.

“Mtu mwenye sifa hizo ambaye anatakiwa kuwa waziri mkuu ni Dk. Harrison Mwakyembe, huyu bwana amekufa na kufufuka haogopi tena, kwa CCM ilivyo sasa haina watu wenye vigezo vya kuwa mawaziri.

“Nalazimika kuona kuwa Dk. Mwakyembe kuwa waziri mkuu, kiongozi huyo aliweza kulipua mambo mengi ambayo yalitikisa nchi, kama kweli Rais Magufuli anataka mtu mchapa kazi na asiye ogopa mikikimikiki basi bila shaka ni Dk. Mwakyembe ila kwa watu ambao wapo CCM tukizungumzia sifa ya uchafu hakuna aliye msafi,” amesema Maisori.

Kwa upande wa viongozi wa dini ambao walitoa maoni yao nao wasema waziri mkuu asipatikane kwa shinikizo la watu au baadhi ya viongozi bali jambo pekee ateuliwe kiongozi ambaye ni mchapakazi na mwadilifu.

Akitoa maoni yake Askofu wa Kanisa na Menonite Jimbo la Dodoma, Amos Muhagachi amesema waziri mkuu ambaye anaweza kupatikana ni yule mwenye sifa ya kuongoza nchi bila kuwa na ubaguzi wa aina yoyote.

“Mimi siwezi kuwa mpiga ramli kwa kusema waziri mkuu awe mtu wa aina gani bali jambo pekee Rais atumie hekima na busara kubwa kumpata kiongozi ambaye ni mchapa kazi asiyekuwa na tabia ya kulipiza visasi au kulenga kujinufaisha,” amesema Askofu Muhagachi.

Naye shekhe wa mkoa wa Dodoma, Mustafa Rajabu amesema waziri mkuu anatakiwa kuwa ni mtu ambaye anajitambua na kuwatambua watu ambao anawaongoza.

Kwa upande wao waendesha bodaboda nao wameonekana kugawanyika huku wakisema serikali haiwezi kuwa na waziri mkuu ambaye ni tofauti na wale waliopita kutokana na mfumo uliopo kwa sasa ndani ya serikali.

Hali ya mji wa Dodoma kwa sasa imeonekana kuwa na shamrashamra nyingi kutokana na uwepo wa wageni wa wabunge ambao wanaendelea kuapishwa.

error: Content is protected !!