January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nchi iko salama, raia wako salama?

aadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya mashujaa Kaboya, Kagera
Spread the love

RAIS wa Jamhuri, Jakaya Kikwete amenukuliwa na vyombo vya habari, Alhamisi iliyopita akisema, nchi iko salama; na jeshi liko imara kulinda nchi na mipaka yake.

Amesema, “Ujumbe wetu mkubwa wa leo ni kwamba tuko tayari wakati wote; na saa yoyote kulinda nchi yetu na mipaka yake. Hatuna nchi nyingine…hatuwezi kumruhusu yeyote kuicheza nchi yetu, ama kuimega…”

Aliongeza, “Laleni usingizi salama. Msisikilize maneno ya mitaani kwa sababu jeshi letu liko imara kabisa kulinda nchi yetu na mipaka yake. Yeyote atakayejaribu kuivamia ama kuichokoza, atakiona cha mtema kuni.”

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo, wakati akihutubia wananchi kwenye maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya mashujaa huko Kaboya, wilayani Muleba, mkoani Kagera.

Hata hivyo, Rais Kikwete hakueleza nani anataka kuvamia Tanzania. Sababu za kufanya hivyo ni nini? Yuko wapi? Amejituma au anatumiwa. Kama anatumiwa, ni nani anayemtuma. Kwa shabaha ipi?

Aidha, Rais Kikwete hakueleza wananchi ni lini jeshi lao lilikuwa dhaifu? Lini limesukwa upya? Lini limeanza kuwa imara na lini halikuwa tayari kulinda nchi na mipaka yake?

Hakueleza pia kama hayo ni matamshi ya kawaida ambayo yangeweza kutolewa na kiongozi yeyote kwenye siku kama hiyo. Hayo hakueleza. Ameacha wananchi wajitafutie wenyewe – mithili ya kuku wa kienyeji – anayehaha kujitafutia taarifa za maadui zake.

Rais Kikwete hawezi kusema nchi iko salama na kutaka wananchi walale salama, wakati wanajua kuwa hawako salama.

Katika siku za karibu, yeye na rais mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame, wamekuwa kwenye “vita” ya maneno.

Mnyukano wa marais hao wawili ulianza pale Rais Kikwete alipotoa ushauri, 25 Mei mwaka huu, kwamba nchi zenye vita vya silaha dhidi ya wapinzani wao wa kisiasa, katika eneo la Maziwa Makuu, zifanye uamuzi wa kuwa na mazungumzo nao, kwani vita pekee vimeonyesha kuwa havitafanikiwa kumaliza tatizo.

Haikuchukua muda, Rais Kagame akajibu matamshi ya rais Kikwete. Alisema serikali yake haiwezi kuzungumza na iliyoita “wauaji” na kuwa hoja ya mazungumzo ni “upuuzi.”

Naye waziri wake wa mambo ya nje amenukuliwa akisema, kauli ya kutaka Kagame azungumze na “wauaji” ni “matusi dhidi ya serikali yake. ”

Ambao Kikwete ametaka Kagame kufanya mazungumzo nao, ni waasi wa kikundi kikuu cha upinzani cha Forces Democratiques de Liberation du Rwanda (FDLR).

Pamoja na ukweli kuwa Rwanda ina historia ya mauaji kwa miaka mingi. Wahutu kwa Watutsi wameuana sana. Kila kabila lilifanya mauaji dhidi ya lingine kupigania utawala na miliki ya ardhi.

Yapo madai Rais Kagame amegomea ushauri wa Rais Kikwete, kwa kuwa anakituhumu Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwa na uhusiano wa karibu na chama cha upinzani cha Democratic Green Party of Rwanda (DGPR).

Taarifa zinanukuu maofisa wa serikali ya Rwanda wakisema, kiungo kikuu kati ya wapinzani wa Kagame na CCM, ni mbunge mmoja wa chama hicho kutoka Tanzania Zanzibar.

Pamoja na mengine, serikali ya Kagame inadai kuwa kitendo cha chama kilichopo ikulu – CCM – kujenga mahusiano ya karibu na wapinzani wa Rwanda, hasa wakati huu wa mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ni moja ya visingizio vya siri vinavyotumiwa na Kagame kugomea ushauri wa Rais Kikwete.

Hivyo basi, Rais Kikwete hawezi kusema nchi iko salama, wakati wananchi wameanza kuona chokochoko dhidi ya nchi jirani kwa kuwa tu, jirani huyo amekataa kuzungumza na wapinzani wake. Amekataa, aachwe.

Yeye mwenyewe ameshindwa au amekataa kukutana na kuzungumza na wapinzani wake wa kisiasa. Tokea mwaka 2010 ulipomalizika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, Rais Kikwete hajakutana na kiongozi mkuu wa upinzani, Dk. Willibrod Slaa. Kama wamekutana, basi itakuwa kwa bahati mbaya tu.

Rais Kikwete amegoma kwenda mkoani Mtwara kuzungumza na wananchi tangu yalipotokea machafuko makubwa yaliyoharibu miundombinu ya serikali, watu binafsi na kujeruhi makumi ya raia.

Badala yake, ofisi yake imetoa tamko la kejeli dhidi ya wananchi kwa kusema, “Wale wanaodai kupigwa na vyombo vya dola mkoani Mtwara, ni vibaka.”

Rais hawezi kutaka wananchi walale alichoita, “Usingizi salama,” wakati ofisi yake inatoa tamko kuwa “Wananchi wanaodai wameshambuliwa na vyombo vya usalama mkoani Mtwara, ni vibaka.” Hawezi.

Nani katika serikali yake amefanya uchunguzi na kubaini wanaodai kushambuliwa na wanajeshi ni vibaka? Nani? Kama uchunguzi haujafanyika, iko wapi tofauti kati yake na Kagame?

Kuna hili pia: Serikali ya Kikwete, kama ilivyo ile ya Kagame, inatuhumiwa kutumia vyombo vya dola kuminya uhuru wa raia – kufungia vyombo vya habari na dola kudhibiti vyama vya upinzani na asasi za kiraia.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, mashambulizi dhidi ya raia; mauaji, utekaji, utesaji, kumwagiwa tindikali, kung’olewa kucha na meno, yameongezeka mara dufu.

Orodha ya watu waliomwagiwa tindikali, kushambuliwa, kuteswa na kupigwa; wanaotilia mashaka kauli ya rais, ni kubwa na inaongezeka kila uchao.

Kwa mfano, nchi yawezaje kuwa salama, wakati serikali haijakamata watekaji na watesaji wa Absalom Kibanda, mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini?

Kibanda alitekwa usiku wa 5 Machi mwaka huu. Alijeruhiwa vibaya kwa nondo, mapanga na kung’olewa meno na kucha; na sasa amepoteza kabisa jicho lake la kushoto.

Tukio hilo la kinyama alilofanyiwa Kibanda linafanana kwa kiwango kikubwa na lile lililomkuta Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka.

Leo ni miezi takribani mitano imepita, tangu Kibanda ashambuliwe. Serikali haijakamata hata panya kwa tuhuma za “kunyofoa” kidole cha Kibanda.

Katika muktadha huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri aliyekatwa sehemu ya viungo vyake na wanaoitwa na serikali “watu wasiofahamika,” hawezi kupata “usingizi salama,” wala kuamini maneno ya rais kuwa “…nchi iko salama na vyombo vya usalama vinalinda nchi na mipaka yake.”

Kibanda hawezi kupata “usingizi salama,” wakati serikali kupitia makamo wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilali, inamtaka atafute silaha na kujilinda.

Serikali inayotaka Kibanda anunue silaha, inajua Kibanda tayari amepoteza jicho lake moja ambalo lingesaidia kuona maadui zake.

Naye Dk. Ulimboka hawezi kuamini maneno ya rais, wakati anaona serikali haijamfikisha mahakamani Ramadhani Ighondo – mtuhumiwa mkuu wa utekaji na utesaji wake.

Dk. Ulimboka anajua nchi haiwezi kuwa salama, wakati Ighondo yuko mitaani.  Hana uhakika kesho atamdaka nani.

Nchi haiwezi kuwa salama na wananchi wakapata “usingizi salama,” wakati serikali ni mtuhumiwa mkuu wa vitendo hivyo.

Vilevile, wananchi hawawezi kukubali kuambiwa nchi yao iko salama, wakati njiani wanapishana na msululu wa askari waliobeba silaha nzito za moto; kama vile nchi iko vitani.

Hawewezi kukubali nchi iko salama kwa kuwa hawana uhakika, askari hawa watafyatua muda gani silaha walizobeba na kwa kumlenga nani?

Hawaamini nchi iko salama na wao wako salama, wakati wanashuhudia ongezeko la matukio ya kihalifu, hadi kusababisha uongozi wa baadhi ya hospitali za serikali jijini Dar es Salaam, kugoma kupokea miili ya watu inayopelekwa na polisi kuhifadhiwa kwenye hospitali zao.

Kama Rais Kikwete anataka aaminike, basi sharti achukue hatua ya kukamata wanaotenda vitendo hivyo. Yeye mwenyewe atoke hadharani kukemea na kuagiza wahusika wote wachukuliwe hatua. Tena asimamie hasa kwa kushuhudia kuwa amri yake inatekelezwa kwa vitendo. Vinginevyo, hakuna atakayemuelewa. Hakuna!

error: Content is protected !!