June 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NBS: Pato la taifa limeongezeka

Spread the love

OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) leo imeeleza kuongezeka kwa pato la taifa kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2015 (Julai hadi Septemba). Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dk. Albina Chuwa amesema, kwa mujibu wa ripoti ya taarifa za pato la taifa, pato hilo limeongezeka kwa asilimia 6.3 ikilinganishwa na asilimia 5.4 ya miezi hiyo mwaka 2014.

Chuwa ametaja sababu ya pato kuendelea kukua kwamba ni kutokana na fursa zinazotolewa na serikali katika sekta za uchumi, kilimo, viwanda, elimu, afya, ujenzi, mawasiliano, maji, umeme, uchimbaji wa madini na vitu vingine.

Pia, ametaja vyanzo vya uchumi ambavyo vimeonesha kutoyumba kwa uchumi wa nchi kuwa ni pamoja na mauzo ya nje ya nchi ambayo yaliongezeka kwa asilimia 3.3 na thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje kupungua kwa asilimia 0.58.

“Hii ni dalili nzuri kwa uchumi unaokua kwa kuwa bidhaa nyingi na huduma zitakuwa zinapatikana ndani ya nchi,” amesema Chuwa.

Shughuli nyingine za kiuchumi zilizokuwa kwa kasi kubwa kwa mwaka 2015 ni pamoja na ujenzi kwa asilimia 17.6, uchukuzi na uhifadhi asilimia 10.6, uendeshaji serikali na ulinzi asilimia 10.6 na uchimbaji wa madini na kokoto asilimia 8.0.

Huku shughuli za kiuchumi zilizoshuka kwa kasi ni, kilimo, uzalishaji viwanda, umeme, biashara za jumla na rejareja, habari na mawasiliano, fedha na bima zilishuka kwa asilimia 3.0 ukilinganisha na mwaka 2014.

Chuwa pia amezungumzia pato la taifa la Kenya kwamba limekuwa kwa asilimia 5.8 kwa mwaka 2015 ikilinganishwa na asilimia 5.2 ya mwaka 2014.

Nakwamba, jumla ya thamani ya pato la taifa kwa bei za miaka husika katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba 2015 ni shilingi trilioni 71.7 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 6.9 kwa mwaka 2015 tofauti na asilimia 6.5 ya mwaka 2014.

“Hivyo, maoteo ya pato lataifa kwa mwaka 2015 yanayotolewa na Wizara ya Fedha na mipango yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 89.1 za mwaka 2015 ikilinganishwa na shilingi trilioni 79.4 ya mwaka 2014,” amesema Chuwa.

error: Content is protected !!