Monday , 4 March 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Ndugai ajipapatua kuhusu Tundu Lissu
Makala & UchambuziTangulizi

Ndugai ajipapatua kuhusu Tundu Lissu

Tundu Lissu, Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki akiwa hospitali ya Nairobi nchini Kenya
Spread the love

KAULI ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kwamba utaratibu wa kukidhi gharama za matibabu ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu unaendelea kushughulikiwa, ni ya kukiri kile anachokisema mbunge mwenyewe kuwa “Serikali haijalipa hata shilingi moja kugharamia matibabu yangu.” Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Aidha, kauli hiyo ambayo Spika Ndugai ameitoa kupitia mahojiano maalum na kituo cha televisheni cha Azam Media Group, inathibitisha kuwa tangu awali serikali haikuwa imekusudia kulipia gharama za Lissu kama ilivyothibitisha wakati mbunge huyo akiondolewa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma kupelekwa nchini Kenya kwa matibabu ya kitaalamu zaidi na penye uhakika wa usalama wake.

Lissu yuko katika Hospitali ya Nairobi, akiendelea kutibiwa tangu Septemba 7 mwaka jana, aliposhambuliwa kwa risasi mfululizo mwilini akiwa ndani ya gari aliyopanda kwenda nyumbani kwake eneo la Area D, akitokea bungeni alikokuwa anahudhuria kikao cha bunge.

Shambulio lilifanywa wakati akiwasili eneo hilo majira ya saa 7 mchana. Mpaka sasa hakuna taarifa ya kukamatwa mtu yeyote kuhusiana na tukio hilo la kutisha na la aina yake kutokea nchini. Alimiminiwa zaidi ya risasi 30 na watu wawili waliotumia gari na ambao ilisemekana kuwa walimfuatilia Lissu tangu alipokuwa anaondoka viwanja vya bunge.

Tangu hapo, matibabu ya Lissu, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), yamekuwa yakisimamiwa na familia yake pamoja na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mara kadhaa amekuwa akisikika akilalamika kuwa hajalipiwa gharama na Bunge ilhali ni haki yake kwa mujibu wa sheria. Aliahidi kuwa ataipigania haki yake hiyo atakaporudi nyumbani.

Matibabu ya Lissu yamekuwa yakizua mjadala mzito wakati wote. Awali bunge na serikali walisema hawatalipa gharama kwa sababu anatibiwa nje ya nchi kwa usimamizi wa chama chake na familia yake. Baadaye kupitia kwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, serikali ipo tayari kulipia gharama za matibabu ya Lissu ikiombwa kufanya hivyo na familia yake. Ikaibuka hoja ni mbunge gani serikali ililipia matibabu yake baada ya kuombwa na familia.

Kufikia sasa kipindi ambacho ni Lissu kuanza awamu ya pili ya matibabu ikitarajiwa kupelekwa katika moja ya nchi za Ulaya kwa ajili ya mazoezi ya kumwezesha kutembea tena, gharama za matibabu yake zimetajwa kufikia Dola 300,000 (sawa na kiasi cha Sh. 600 bilioni).

Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema, alitoa taarifa hiyo mbele ya vyombo vya habari juzi Jumapili alipokutana na wahariri; na akasema wazi kuwa gharama hizo zimelipwa na watu mbalimbali wakiwemo Watanzania, kwa kushirikiana na familia na Chadema.

Mbowe amesema Lissu sasa anaanza kutembea, na anatarajiwa tarehe 6 Januari (Jumamosi hii) kusafirishwa kwenda moja ya nchi za Ulaya kwa ajili ya kuanza awamu nyingine ya matibabu – kufanya mazoezi ya kutembea mwenyewe.

Lissu mwenyewe amekaririwa kupitia mitandao ya kijamii akisema hivi karibuni kuwa amepona. “Nimepona. Nitatembea na nitarudi nyumbani kwetu kuendelea kufanya kazi ambayo wananchi wanaonesha kukubali mchango wangu.”

Wakati wa mkutano wa Mbowe na wahariri, uliofanyika nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam kama sehemu ya kukaribisha mwaka 2018, Lissu alisikika kupitia simu ya moja kwa moja akisema, “Sijambo sana viongozi wangu na ndugu zangu. Sijambo. Sasa sina jeraha lolote, sina nyuzi (iliyotokana na mshono), na nimeanza kusimama na kutembea mwenyewe. Leo walinichukua huko nje na kunifundisha kutembea tena. Nilijitahidi nikafikia kusema nimechoka sasa nirudisheni kule kitandani kwangu.”

Katika maongezi hayo alisema ataondoka Nairobi tarehe 6 mchana kwenda Ulaya. “Wanasema nikitoka kanisani, nitarudi hospitalini na kutoka hapo nitachukuliwa kwa ambulance mpaka uwanja wa ndege kwa safari ya Ulaya,” alisema. Hakutaja anapelekwa nchi gani ya Ulaya. Mbowe hapo awali, alisema kimkakati kwa sasa hawaitaji nchi anayopelekwa Lissu.

Alikuwa ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji aliyeanza kuzungumza kwa simu yake ya mkononi na Lissu. Baadaye alimpa simu Mbowe, akafuata Frederick Sumaye na Profesa Mwesiga Baregu. Wote hao ni wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

Ndugai amesema yeye binafsi amekutana na familia ya Lissu na yapo makubaliano yaliyofanywa kuhusu suala hilo. Anatoa maelezo hayo wakati hivi karibuni Katibu mpya wa Bunge, Stephen Kagaigai, aliposikia malalamiko ya Lissu na familia yake kuwa wamepuuzwa na Bunge, alijibu kwa kutaka aelezwe “hizo haki ambazo Lissu hapatiwi na bunge ni zipi.”

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mtoto wa Mzee Mwinyi amwaga machozi

Spread the loveMtoto wa Hayati mzee Mwinyi, Abdullah Ali Hassan Mwinyi ameshindwa...

Habari za SiasaTangulizi

Mzee mwinyi alikuwa mwanademokrasia wa kweli

Spread the loveMtoto wa Hayati Ali Hassan Mwinyi, Abdullah Ali Hassan Mwinyi...

Habari za SiasaTangulizi

Samia: Mwinyi alikuwa maktaba inayotembea

Spread the loveRais Samia Suluhu hassan amesema Hayati rais mstaafu, Ali Hassan...

Habari za SiasaTangulizi

Kikwete: Mwinyi alinianzishia safari yangu ya kisiasa

Spread the loveRAIS Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema atamkumbuka...

error: Content is protected !!