Saturday , 25 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa NCCR-Mageuzi yasusia uchaguzi Muhambwe, yampa ujumbe Rais Samia
Habari za Siasa

NCCR-Mageuzi yasusia uchaguzi Muhambwe, yampa ujumbe Rais Samia

Edward Simbeye, Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma
Spread the love

 

CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimetangaza kutoshiriki Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Muhambwe mkoani Kigoma, kwa maelezo kwamba dosari zilizojitokeza katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2020, hazijafanyiwa kazi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Hatua hiyo imetangazwa leo Ijumaa tarehe 2 Aprili 2021, na Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma NCCR-Mageuzi, Edward Simbeye, wakati anazungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

Uchaguzi mdogo katika Jimbo la Muhambwe umeitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC), baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo (CCM), Atashasta Nditiye, kufariki dunia tarehe 12 Februari 2021.

Simbeye amesema kuwa, mapendekezo waliyotoa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, hayajafanyiwa kazi, hivyo chama hicho hakina imani kushiriki kwenye uchaguzi wa Muhambwe, kwa kuwa chombo kinachousimamia (NEC), haikijafanyiwa mabadiliko.

“Baada ya uchaguzi wa 2020 tulisema NCCR tunahitaji muafaka wa kitaifa, tuliishauri Serikali kwamba ni vyema muafaka wa kitaifa ukapatikana sababu utaamua hatma ya Taifa letu juu ya kitu kinachoitwa katiba mpya, tume huru na maridhiano ya kisiasa na kiuchumi.

Hivi vyote havijafanyika tena, upinzani hawajakaa kuzungumza kinachohusu hatma ya Watanzania, maendeleo na siasa ya Kitanzania, tunaendaje kwenye uchaguzi tukiwa katika hali hii?” amehoji Simbeye.

Kwa mujibu wa ratiba ya NEC, uchaguzi huo mdogo utafanyika tarehe 2 Mei 2021, fomu za uteuzi zinatolewa kuanzia tarehe 28 Machi hadi 3 Aprili mwaka huu, kisha kampeni zitaanza tarehe 4 Aprili hadi 1 Mei, 2021.

Simbeye amesema kuwa, licha ya utawala kubadilika baada ya aliyekuwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, kufuatia kifo cha Dk. John Magufuli, bado hawana imani na mazingira ya uchaguzi.

“Kuna msemo wa Kiswahili unasema sumu haijaribiwi kwa kuonjwa, Watanzania walikuwa wakitaka tume huru ya uchaguzi, tumembadilisha rais ndio, lakini hatujabadilisha tume kuwa huru, hatujazingatia maoni ya Watanzania ya kutaka katiba mpya na tume huru,” amesema Simbeye

Dk. Magufuli alifariki dunia akiwa madarakani, miezi mitano baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania tarehe 5 Novemba mwaka jana, baada ya kushinda kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Mwanasiasa huyo alifariki dunia tarehe 17 Machi 2021, kwa ugonjwa wa mfumo wa umeme wa moyo, katika Hopsitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam. Mwili wake ulizikwa nyumbani kwao Chato mkoani Geita, tarehe 26 Machi 2021.

Simbeye amesema NCCR-Mageuzi haitashiriki uchaguzi wowote, hadi ushauri wao utakapofanyiwa kazi, huku akimuomba Rais Samia kukaa mezani na wadau wa siasa kwa ajili ya kumaliza tofauti zilizopo.

“Hatutashiriki uchaguzi mdogo wa Muhambwe na mwingine wowote mpaka muafaka wa kitaifa upatikane, sasa tunachohitaji sio kutibu maumivu ya uchaguzi, tunahitaji kutibu vidonda vya uchaguzi, na kutibu ni kukaa chini pamoja wadau wote . Sasa bado nchi imevimba, ina maumivu ya uchaguzi uliopita,” amesema na kushauri Simbeye:

“Hakuna chochote ambacho sisi kwa maoni yetu kitaenda kubaidlika, lazima tufanye mabadiliko makubwa ambayo muafaka wa kitaifa, tunamuomba rais arudi azingatie maoni tunayompa.”

1 Comment

  • Asante nccr izo ni dariri za kukataa tamaa usio mueza usishindane ikiwezakana ungananae na wala sio dhambi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia aagiza iundwe kamati ya pamoja ya Mawaziri mradi wa BBT

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewaagiza mawaziri kuunda kamati...

Habari za Siasa

Rais Samia apangua makatibu tawala mikoa, ateua Kamishna DCEA

Spread the loveALIYEKUWA Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Gerald...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

M/kiti bodi ya wadhamini Chadema afariki dunia

Spread the loveMWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Demokrasia na...

Habari za Siasa

Zitto: Nikifa Ado atavaa viatu vyangu

Spread the love  KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe...

error: Content is protected !!