July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nchi imelazimisha vijana kukosa ajira

Baadhi ya vijana waliojitokeza kwenye usaili wa ajira za Uhamiaji

Baadhi ya vijana waliojitokeza kwenye usaili wa ajira za Uhamiaji

Spread the love

LINAPOKUJA suala la ajira kwa vijana wazungumzaji wakubwa sio vijana wasio na ajira, bali wale waliofanikiwa au viongozi wa kiserikali ndiyo huzungumza na kujaribu kujibu maswali ya kwa nini vijana wengi wa kitanzania hawana ajira. Anaandika Mwandishi wetu … (endelea).

Kwa bahati mbaya majibu ya wote ama viongozi wa serikali au wanaharakati wa ajira (ambao ni vijana wa makamo waliofanikiwa) yanaegemea kwenye dhana maarufu ya “mind set” ukimuuliza Waziri wa Kazi na Ajira, kwa nini vijana wengi wenye vigezo vya kupata ajira hawana ajira nchini, atakujibu porojo nyingi.

Hitimisho litakuwa “vijana wanapaswa kubadili mind set zao.” Ukimuuliza kijana aliyefanikiwa katika maisha wengi ni vijana wa makamo 35+, atakujibu “vijana wengi hawajitambui wapo wapo akili zimelala”.

Makala haya yanafananisha majibu hayo sawa na kutibu mgonjwa bila kumuuliza nini kinamsumbua, mara kadhaa nimekuwa nikiugua na kuhudhuria hospitali, kabla ya kuelekezwa nipime ama damu, mkojo au choo kila daktari hunitaka nieleze nini kinanisumbua na tatizo lilianza lini?

Pia hutaka kujua kama kuna matibabu ya aina yeyote nimepata kabla ya kufika pale hospitali. Baada ya taarifa za namna hiyo na zingine, daktari hunielekeza maabala kwa ajili ya vipimo.

Nashawishika kusema kuwa hii ndiyo njia sahihi ya kutatua tatizo lolote lenye kuathili jamii, lazima mwathirika ahusike moja kwa moja ili kupata kiini cha tatizo linalomsumbua na kutafuta njia bora ya kulitatua.

Napenda kukuhakikishieni kuwa sio kweli kwamba vijana wana mtazamo hasi kama ambavyo imekuwa ikisemwa, vijana wengi wanajishughulisha kwa namna moja ama nyingine.

Unapokuwa umetangaza kazi ukapata vijana 23,000, 11,000, 7,000 tafsiri ni kuwa vijana hawa wako tayari kufanya kazi, wana vigezo na ari ya kutosha.

Unapotembea mtaani ukakutana na vijana wanauza mitumba, matunda, fedha kwa ajili ya chenji, tafsiri sahihi ni kuwa vijana wanajituma na wako tayari kufanya kazi.

Unapoona mama lishe wanachuuza chakula, vijana wanafungua saloon za kutengeneza nywele, maduka; sio kweli kwamba wana tatizo la “mind set”.

Hii ni tafsir hafifu sana, wako vijana maelfu kwa maelfu wanaendesha bodaboda, hata wale Panya Road wanapaswa kuangaliwa kwa jicho lingine kama ambavyo watanzania wanaendelea kuaminishwa.

Kama vijana mmoja mmoja wamekwishabadilika na wamepiga hatua, wanafanya ujasiriamali wanasaka pesa kwa nguvu zote kwa njia halali na zisizo halali kwa hiyo, sio kweli kwamba wana mtazamo hasi.

Familia za sasa hakuna kula kulala kila familia inayo shughuli ya kuwaingizia kipato bila kujali wameajiriwa ama wanafanya ujasiliamali.

Kwa hiyo, tatizo ni tija katika shughuli, ni upatikanaji wa ajira zinazolipa, ni upatikanaji wa faida katika shughuli za kiuchumi, pengine swali kwa viongozi wenye kuongelea mustakabali wa vijana ingekuwa “kwanini fedha hakuna na iliyopo iko kwa wachache?

Jibu rahisi na lenye mashiko ni kuwa sekta za kiuchumi zimeshindwa kuwaza nje ya boksi ama kwa bahati mbaya au kukusudia kwa manufaa ya tabaka la wachache wenye nacho.

Kwa mfano, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linashindwa kujenga kiwanda japo kimoja chenye kuzalisha vifaa vya ujenzi kwa ubora wa hali ya juu? Sekta ya ujenzi pekee inatoa ajira kwa watu 35 milioni nchini India.

Hao wanaokaa vikao vya kujadili mustakabali wa vijana wamewahi kujadili namna gani watatengeneza ajira kupitia sekta hii au ndio wanatatua tatizo la ajira kwa kutujazia Wachina na Wahindi kwenye sekta ya ujenzi?

Kwa idadi ya baiskeli, pikipiki na magari yaliyopo nchini kwa sasa nadhani kiwanda kikubwa cha uzalishaji wa vipuli na mataili kingetengeneza ajira lukuki kwa vijana wasomi na wasiosoma.

Mamlaka ya Bandari, Tanroads wameshindwa nini kuwaza kutafuta mabilioni kadhaa wakayawekeza kwenye ujenzi wa kiwanda kikubwa bora cha kuzalisha vipuli na mataili ili kushughulika na tatizo la ajira na kuinua uchumi wa nchi?

Ninavyoamini mimi, Shirika la Umeme nchini (Tanesco), haliwezi kupata fedha ya kulipa IPTL halafu likakosa shilingi trilioni moja hata kwa kukopa kujengea kiwanda cha kutengeneza vifaa vya umeme vyenye ubora wa kimataifa na likawauzia wateja wake na wale wa maziwa makuu na hatimaye kutengeneza ajira kwa mamia ya vijana.

Hivi hata Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) haiwezi kuwezeshwa kuwa na kiwanda madhubuti cha kutengeneza madawa tiba yenye ubora na viwango vya kimataifa na hivyo kuuzia wananchi dawa salama na zenye kuaminika na hivyo tukawa tumezalisha ajira.

error: Content is protected !!