Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Ndugai agomea milioni 43 matibabu ya Lissu.
Habari za SiasaTangulizi

Ndugai agomea milioni 43 matibabu ya Lissu.

Job Ndugai, Spika wa BUnge la Tanzania. Picha ndogo Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki
Spread the love

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ametua nchini akitokea nchini Kenya anapomuuguza Mbunge wa Singida Mashariki ( Chadema), Tundu Lissu na kufunguka kwamba Spika Job Ndugai amezuia Sh. milioni 43 zilizochangwa na wabunge kusaidia matibabu huku akivituhumu vyombo vya ulinzi na usalama kwamba vinahusika kumpiga risasi mbunge huyo, anaandika Hellen Sisya.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mbowe amesema licha ya fedha hizo kuchangwa na wabunge wote wakiwamo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) , mpaka sasa hazijatolewa kwa ajili ya kugharamia matibabu ya Lissu.

Amesema licha ya kuzungumza na Spika Ndugai na kukubaliana nae kwamba ampatie utaratibu wa kuzituma moja kwa moja hospitalini nchini Kenya anapotibiwa Lissu, lakini bado hilo halijafanyika mpaka sasa.

Mbowe ambaye alirudi nchini jana jioni, amesema kuwa siku Lissu alipopigwa risasi mjini Dodoma, alifanya kikao na Spika pamoja na Waziri wa Afya, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kwa ajili ya kuangalia namna bora ya kumsaidia Lissu.

Hata hivyo, Waziri Mwalimu pamoja na Spika walitaka Lissu akatibiwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na kama itashindikana ndipo apelekwe nchini India.

Mbowe amesema baada ya kuona hali ya Lissu ilivyo alitaka apelekwe nchini Kenya, jambo ambalo lilipingwa na Spika pamoja na Waziri na wakasema kama ni hivyo wao hawatahusika na gharama za matibabu hayo.

Akifafanua mbele ya waandishi wa habari, Mbowe ameongeza kuwa ni jambo la ajabu kuona fedha zilizochangwa na wabunge, Spika ameendelea kuzikalia badala ya kuzitoa ili zisaidie kufanya kazi ya kumtibu Lissu.

Kuhusu tuhuma za nani aliyehusika kumpiga Lissu risasi, Mbowe aliweka bayana kwamba mtuhumiwa namba moja ni vyombo vya ulinzi na usalama ingawa hakumtaja mtu kwa jina.

Aidha, Kuhusiana na kauli ya Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma aliyoitoa jana kwamba suala la Lissu viachiwe vyombo vya dola, amesema yeye hana utalaam huo na kwamba bora akae kimya asubiri masuala ya kisheria ambayo yanamhusu.

Hata hivyo , aliwataka Watanzania kutoamini baadhi ya taarifa zinazotolewa na watu mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii na kwamba wanaozitoa hawajaonana na Lissu na kuzungumza naye.

Kuhusu kauli ya serikali kusema ipo tayari kugharamia matibabu ya Lissu popote duniani endapo familia ya Lissu itatuma maombi, Mbowe amesema kuwa hilo halitawezekana kwani hata nchini Kenya serikali ingeweza kusaidia na akatibiwa huko.

Ameahidi kwamba siku Lissu akirejea nchini, ataanika kila kitu kilichompata ili Watanzania wapate ukweli na undani wa tukio lote lilivyotokea mjini Dodoma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!