Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa NCCR-Mageuzi yaungana na Chadema kususia kongamano la TCD
Habari za SiasaTangulizi

NCCR-Mageuzi yaungana na Chadema kususia kongamano la TCD

Spread the love

CHAMA cha siasa cha upinzani cha NCCR-Mageuzi, kimesema hakitashiriki kongamano la haki, amani na maridhiano, lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kikidai maandalizi yake hayajafuata utaratibu na baadhi ya mapendekezo yake kutofanyiwa kazi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Msimamo huo ni sawa na ule uliotolewa na chama kikuu cha upinzani nchini humo cha Chadema wa kutokushiriki kongamano hilo litakaloanza kesho Jumanne jijini Dodoma na kutarajiwa kufunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kususiwa kwa kongamano hilo na vyama viwili vyenye nguvu kisiasa vitafanya vyama vitatu pekee vitakavyoshiriki ambavyo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), ACT-Wazalendo pamoja na Chama Cha Wananchi (CUF).

Leo Jumatatu, tarehe 4 Aprili 2022, makao makuu ya NCCR-Mageuzi, jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Sheria na Katiba wa chama hicho, Wakili Boniface Mwabukusi, ametoa maazimio ya kikao cha kamati kuu iliyokutana jana Jumapili chini ya mwenyekiti wake, James Mbatia.

Mwabukusi ametaja mapendekezo ya NCCR-Mageuzi, ambayo amedai hayajafanyiwa kazi kuelekea maandalizi ya kongamano hilo, ikiwemo la viongozi wa vyama vya siasa kuzungumza na Rais Samia kwa ajili ya kujadili ajenda zitakazojadiliwa katika kongamano hilo.

“Kwa bahati mbaya sana chama kilipokea barua ya kukijulisha utayari wa Rais kuonana na viongozi wa chama mnamo tarehe 18 Machi 2022, lakini kwa bahati mbaya ilipofika tarehe hiyo walipewa udhuru wa kuahirishwa wakaahidiwa kikao kitafanyika tarehe 21 Machi 2022, lakini tarehe 20 walipokea taarifa ya kuahirishwa tena,” amesema Mwabukusi.

Mwabukusi amesema “Tulishiriki kikao cha kamati ya ufundi ya TCD, tulihimiza umuhimu wa jambo hili, kwa bahati mbaya sana licha ya ahadi ya TCD kwamba viongozi watakutana na Rais kabla ya kikao cha Dodoma, haikutimizwa mpaka leo.”

Katika hatua nyingine, Mwabukusi amedai NCCR-Mageuzi hakitashiriki kongamano hilo kwa kuwa ajenda zake zimeghushiwa, pamoja na vyama husika kutopewa taarifa za ajenda ambazo zinakwenda kujadiliwa.

“Msingi wetu ni kwamba, kikao cha Dodoma ni maziwa yaliyoghushiwa, hatuko tayari kuwapa Watanzania maziwa yaliyoghushiwa kwa kushiriki kikao. Haiwezekani kikao kimoja kina ajenda tofauti. Ukisoma taratibu za ratiba ya kingereza na kiswahili, ni mkutano wenye sura ya kinyonga ambayo ina lengo la kuwatega watakaohudhuria, kuridhia mambo ambayo wajumbe hawakupewa taarifa,” amesema Mwabukusi.

“Mpaka tunakwenda kwenye kongamano kila chama lazima kiwe kimepatiwa makabrasha ya ajenda, yapitiwe na kukubaliana kikamilifu ndiyo twende Dodoma. Kwa mara ya kwanza unaambiwa muswada ni wako hujui hata sentensi ya kwanza ina maana gani, huku ni kujigeyza kuwa madalali wa demokrasia,” amesema Mwabukusi.

Aidha, Mwabukusi amemtuhumu Mkurugenzi Mtendaji wa TCD, Bernadetha Kafuko, amewaita wanachama wa NCCR-Mageuzi kushiriki kongamano hilo, kinyume cha sheria bila kuwashirikisha viongozi wao.

“TCD inajaribu kuchomoa watu kwenye vyama bila kufuata kanuni, chama ni taasisi unapotaka kufanya jambo unawafuata viongozi. TCD inachagua wanachama wa kawaida inawaambia wewe kiongozi wa NCCR njoo kikaoni. Tuna barua ya namna hiyo mtu anaambiwa wewe kiongozi uje. Chama hakina taarifa za kongamano ila mwanachama anazo,” amesema Mwambukusi.

Mwabukusi amesema, Kamati Kuu ya NCCR-Mageuzi, imeagiza wanachama wake walioko safarini kuelekea Dodoma kushiriki kongamano, warejee.

“Kinachoendelea Dodoma ni ubunifu wa baadhi ya watu ndani ya TCD, wanafanya hivi kwa nia ya kutweza na kubagaza demokrasia ndani ya nchi yetu,” amesema

“Kamati Kuu imeelekeza wajumbe waliotoka mikoani kuhudhuria warejee walikotoka. Hatutahudhuria wala kushiriki na hatutajifunga na chochote kitakachoendelea mpaka pale mapendekezo yetu yatakapofanyiwa kazi,” amesema Mwambukusi.

Mtandao huu umemtafuta Kafuko kwa simu, ili kuoata ufafanuzi wa madai hayo, ambaye amesema yeye sio msemaji wa taasisi hiyo.

“Naomba umpigie Mwenyekiti wa TCD, atakupa ufafanuzi wote, mimi sio msemaji mkuu wa taasisi,” amesema Kafuko.

1 Comment

  • Asanten.nccr.chadema endereen ivyo ivyo matokeo yake ni majuto kwenu kuvuja kwa pakacha nafuu kwa chama tawala

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!