July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NCCR: NEC fuateni sheria muondoe utata

Spread the love

“TAMKO lolote linalotoka kwa mtu yeyote lisilofuata Katiba na Sheria kuhusu mwananchi akishapiga kura Oktoba 25, halikubaliki,” anasema Faustine Sungura, Mkuu wa Idara ya Kampeni na Uchaguzi wa Chama cha NCCR-Mageuzi. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea).

Ni kauli aliyoitoa leo makao makuu ya chama hicho Dar es Salaam, akizungumzia utata unaotumika kutengeneza mazingira ya serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kutumia nguvu kudhibiti watu watakaobakia karibu na vituo vya uchaguzi baada ya kupigakura.

Utata kuhusu umbali ambao wananchi wanapaswa kukaa nje ya vituo vya uchaguzi umeongezeka baada ya Rais Jakaya Kikwete, kuamrisha vyombo vya dola kudhibiti wananchi watakaovunja sheria siku ya uchaguzi. Alisema wananchi wakishapigakura waondoke vituoni.

Hoja iliyopo na ambayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeieleza, na ikatiliwa mkazo na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu, ni kwamba hakuna ruhusa ya wananchi kukaa vituoni baada ya kupigakura. Tume imesema ni marufuku mpigakura kubaki ndani ya mita 200.

Sungura amesema “Kifungu cha 104(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, kinasema ‘hakuna mtu atakayeruhusiwa kufanya mkutano nje au ndani ya kituo wakati zoezi la uchaguzi linaendelea, au katika eneo la mzunguko lisilozidi mita 200 kutoka kwenye kituo cha uchaguzi, au kufanya kitu chochote kinachoashiria kumfanyia kampeni mgombea yeyote’ (tafsiri kutoka lugha ya Kiingereza).”

Sungura amesema kifungu hicho hakina utata wowote na kwa hivyo anasisitiza, kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi “mpigakura hakatazwi kubaki kituoni mara baada ya kupiga kura na anaweza kuamua kubaki kituoni au ndani ya mzunguko wa mita 200, isipokuwa anachokatazwa ni kuonesha viashiria vya kumfanyia kampeni mgombea.

“Tuachane na maneno yote, tuangalie sheria, tunafahamu kuwa mwaka huu ni wa mabadiliko na hakuna tatizo kwa mpigiwa kura kulinda kura yake na wapigakura kulinda kura za wagombea wao,” anaeleza Sungura.

Amesema Kifungu cha 3 cha sheria hiyo kinadhihirisha kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, inawajibu wa kisheria kusimamia mchakato wote wa mambo ya uchaguzi na kutoa maelezo kimaandishi yaliyosainiwa na Mwenyekiti au Mkurugenzi wa Tume. Anasema NEC haikufanya hivyo zaidi ya kutoa tangazo kwenye magazeti.

Sungura amesema kipengele cha pili kidogo cha Kif. 104 kinafafanua hatma ya makosa ya ukiukwaji wa Sheria ya Uchaguzi, kikisema, “mpigakura atakayekiuka makatazo yaliyoainishwa kwenye sheria hii akapatikana na hatia, atapigwa faini ya kiasi cha fedha kisichopungua Sh. 50,000 na kisichozidi Sh. 100,000.”

Adhabu mbadala ya kosa hilo ni kifungo cha miezi sita hadi 12 (mwaka mmoja).

Sungura amefafanua kuwa wao NCCR-Mageuzi wanaona suala la mpigakura kuondoka au kubaki vituoni lingebaki kuwa hiari ya mpigakura na sio kuamrishwa asikae wakati sheria haimkatazi.

“Tunachukua fursa hii kuuarifu umma ya kuwa viongozi na wanachama wote wa NCCR-Mageuzi wameandaliwa kufuata sheria za uchaguzi na siyo vinginevyo,” amesema.

Anaona kuna mihemko ya kisiasa na taarifa zilizotolewa isivyo halali kwa kuwa haziendani na sheria. “Tunaiomba sana NEC isimamie sheria ili uchaguzi ufanyike kwa amani.”

Sungura amesema pia kuwa kutegemea mawakala peke yao haitoshi hasa kwa kuwa utaratibu unaotumiwa na Tume ni wasimamizi wa uchaguzi kuwaapisha mawakala wa vyama vyote kwa siri wakiwa peke yao, hatua isiyoaminika kwa kuwa mazingira yanatoa mwanya wa kuwatisha au kuwahonga mawakala watumikie maslahi ya CCM.

NCCR-Mageuzi na vyama vyenzake katika ushirikiano wa Ukawa, vimeelekeza wananchi wabaki maeneo ya karibu na vituo vya uchaguzi wakishapiga kura ili kulinda kura dhidi ya kuibwa na kunufaisha maslahi ya CCM waliotangaza kuwa watapata ushindi hata kwa “goli la mkono.”

error: Content is protected !!