October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nassari, Qambalo wajiunga CCM, wajikomba 

Willy Qambalo (kulia) na Joshua Nassari muda mchache kabla ya kujiunga rasmi na CCM

Spread the love

JOSHUA Nassari, aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki mkoani Arusha na Willy Qambalo, aliyekuwa Mbunge wa Karatu, wote kutoka Chadema, wametimkia CCM. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Akizungumza baada ya kujiunga na CCM, Nassari amesema, ataonekana hana akili kama atampinga Rais John Magufuli.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano tarehe 8 Julai 2020, baada ya kupokewa na Kheri James, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya CCM (UVCCM) mkoani humo.

Nassari amesema, aliingia kwenye siasa ili aijenge Tanzania, na kwamba aliyoyapigania kwa sasa anayatekeleza Rais Magufuli.

“Yako mengi tutayazungumza huko mbele, nilichagua kuingia kwenye siasa ili kuijenga nchi, ndio maana nilichimba visima, nilinunua vitanda Hospitali, sasa yote ambayo nilikuwa napigania JPM (Dk. John Pomba Magufuli) ameyafanya, nikimpinga nitaonekana sina akili,” amesema Nassari na kuongeza:

“Haikuwa kazi rahisi kufanya haya maamuzi ya kuja CCM, yale yote mnayotaka kuyasikia na kuyaona kutoka kwangu mtayasikia na kuyaona hata kama sio leo, sababu kubwa iliyonileta CCM ni kwa kuwa naipenda nchi yangu,” amesema Nassari.

Nassari amewaomba radhi Watanzania watakaokwazwa na uamuzi wake wa kujiunga na CCM, huku akiweka bayana kwamba hatojali watu watakaoibuka na kumsema vibaya kufuatia hatua yake.

“Watanzania wanaokwazwa kwa kuona nimeingia CCM ambao walitamani kuendelea kuniona upinzani, naomba mnisamehe. Siwezi kuendelea kuwa mnafiki, roho yangu imekataa.

“Nimeamua kuiweka nchi yangu mbele, najua wapo watakaonitukana, watakaosema hili na lile kisa mimi kuhamia CCM lakini sitojali,” amesema Nassari.

Aidha, Nassari ameishukuru Chadema kwa kumlea kisiasa, na kueleza kwamba ameshakiandikia barua chama hicho, kukijulisha uamuzi wake wa kujiunga na CCM.

“Siku zote nafanya siasa za kiungwana, nimeshawaandikia barua Chadema, na ukweli naishukuru Chadema ilinichukua nikiwa mdogo, nawashukuru kwa kunilea. Nitakuwa mjinga kama sitoikumbuka historia,” amesema Nassari.

Qambalo ambaye amekuwa Mbunge wa Karatu kwa vipindi vitatu mfululizo, amesema amemua kujiunga na CCM, ili kuunga mkono utendaji wa Rais Magufuli, aliyemfananisha na hazina ya Taifa.

“Nimekuja nyumbani sababu huko nyuma sikuwa mwanasiaa sana, tangu nimeingia bungeni nimejifunza mambo mengi sana, lakini la pili juu ya huyu bwana anayeongelewa na watu wengi Rais Magufuli ni hazina kwa Watanzania, amefanya mambo mengi sana,” amesema Qambalo.

error: Content is protected !!