Saturday , 3 June 2023
Home Habari Mchanganyiko NBC yakabidhi gawio la 20 bilioni kwa wanahisa wake
Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi gawio la 20 bilioni kwa wanahisa wake

Spread the love

SERIKALI imepokea kiasi cha Sh. sita bilioni kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ikiwa ni sehemu ya gawio la kiasi cha Tsh 20 bilioni ambayo benki hiyo imetenga kwa ajili ya wanahisa wake  kufuatia faida iliyopata katika kipindi cha mwaka 2022. Serikali inamiliki asilimia 30 ya hisa za benki hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi amekabidhi gawio hilo kwa Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu aliyeiwakilisha serikali katika hafla fupi ya makabidhiano hayo iliyofanyika mapema leo Jumatano jijini Dar es Salaam na kuhudhrliwa na wadau mbalimbali kutoka serikali na maofisa waandamizi wa benki hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mchechu pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kipindi cha mwaka 2022, aliwasilisha salamu za Rais Samia Suluhu ambae pia aliipongeza benki hiyo huku akitoa wito kwa taasisi na mashirika yenye umiliki wa umma kuhakikisha yanatimiza wajibu wao wa kuwasilisha gawio litokanalo na faida za uendeshaji wa shughuli zao kwa serikali.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu (wa tatu kushoto) akipokea mfano wa hundi yenye thamani ya Sh. 6 bilioni kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (kushoto) ikiwa gawio la mwaka 2022 kwa Serikali ambayo inamiliki asilimia 30 ya hisa za benki hiyo. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NBC, Dk. Elirehema Doriye (wa pili kushoto) pamoja na maofisa waandamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

“Serikali inafurahishwa na utendaji ulioimarika wa Benki ya NBC. Sisi kama wanahisa, tunafurahi kuona uwekezaji wetu unatoa matunda. Gawio la Sh. 6 bilioni ambalo Serikali imepokea leo litaongeza ukubwa wa kapu letu la makusanyo ambayo yamekuwa yakielekezwa katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo hususani ile ya kimkakati. Hivyo naipongeza sana Benki ya NBC kwa mafanikio haya…hongereni sana,’’ amesema Mchechu.

Aidha, Mchechu ametumia fursa hiyo kuwasilisha agizo la Rais Samia Suluhu anayataka mashirika na taasisi nyingine zenye umiliki wa umma kuhakikisha zinatimiza wajibu wao wa msingi wa kuwasilisha gawio kwa serikali.

“Anachosisitiza Rais kwenye hili ni kwa taasisi hizi kutimiza wajibu huu kwa fedha zitokanazo na faida iliyopatikana tu na si kwa taasisi hizi kukopa mahali popote ili kulipa gawio. Hata hivyo, taasisi zitakazoshindwa kutimiza wajibu ipo haja ya viongozi wa taasisi hizi kujitafakari ili kuona kama kweli wanastahili kuendelea kuongoza taasisi zisizo tengeneza faida kwa taifa,’’ amesema.

Awali akizungumza kwenye tukio hilo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NBC, Dk. Elirehema Doriye, ameeleza kuwa mafanikio na mwenendo chanya wa benki hiyo unathibitisha imani kubwa waliyonayo wateja kwa kwa Benki hiyo.

“Tuna furaha kusalia katika dhamira yetu ya kufikia malengo yetu muhimu katika kupanua nyayo zetu na kuwekeza katika teknolojia ili kuboresha uzoefu wa wateja wetu. Faida yetu ya kabla ya kodi ilikua kwa asilimia 36 hadi Sh. 81.9 bilioni kutoka Sh. 60 bilioni mwezi Desemba 2021.’’

“Ongezeko hili la faida ndilo linatuwezesha kutoa Sh. 20 bilioni kama gawio kwa wanahisa wetu; leo, tunafurahi kukabidhi hundi ya Sh. 6 bilioni kama gawio kwa mwaka 2022. Tunatazamia mustakabali wenye matumaini zaidi huku pia tukiwa tunaendelea kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wetu,” amesema Doriye.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri kwa taasisi za fedha kama Benki ya NBC kustawi huku pia akiipongeza Bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo pamoja na wafanyakazi kwa jitihada kubwa walioifanya hadi kufikia mafanikio hayo.

“Utendaji kazi wa Benki unaonyesha mazingira bora ya biashara ambayo yalituruhusu kuwafikia wateja wetu kwa urahisi. Tutaendelea kuwekeza katika teknolojia, kupanua nyayo zetu na kuboresha huduma zetu zetu ili kukidhi na kuzidi matarajio ya wateja wetu,” amesema Sabi.

Akizungumzia uwajibikaji wa benki hiyo kwa jamii Sabi amesema katika kipindi cha mwaka 2022 benki hiyo ilifanikiwa  kukusanya pesa kiasi cha Sh. 200 milioni kupitia mbio za NBC Dodoma Marathon 2022 ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi.

“Benki ya NBC ndiyo mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania ‘NBC Premier League”, ambayo inazalisha ajira na kusaidia uwezeshaji na ushirikishwaji wa kifedha.’’

Ameongeza Sabi huku akibainsha kuwa benki hiyo iliongeza matawi matano mapya katika kipindi cha mwaka wa 2022 huku wakala wa mtandao wa benki hiyo “NBC Wakala” ukikua kwa asilimia 82 kutoka mawakala 5,121 hadi 9,525.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Magunia 731 ya bangi yakamatwa, mamia ya hekari yateketezwa Arumeru

Spread the love  MAMIA ya magunia ya madawa ya kulevya aina ya...

Habari MchanganyikoTangulizi

Bosi NIC apandishwa kizimbani, akabiliwa na mashitaka 365

Spread the love  ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Taifa...

Habari Mchanganyiko

Serikali yakabidhi eneo la mahakama ya Afrika ya haki za binadamu

Spread the loveSerikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa...

Habari Mchanganyiko

Udhamini wa NMB mikutano ya ALAT wafikia 1.2 bilioni

Spread the loveBENKI ya NMB imeendelea kufanya kazi kwa karibu na Asasi...

error: Content is protected !!