December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NCCR-Mageuzi wajinoa Dodoma

Spread the love

CHAMA cha NCCR- Mageuzi, kimejifungia jijini Dodoma, tayari kunoa makada wake muhimu watakaoshriki uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa Oktoba mwaka huu. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinasema, takribani “wabunge watarajiwa,” mia moja na kumi (110), wako mjini humo, kuhudhuria mafunzo ya siku mbili, yenye lengo la kujinoa kwa ajili ya uchaguzi huo.

Wengine waliohudhuria mkutano huo, ni katibu mkuu wa chama hicho, Elizabeth Mhagama; mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu; mbunge wa Rombo, Joseph Selasini na Kamishena wa mkoa wa Mara na ambaye kabla ya kujiunga na chama hicho, alikuwa kada maarufu wa Chadema wilayani Tarime, Mchungaji Elias Nyangabona.

Antoni Komu akikabidhiwa kadi ya NCCR- Mageuzi na James Mbatia

Katika orodha hiyo, yupo pia wakili mashuhuri wa mahakama kuu anayefanyia kazi zake katika mikoa ya Mbeya na Arusha, Boniface Mwambukusi; mkuu wa kitengo cha uenezi na mahusiano wa chama hicho, Edward Simbeye, Kamishena wa chama hicho na ambaye alikuwa diwani wa Kata ya Kinondoni (Chadema), Mustafa Muro na wabunge wa Viti Maalum, Joyce Sokombi na Suzana Masele. 

Mkutano huo unafanyika katika ukumbi wa Africa Dream, uliyopo eneo la Area D na unahudhuriwa na karibu viongozi wote wakuu wa chama hicho, wakiongozwa na mwenyekiti wake, James Mbatia.

Akifungua mkutano huo, Mbatia alisema, chama chake, kinaingia katika uchaguzi huu, ili kuhakikisha kinapata wabunge wa kutosha, ili kubadilisha nchi kwa kuipatia Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  

Alisema, “tunaingia kwenye uchaguzi huu mkuu, tukiweka kipaumbele chetu katika kupata idadi kubwa ya wabunge ili kuweza kushinikiza kupatikana kwa Katiba Mpya.”

Aliongeza, “tunafanya hivyo kwa kuwa Katiba Mpya ndio takwa la wananchi, walilolieleza kupitia Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na kuasisiwa na Tume ya Rais, iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba.

“Tunataka Katiba Mpya kwa kuwa ndio hitaji la sasa la taifa letu. Tunakwenda kwenye uchaguzi huu, tukiweka kipaumbele chetu kwenye eneo hilo.”

Joseph Selasini akikabidhiwa kadi ya NCCR- Mageuzi na James Mbatia

Kwa mujibu wa waandaji wa jumuiko hilo, mkutano wa “wabunge” – watia nia wa NCCR- Mageuzi, katika uchaguzi ujao wa Oktoba – umelenga, pamoja na mambo mengine, kuweka mikakati ya ushindi katika uchaguzi huo.

NCCR- Mageuzi kinaingia katika uchaguzi huu mkuu kwa mara ya kwanza, kikiwa imara tokea kiliposhindwa vibaya kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, kufuatia kuibuka kwa mgogoro mkubwa kati ya Kamati Kuu (CC) na aliyekuwa mwenyekiti wake, Augustine Mrema.

Katika mgogoro huo ambao uliishia kwa Mrema kuondoka chama hicho na kujiunga na Tanzania Labour Party (TLP), wabunge kadhaa, akiwamo aliyekuwa katibu wa NCCR- Mageuzi, Mabere Marando, walishindwa kutetea viti vyao.

Joyce Sokombi (kulia) akiwa na mwanachama mwengine wa NCCR- Mageuzi,

Uimara wa sasa wa NCCR- Mageuzi, unatokana na hatua yake ya kuwanasa waliokuwa wasisi wake, hasa Antony Komu na Joseph Selasini.

Akizungumza katika mkutano huo, Susan amesema amejipanga kwenda kugombea Ubunge jimbo la Ilemela Mkoa wa Mwanza na ana imani ataibuka mshindi.

Jimbo hilo kwa sasa linaongozwa na Angelina Mabula wa CCM ambaye ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

error: Content is protected !!