August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ndugai aendeleza panga pangua Kamati za Bunge

Spread the love

JOB Yustino Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameteuwa wajumbe wapya 16 wa Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, anaandika Aisha Amran.

Uteuzi huo umetokana na mabadiliko yaliyofanyika baada ya baadhi ya waliokuwa wajumbe wa kamati hiyo kuhamishiwa katika kamati zingine kwa nia ya kuboresha utekelezaji wa majukumu ya kibunge.

Wajumbe wapya wa kamati hiyo ni Asha Juma, Daniel Mtuka, Dk. Faustine Ndugulile, Dk. Hadji Mponda, Dk. Jasmine Bunga, Gibson Meiseyeki, Joseph Mhagama, Juliana Shonza, Kemirembe Lwota, Lucia Mlowe, Mary Muro, Martha Mlata, Masoud Salim, Oscar Mukasa, Stanslaus Nyongo na Yusuph Makame.

Hii ni mara ya tatu kwa Spika Ndugai kufanya mabadiliko kwa kuhamisha wajumbe mbalimbali katika kamati zao ndani ya kipindi cha miezi kumi. Mara ya mwisho alifanya mabadiliko kama hayo mnamo tarehe 26 Mei mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Ofisi ya Bunge, mabadiliko hayo yanalenga kuwawezesha wabunge kujifunza na kujipatia uelewa na uzoefu katika kutekeleza shughuli mbalimbali za Bunge.

Kutokana na mabadiliko hayo, wajumbe wa kamati hiyo watakutana kwa ajili ya kufanya uchaguzi wa viongozi wao na kuandaa ajenda za vikao vya kamati.

“Msingi wa mabadiliko haya unatokana na Ibara ya 96 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, inayolipa Bunge mamlaka ya kuunda Kamati za Bunge kwa kadri linavyoona inafaa kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa majukumu yake.

Na Kanuni za Bunge zinampa Spika mamlaka ya kuteua wajumbe katika kamati mbalimbali za Bunge ikiwa ni pamoja na mamlaka ya kuongeza, kubadilisha au kupunguza idadi ya wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge,” imeeleza taarifa hiyo.

error: Content is protected !!