
Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema sheria zinazopitishwa na Bunge zimekuwa zikilidhalilisha Bunge na kusababisha watu kulibeza. Anaripoti Danson Kaijage – Dodoma … (endelea)
Spika Ndugai ametoa kauli hiyo mwishoni mwa Wiki wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya Mawaziri na Manaibu Waziri yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi na kufanyika Jijini Dodoma.
Alisema Mawaziri na Manaibu Waziri wanatakiwa kuheshimiana huku wakijua wazi kuwa kazi yao kubwa ni kuwatumikia wananchi pamoja na kuisaidia serikali.
“Baadhi ya Mawaziri na Manaibu Mawaziri hawapendani wala kuelewana na wakati mwingine mawaziri hawakai katika vikao vya Bunge ili kujibu hoja, jambo ambalo kimsingi ni baya.
“Pia tumeona upitishwaji wa sheria unakuta Mwanasheria Mkuu wa serikali na Waziri wanavutana na hawaelewani na ndiyo maana Bunge limekuwa likitunga sheria ambazo hazidumu, zinabadilishwa mara kwa mara.
“Hii tabia ya kuleta miswada bungeni ya kubadilisha sheria linasababisha watu kulibeza Bunge na kuanza kusema ‘Bunge la Ndugai’ bure kabisa halina kitu na hii inatokana na kuwa na utungaji wa sheria ambazo hazina masilahi mapana ya taifa” amesema Ndugai.
Ndugai amesema ili kufanya kazi nzuri kwa maslahi mapana ya Taifa Mawaziri na Manaibu wao wanatakiwa kupendana na kushirikiana huku wakitambua kuwa vyeo hivyo ni vya muda na aliye Naibu anaweza kupanda na kuwa Waziri na Waziri akashuka.
Aidha, Ndugai amewataka Mawaziri na Manaibu wake kuhakikisha wanafanya kazi ya kulisaidia Taifa na kuacha kutanguliza maslahi yao binafsi.
Aidha, Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo amesema jambo muhimu kwa wabunge na manaibu mawaziri ni kujenga tabia ya upendo umoja na ushirikiano.
“Nikweli kama sisi hatuwezi kupendana na kushirikiana kamwe hatuwezi kufanya kazi ambayo imemusudiwa.
“Sambamba na hilo ni vyema Bunge kuwa makini wakati wa kupitisha sheria ili kuondokana na tabia ya kubadilisha badilisha sheria Bungeni” amesema Waziri.
Halo Spika Ndugai,
Neno serikali limekuwa linatumika vibaya kwa miaka mingi. Serikali maana yake ni mihimili mitatu, yaani, Bunge, Mahakama, na Uraisi.
Ni kweli “Bunge la Ndugai” ni bure kabisa. Kwanza, lina wabunge 300+. Ni wengi mno na hawajabobea Sheria, Sera au Usimamizi. Sizungumzii uongozi au utawala, bali Bunge butu. Halimsaidii raisi wala kutunga sheria zenye kulinda uchumi na haki ya wananchi.
Kwa nini hakuna sheria inayotaka makampuni yote yakishafanya kazi kwa miaka mitatu, yanaingia kwenye stock na asilimia kubwa ni ya serikali na wananchi.
Hivi Sasa hamjatunga sheria ya kuwalinda watanzania wabunifu. Ni lazima waendelee kuwa na hatimiliki ya kazi zao. Badala yake wanauza na kupoteza mapato ya muda mrefu.
Kampuni za madini zikaguliwe kila mwaka na kwa kushitukiza, kutambua na kulinda madini yetu ya almasi, dhahabu, Tanzanite, gesi ya Helium na Asilia. Mikataba iwe ya muda mfupi, miaka 3 au 5. Kusaini miaka 20, 30. 50, 100 ni kujiuza. Mbona hawafanyi hivyo kwao?
Spika Ndugai, sheria za ardhi ni mbovu, ndiyo maana kuna migogoro. Rekebisha hili. Mawaziri au serikali hazitungi sheria. Hoja pia inaweza kujadiliwa na sheria ikarekebishwa.
Mama Samia alipolalamikia Tanzanite, umeshatunga sheria? Wale wabunge takribani 300 wanafanya nini?
Umelalamikia madiwani kukwepa wabunge. Basi, tunga sheria inayosema kikao cha madiwani kihusucho fedha za serikali kuu, hakiruhusiwi bila kuwa na wabunge wote au kupata ridhaa ya mbunge asiyekuwepo.
Hivyo, kazi ya mkurugenzi na wengine ni kutoitisha mkutano bila uwazi na uwepo wa mbunge.