June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NCCR kindakindaki UKAWA – Wadhamini

Spread the love

CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimewakana viongozi wake wa juu akiwemo Katibu Mkuu, Mosena Nyambabe, waliotoa msimamo wa kushutumu mwenendo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) waliosema unakiua chama hicho. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea)

Msimamo huo umetolewa leo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya chama hicho, Mohamed Tibanyendera katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya chama, Ilala, Dar es Salaam.

“Dhamira ya Ukawa ni kushinda sio kugombea tu, ndio maana tunaangalia jimbo fulani lina uwezekano wa kupita kwa chama chetu? Kama haiwezekani tunawaachia wenye ubavu ili Ukawa ipite,” amesema Tibanyendera ambaye ni kitaaluma ni mwanasheria.

Amesema uongozi wa juu haujapokea malalamiko kwa kiongozi au wanachama wowote yanayohusiana na mwenendo wa Ukawa na kwamba viongozi waliotoka hadharani jana na kudai kuwa NCCR-Mageuzi kinatengwa na kujikuta kinadhoofika.

Nyambabe pamoja na Makamu Mwenyekiti Bara, Leticia Mussore na wajumbe kadhaa wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), waliitisha mkutano na kuwaambia waandishi kuwa chama kimenyimwa fursa ya kusimamisha wagombea zaidi ya 12 waliopata katika mgawanyo.

Amedai kwamba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeweka wagombea baadhi ya majimbo hayo. Kadhalika wakasema viongozi wa Ukawa hawajatimiza masharti mbalimbali ya kutekeleza katika kuimarisha muungano huo, udhaifu waliosema, “umekikosesha chama hicho fedha za kufanya kampeni ili kupata viti bungeni.”

Viongozi hao walifikia hatua ya kumlaumu Mwenyekiti James Mbatia kwamba amekuwa akiridhika kukidhoofisha chama na amejitokeza kuwa ndio msemaji wa Chadema kuliko kukitetea chama anachoongoza.

Walimtaka Mbatia afikirie hatima ya chama chao badala ya kujiegemeza kwenye Ukawa ambao mwelekeo wake ni wa kukijenga Chadema zaidi kuliko masuala mengine.

Lakini katika taarifa yake leo, Tibanyendera amesema Katiba ya chama iliyodurusiwa mwaka jana, ndio muongozo mkuu wa mwenendo wa chama na “hatuamini juu ya mtu anayekiuka katiba ya chama kuwa amefanya jambo jema.”

“Kilichofanyika na Katibu Mkuu pamoja na Makamu Mwenyekiti, ni ukiukwaji wa Katiba ya chama,” amesema katika sauti inayoonesha kwamba kunaibuka mvutano wa kiuongozi kwenye chama hicho.

Kwa kuwa mpaka alipokuwa anazungumza na waandishi hajapokea taarifa rasmi za malalamiko ya viongozi waliokutana jana na waandishi, na hajui wana lengo gani anachoweza kusema ni kwamba taarifa walizozitoa ni hisia binafsi na sio maoni ya chama.”

Amesema msimamo wa chama unatokana na vikao halali vya chama na kama mtu ana maoni, anaruhusiwa kuyatoa, kama ni ya chama mtu huyo anapaswa apate baraka za kichama. “Hawa hawakupata baraka za chama,” amesema.

Tibanyendera amesema Nyambabe ni mmoja wa wagombea ubunge wa chama hicho lakini hajawahi kusikika akilaumu chochote wala kutamka kujiuzulu.

Amesihi viongozi wa ngazi ya juu wajenge umoja katika chama na linapotokea tatizo, walishughulikie kwenye vikao halali.

Amesema bado wanauamini Ukawa. “Tunaamini katika Ukawa, hatutoki katika Ukawa na tutakuwa wa mwisho kujitoa Ukawa, tofauti za kimtazamo ni suala la kawaida,” amesema.

“Ukiona hivi ujue demokrasia inakua nchini na uelekeo wa kukitoa chama tawala inaelekea kutimia na uhakika unaonekana,” amesema.

Kamishna wa chama hicho mkoani Tanga, Ramadhan Manyeko ambaye alishiriki mkutano wa jana, leo amesema mbele ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini kuwa msimamo wake ni kuendelea kushiriki UKAWA kwa sababu hakujua kilichokuwa kizungumzwe alipoitwa na Katibu Mkuu Nyambabe.

“Niliitwa na katibu mkuu lakini kwenye ule mkutano sikushiriki kutoa hata neno na nilishangaa kusikia yaliyokuwa yakizungumzwa pale mkutanoni… nilijiridhisha kuwa haukuwa msimamo wa chama bali watu binafsi,” amesema.

Nyambabe alifanya mkutano na waandishi kwenye Hoteli ya Landmark, Ubungo. Hakueleza maendeleo ya kampeni jimboni Serengeti, mkoani Mara ambako alipitishwa kugombea kuwakilisha UKAWA.

Juzi Mbatia akiwa Hoteli ya Millenium Kijitonyama, alishutumu mbinu za CCM kuhujumu Ukawa lakini akasema wamezibaini na hazitafanikiwa kwa sababu Ukawa unaimarika siku hadi siku na kuwa tishio pekee la utawala wa CCM.

error: Content is protected !!