January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nasubiri kuona ya Obasanjo Tanzania

Rais Mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo

Spread the love

BABA wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alikuwa mlezi wa kweli wa taifa hili. Alikuwa mtu huru. Aliweza kukataa jambo lolote lile ambalo halikuwa na maslahi kwa taifa.

Kwa maneno yake mwenyewe aliwahi kusema, “Watanzania wanataka mabadiliko. Wasipoyaona ndani ya CCM watayatafuta nje ya chama hiki.

Ilikuwa mwaka 1995, kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, ubunge na udiwani. Alisema, CCM siyo mama yake. Anaweza kuondoka na kujiunga na chama kingine.

Kumekuwa na upepo wa wanasiasa kuhama hama vyama vya upinzani kwenda chama tawala au chama tawala kwenda vyama vya upinzani kutokana na sababu mbalimbali, lakini wote husahau jambo moja muhimu, kutuonesha ubaya wa vyama hivyo kabla hawajatoka kwa vitendo.

Rais Mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, amefanya kile ambacho Nyerere alikionesha au kukifanya na huenda angeshakifanya kama Mungu angempa pumzi angalau miaka kumi tu mbele tangu kifo chake; kuchana kadi na kujiondoa kwenye chama kilichompa urais.

Rais huyu ambaye kwangu anaweza kuwa shujaa kwa kitendo hicho, alimlima rais wa sasa barua kuhusu mwenendo wa nchi yao.

Kama kawaida ya Waafrika walianza kumpikia majungu na kupanga kumfukuza uanachama. Obasanjo hakusubiri, akajiondoa.

Watanzania wengi wamekuwa wakifanya siasa za woga, kuogopa mamlaka zao. Wako tayari waitetee mifumo mibovu iliyomo ndani ya vyama vyao kwa sababu tu wanalinda vyeo vyao. Kwa mfano, mbunge wa CCM anaweza kutetea muundo wa serikali mbili, si kwa sababu anaupenda bali amelazimishwa na akienda kinyume, anaweza kufukuzwa uanachama na kupoteza ubunge wake. Bora liende. Liwalo na liwe.

Wapinzani pia wamekuwa watu wa kufuata mikumbo na sio watu wa kusimamia mawazo yao. Nafahamu kuna wakati ni lazima ukitetee chama chako lakini si kila wakati. Profesa Mwesiga Baregu alipokuwa mjumbe wa Tume ya mabadiliko, aliombwa na chama chake ajiondoe katika tume hiyo kwa kile kilichoitwa kukosa weledi.

Alipokuwa anajibu tuhuma hizo, Prof. Baregu alisema, “Nikiambiwa nichague nchi na chama nitachagua nchi.”

Hawa ndio wazalendo. Watu wasiokuwa katika siasa kwa maslahi yao, ila kwa maslahi ya taifa. Tutawasikia lini kina Alhaji Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa wakitoa maonyo juu ya rushwa na ufisadi unaoendelea nchini kama kweli wao walikuwa wasafi?

Lini watawatisha viongozi wa chama na serikali kuenenda katika misingi mizuri na hata kutishia kufanya kama alivyofanya Obasanjo? Au wote sio wasafi?

Jaji mstaafu Joseph Warioba tumemwona akijaribu lakini hajapiga hatua zaidi. Bado anaiogopa CCM. Frederick Sumaye naye amejaribu kidogo mpaka akasema wakiendelea na rushwa hii atajiengua katika chama hicho lakini yawezekana anatafuta huruma ili aupate urais anaohangaikia kwa udi na uvumba.

Tunawataka viongozi ndani ya nchi yetu watakaosimamia maslahi mapana ya nchi. Watakosimama kuonesha njia kwa vijana tunaokua. Vijana wengi sasa wananuka rushwa hata kabla hawajapata ofisi. Sijui wakipata itakuwaje!

Viongozi wapo kimya, wastaafu hawakemei hali hii, wamenyamaza kimya. Nachelea kusema wote sio wasafi, walijichafua wakiwa madarakani na hivyo wanaogopa siri zao kugundulika. Kama kuna wasafi basi sio wazalendo wa kweli wa taifa letu. Namtafuta Obasanjo wa Tanzania.

Mwandishi wa Makala haya ni Y.M. LULYEHO anapitakana (DUCE-DSM) no: 0788936187

error: Content is protected !!