June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NCCR yaionya serikali

Spread the love

IKIWA ni siku moja kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu, Chama cha NCCR – Mageuzi kimevionya vyombo vya serikali kuacha kutumika kukiingiza madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Kampeni ya Uchaguzi wa NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura amesema “chama chetu kinasikitishwa na jinsi rasilimali za umma zinavyotumika katika kampeni za CCM.

“Kwa mfano, tumeshuhudia Rais Jakaya Kikwete akitumia rasilimali za serikali kuifanyia kampeni CCM. Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu imemkingia kifua mkuu wa nchi kwa kunukuu Ibara ya 42 (3) ya Katiba ya nchi, kuhalalisha muda wa rais kukaa madarakani,” amesema Sungura.

Sungura ametaja upendeleo mwingine unaofanywa na serikali katika kuiingiza CCM madarakani kuwa ni hukumu iliyotolewa jana na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuhusu kesi iliyofunguliwa na Ammy Kibatala kupitia wakili Peter Kibatala kuhusu wananchi kukaa umbali wa mita 200 baada ya kupiga kura iliyokuwa na mvutano.

Kesi hiyo namba 37 ya mwaka huu, mlalamikaji aliiomba mahakama itoe tafsiri ya kifungu cha 104 kidogo cha (1) cha Sheria ya Uchaguzi kama kinazuia ama la wananchi kukaa umbali wa mita 200 baada ya kupiga kura katika vituo.

Amesema 17 Oktoba mwaka chama hicho kilitoa taarifa kwa vyombo vya habari, pamoja na mambo mengine, kilizungumzia uhuru wa mpiga kura kubaki au kuondoka kwenye eneo la mduara wa mita 200 kutoka kwenye kituo cha kupiga kura.

“Kifungu cha 104 (1) cha Sheria ya Uchaguzi, kinakataza tu kufanya kampeni, kuvaa sare ya chama au kitu au ishara inayoashiria kumfanyia kampeni mgombea wa chama cha siasa,” Sungura amesema.

Aidha, amesema kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya uchaguzi, maelekezo yoyote yanayokinzana na sheria na yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ni batili.

Amesema maelekezo yasiyo halali yanalenga kuwaogopesha wapigakura na kutoa mwanya kwa CCM kunyakua madaraka kwa miaka mitano.

“Kifungu cha 63(2) cha sheria ya uchaguzi, kinaeleza wazi aina ya watu wanaoruhusiwa kuwa ndani ya kituo cha kupiga kura, kifungu hicho hakiwezi kutumika kwa watu walio nje ya kituo cha kupiga kura,” amesema Sungura.

Pia, amesema mamlaka ya kituo cha kupigia kura yanaishia kwenye mipaka ya kituo cha kupiga kura tu, kifungu cha 104(1) cha sheria ya uchaguzi kinatoa eneo la mita 200 tu kutoka kilipo kituo cha kupiga kura.

Kwa sababu hiyo halali na iliyopo kwa mujibu wa sheria, mtu akiamua kukaa nje ya mita 200 na bila kufanya fujo haiwezi kuhesabiwa kuwa unavunja sheria.

Mbali na vyombo hivyo, pia amevitaja vyombo vya habari vya serikali likiwemo gazeti la Habari Leo kukiuka taratibu na sheria za nchi, kwa kuipendelea CCM katika kutangaza na kuchapisha habari za uchaguzi.

“NCCR-Mageuzi hatupo tayari kuona baadhi ya watu wanatumia vibaya madaraka ya umma kukisaidia Chama Cha Mapinduzi ili kuendelea kuwanyonya Watanzania,” amesema Sungura.

error: Content is protected !!