November 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NCCR-Mageuzi: Hatukutarajia Rais Samia awe kama Magufuli

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

CHAMA cha siasa cha upinzani nchini Tanzania cha NCCR-Mageuzi kimesema, hakikutarajia kama Rais wa sasa wa Taifa hilo, Samia Suluhu Hassan angekuwa na msimamo kama wa mtangulizi wake, Hayati John Magufuli kuhusu usitawi wa demokrasia. Anaripoti Kelvin Mwaipungu…(endelea).

Wamesema, Hayati Magufuli alizuia shughuli za kisaisa zinazotambulika kisheria na bnaada ya Rais Samia kuingia madarakani wangepata ahueni ya kufanya siasa kwa mujibu wa Katiba na sheria.

Hayo yamesemwa leo Jumanne, tarehe 10 Agosti 2021 na Naibu Katibu Mkuu wa Bara wa NCCR-Mageuzi, Anthony Komu wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, Ilala jijini Dar es Salaam.

Komu amesema, Tanzania ni nchi ya vyama vingi na katika kusimamia hilo, kuna sheria ambazo zinatoa uhuru wa vyama kufanya siasa wakati wote lakini viongozi wa chama tawala- Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanazuia kinyume cha taratibu.

Anthony Komu, Naibu katibu Mkuu NCCR- Mageuzi

“Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Rais Maguguli alisema shughuli za siasa zisimame, katika hali hiyo ambayo hatukutarajia Rais wa awamu ya sita (Samia Suluhu Hassan) amekuja na utamaduni huohuo wa kusimamisha shughuli za siasa kinyume na katiba,” amesema Komu

“Tulienda kwenye uchaguzi mkuu 2020, ambao ulivurugwa kwa vyama vya upinzani kutopata wawakikilishi halafu Rais Samia anasema, wanaotakiwa kufanya shughuli za siasa ni wale waliochaguliwa, tunauliza waliochaguliwa wako wapi?”

Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati John Magufuli

Rais Samia, aliingia madarakani tarehe 19 Machi 2021, kufuatia kifo cha Rais Magufuli kilichotokea 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam na mwili wake, kuzikwa kijijini kwao 26 Machi 2021.

Rais Samia ametoa uhuru kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya ndani pekee au madiwani na wabunge kwenye maeneo yao ya uchaguzi huku mikutano ya hadhara akiipiga marufuku.

error: Content is protected !!