January 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ndugai apita bila kupingwa Uspika CCM

Spread the love

KAMATI ya Bunge ya Chama cha Mapinduzi (CCM) limempitisha bila kupingwa mgombea wa Uspika, Job Ndugai kugombea nafasi hiyo katika Bunge la 11, baada ya wagombea wenzake kujitoa. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Ndugai alipishwa kwa kauli moja baada ya wagombea wawili waliyojitokeza awali kujitoa na kulazimika kumpitisha Ndugai ambaye alikuwa Naibu Spika wa Bunge la 10.

Wagombea hao walikuwa ni Tulia Akson na Abdallah Ally Mwinyi huku ikielezwa kwamba waliaamua kufanya hivyo kwa madai kuwa wanaamini Ndugai anauwezo wakufanya kazi hiyo kutokana na uzoefu aliyoupata katika Bunge la 10.

Hata hivyo, vyanzo vya ndani katika kamati ya bunge ya wabunge wa CCM inaeleza kuwa Ndugai amepitishwa kuwania nafasi hiyo kutokana na wagombea wenzake kushawishiwa kujitoa.

Chanzo hicho cha kuaminika kililiambia MwanaHALISI Online kuwa baada ya kufika katika ukumbi wa wa mikutano wa CCM Makao Makuu ‘White House’ aliyekuwa wa kwanza kujieleza alikuwa Abdallah Ally Mwinyi, ambaye amesema kuwa licha ya kuwa na nia ya dhati katika kuwania nafasi hiyo lakini ameamua kujitoa huku akidai kuwa anamuunga mkono mwenzake ambaye ni Ndugai.

Chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa baada ya Dk. Tulia Akson kupewa nafasi ya kujieleza, naye pia aliwaambia wajumbe kwamba kweli alikuwa na nia kubwa ya kuwania nafasi hiyo ili aweze kuwa mmoja wa wabunge.

Mbali na hilo chanzo chetu kinaeleza kuwa Dk. Akson alieleza kwamba alikuwa anatamani kuwa miongoni mwa wabunge, kutokana na imani ya Rais kumteua na kuwa mbunge wa viti maalumu hiyo ilimfanya ajitoe kwenye nafasi hiyo ya kuwania nafasi ya uspika.

Hata hivyo, Dk. Akson amesema kutokana na kuwa mbunge wa kuteuliwa kwa sasa anayo shauku kubwa ya kuwania nafasi ya unaibu spika kutokana na kuwa yeye ni mmoja wa wabunge tofauti na angekuwa nje.

Baada kuteuliwa, Dk. Akson alijigamba kuwa ana matarajio makubwa ya kuwa mgombea unaibu spika jambo ambalo linatajwa kwamba linaweza kumfanya aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge la 10, Mussa Zungu.

“Kuna uwezekano Zungu akajikuta katika wakati mgumu zaidi iwapo Dk. Akson atagombea unaibu kwani kuna kila dalili za kutaka naibu Spika awe mwanamke ili kuendesha bunge kwa usawa wa kijinsia,” kilisema chanzo cha habari wetu.

Kwa upande wake katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amesema kamati ya bunge ya CCM kwa kauli moja imempitisha aliyekuwa Naibu Spika wa bunge la kumi na mbunge wa Kongwa Ndugai.

Hata hivyo Nape hakuweza kufafanua ni kwanini wagombea wengine walijitoa na kutokupigiwa kama ilivyo katika miaka yote.

“Hakuna sababu bali wamejitoa kwa sababu wanamuamini Ndugai kwamba ana uwezo wa kuviendesha vikao vya Bunge kwa kuzingatia kanuni,” amesema.

Nape, amesema baada ya kupatikana jina hilo litapelekwa Ofisi za Bunge kwa ajili ya kuteuliwa kuwa mgombea wa nafasi hiyo kwa kushindana na mgombea wa kambi ya upinzani.

Kwa upande wake Ndugai baada ya kupitishwa na chama chake ili kuwania nafasi ya Uspika, amesema ataendesha bunge kwa viwango vya juu na tofauti na ilivyokuwa kwa miaka yote.

Amesema tangu Tanzania ipate uhuru, haijawahi kuwa na bunge kama bunge la kumi na moja kwa kuwa bunge la sasa lina vijana wengi na wasomi wengi.

“Bunge la 11 ni bunge ambalo lina vijana wengi ambao ni wasomi hivyo kutakuwepo na changamoto kubwa katika Bunge hili ni kuhakikisha haki inatendeka kwa vyama vyote kwa kuzingatia misingi ya kanuni.

“Nitawatendea haki wabunge wote wa vyama vyote hapatakuwepo na uonevu wowote kwa mbunge yoyote ambaye atakuwa akifuata kanuni na utaratibu wa kibunge,” amesema Ndugai.

error: Content is protected !!