July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ndege ya Marekani yaanguka Afghanistan

Spread the love

WATU 11 wamefariki dunia baada ya ndege ya kijeshi ya Marekani aina ya Hercules kuanguka katika uwanja mmoja wa ndege nchini Afghanistan.

Jeshi la Marekani limesema kuwa ndege hiyo yenye muundo wa C-130 ilianguka majira ya saa sita usiku katika Uwanja wa Ndege wa Jalalabad.

Kanali wa jeshi la Marekani Brian Tribus ameiambia Shirika la Habari la AFP kuwa watu sita kati ya waliouawa walikuwa wanajeshi wa Marekani, na waliosalia walikuwa raia.

Ndege za muundo wa C-130 hutumiwa na jeshi kusafirisha wanajeshi na mizigo mizito katika maeneo yanayokusudiwa.

Ndege hizo ni tofauti na zile zinazotumika katika maeneo ya vita ambazo pia hazitumia rubani kwani zinaendeshwa kwa mitambo maalumu.

Kwa upande wake, msemaji wa kundi la Taliban ambalo hivi karibuni liliutwaa tena mji wa Kunduz, Zabihullah Mujahid alisema kuwa ndege hiyo imedunguliwa na wanamgambo wake walioweka kambi katika eneo la kaskazini mwa Afghanistan.

Katika taarifa iliyotolewa kupitia mtandao wa twitter, msemaji huyo alisema kuwa kundi hilo lilitungua ndege hiyo kama sehemu ya ulipizaji wa kisasa cha mashambulizi wanayofanyiwa.

Hata hivyo, mashirika ya habari yanasema hakuna ishara yoyote kwamba hilo lilikuwa shambulio lililofanywa na wapiganaji hao wa Taliban.

Jeshi la Marekani limesema linaendelea kuchunguza kile kilichosababisha ajali hiyo.

Ajali hiyo ya ndege imetokea huku ndege za kijeshi za Marekani zikisaidiana na wanajeshi wa Afghanistan kujaribu kukomboa mji wa Kunduz uliotekwa na wapiganaji wa Taliban.

Kwa sasa kumekuwa na mfulilizo wa milio ya makombora na risasi katika eneo hilo la Kunduz.

Takriban wanajeshi 10,000 wa Marekani wako nchini Afghanistan baada ya mpango wa kuondoa majeshi hayo kubadilishwa mapema mwaka huu kama ilivyotarajiwa awali.

Rais Barack Obama wa Marekani alikuwa ameahidi kuacha wanajeshi wachache sana wa Marekani nchini humo ambao wangekuwa wa kulinda ubalozi wa Marekani kufikia mwisho wa mwaka 2016.

error: Content is protected !!