January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NBC yatoa mifuko 920 ya saruji, madawati 100 kuboresha elimu Mara, Mtwara

Spread the love

 

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imetoa msaada wa mifuko ya saruji 920 (sawa na tani 46) yenye thamani ya sh milioni 21 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili katika shule ya Sekondari Kiriba iliyoko Halmashauri ya wilaya ya Musoma Mkoani Mara sambamba na msaada wa madawati 100 katika shule za Sekondari Libobe na Tangazo zilizopo Mkoani Mtwara ikiwa ni hatua ya benki hiyo katika kuunga mkono juhudi za serikali pamoja na wananchi katika kuboresha elimu hapa nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mtwara … (endelea)

Wakizungumza kwenye hafla za kukabidhi misaada hiyo zilizofanyika mwishoni mwa wiki katika shule hizo, Meneja wa benki ya NBC Tawi la Musoma Bi Sophia Lyimo pamoja nae Meneja wa Benki ya NBC tawi la Mtwara Bi Editha Mwakatobe walisema misaada hiyo inalenga kuunga mkono jitihada ambazo tayari zinaendelea kuonyeshwa na serikali pamoja na wananchi katika maeneo husika kwa kuboresha miundombinu ya elimu.

“Mifuko hii 920 ya saruji tunayoikabidhi hii leo ni kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa mabweni mawili ya wasichana na wavulana katika Shule hii ya Sekondari Kiriba. Wananchi na serikali wamefanikisha ujenzi wa maboma ya mabweni na sisi tumeona tuwaunge mkono kwa kuwapatia saruji ili waweze kufanikisha mpango huu muhimu unaolenga kuwasaidia wanafunzi wanaosoma hapa wasitembee umbali mrefu kufuata elimu,’’ alisema Bi Lyimo.

Aliipongeza serikali kwa kutoa kiasi cha sh mil 60 kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule hiyo.

Akizungumza kwenye hafla kama hiyo ya kukabidhi madawati 50 kwa ajili ya shule ya sekondari ya Libobe iliyopo wilayani  Mtwara, Meneja wa Benki ya NBC tawi la Mtwara Bi Editha Mwakatobe alisema msaada ni sehemu ya msaada wa madawati 100 unaotolewa na benki hiyo kwa shule hiyo Sekondari pamoja na sekondari ya Tangazo iliyopo wilayani humo pia, lengo likiwa ni hilo hilo la kuhakikisha wanasaidiana na serikali pamoja na wananchi katika kuboresha mazingira ya elimu nchini.

“Lengo letu ni kuhakikisha ndoto za watoto hawa kielimu zinafikiwa na pia kumuunga mkono Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassani katika utoaji wa elimu bora. Kwa hiyo tunakabidhi madawati na viti hivi kwa ajili ya wanafunzi hawa kwa kuwa ni  furaha ya NBC kuona watoto wanaondokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili hasa katika swala la elimu” alisema Bi Mwakatobe.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada wa viti na madawati kwa ajili ya Sekondari ya Lipobe, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Bw Dunstan Kyobya  pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa msaada huo alisema serikali imejipanga kuhakikisha inamaliza changamoto za kielimu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo benki hiyo huku akitolea mfano shule hiyo ambayo inaendelea na ujenzi wa madarasa mawili na ofisi ya walimu kupitia fedha kiasi cha sh mil 40 zilizotolewa na serikali.

“Msaada huu umekuja wakati muafaka kwasababu mahitaji ni viti na meza 72 kwa ajili ya wanafunzi watakaonza masomo mapema mwakani…tunawashukuru sana benki ya NBC kwa kutuunga mkono baada ya kuwapelekea maombi yetu na wao hawakusita kutusaidia. Huu ni mwanzo tu kwa kuwa wiki ijayo Benki ya NBC tena watatukabidhi msaaada kama huu kwa ajili ya Sekondari Tangazo,’’ alishukuru.

Zaidi Bw Kyobya aliiomba benki hiyo kuangalia uwezekano wa kufungua tawi au huduma ya uwakala katika eneo hilo ili kusaidia upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi hao ambao licha ya kupata fedha nyingi kupitia kilimo cha zao la korosho bado wamekuwa wakibabiliwa na uhaba wa huduma za kifedha.

Kwa upande wao wakuu wa shule hizo waliishukuru benki ya NBC kwa namna ilivyoguswa katika kuchangia sekta ya elimu ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa, mabweni na msaada wa madawati kwa kuwa jitihada hizo zimekuwa zikisaidia kuongeza kasi ya serikali na wanachi wanaojitolea kuboresha utoaji wa elimu hapa nchini.

“Binfasi nimefarijika sana kwa msaada huu kutoka NBC na kwa kweli bado tunahitaji wadau wengine wajitoe kusaidia kama walivyofanya benki hii. Tulituma maandiko ya kuomba msaada kwao na tunashukuru waliyapokea na kuyafanyia kazi na matokeo yake ndio haya tunayaona hii leo tunapokea msaada huu mkubwa wakilenga kuunga mkono jitihada za wananchi na serikali yetu…asanteni sana NBC,’’ alisema Mtani Shadrack, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kiriba, wilayani Musoma.

error: Content is protected !!