WAKALA wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), umetangaza nauli mpya kwa watumiaji wa mabasi yaendayo haraka, zitakazoanza kutumika kuanzia tarehe 16 Januari 2023. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Nauli hizo mpya ambazo zimeongezeka kwa wastani wa Sh. 100, zimetangazwa leo tarehe 14 Januari 2023 na DART kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Taarifa ya DART imeeleza kuwa, nauli hizo mpya zimeidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA).
Nauli ya Kimara hadi Kivukoni, Gerezani na Morocco imeongezeka kutoka Sh. 650 hadi 750, wakati Gerezani hadi Muhimbili ikiwa Sh. 750 badala ya 650. Nauli ya Kutoka Kimara hadi Mbezi imepanda kutoka Sh. 400 hadi 500. Kimara hadi Kibaha (Sh. 650 hadi 700), Kimara hadi Mloganzila (Sh. 650 hadi 700).
Aidha, nauli kwa wanafunzi haijapanda, imebaki Sh. 200.
MwanaHALISI Online imeutafuta uongozi wa DART kwa njia ya simu, kwa ajili ya kupata sababu za ongezeko hilo, bila mafanikio.
Leave a comment