Saturday , 22 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Nassari awang’ang’ania ‘maswahiba’ wa rais
Habari za SiasaTangulizi

Nassari awang’ang’ania ‘maswahiba’ wa rais

Joshua Nassari, Mbunge wa Arumeru Mashariki (katikati). Kushoto ni Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea
Spread the love

MBUNGE wa Chadema katika jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, ametinga kwa mara ya pili kwenye ofisi za taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuwasilisha ushahidi wa madai ya rushwa yanayowakabili wateule wa Rais John Magufuli, anaandika Faki Sosi.

Akiongozana na mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, Nassari amesema amefika  tena Takukuru baada ya kumsiki mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo akiahidi kufuatilia madai yake hadi mwisho.

Alisema, “nimekuja tena hapa Takukuru kuwasilisha ushahidi mwingine usio na shaka dhidi ya mkuu wa wilaya ya Arumeru, Alexunder Mnyeti na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Meru, Christopher Kazeri.

Taarifa zinasema, viongozi hao wawili wa serikali, wanaonekana kwenye video iliyowasilishwa na Nassari Takukuru, wakishawishi madiwani kadhaa wa Chadema kukihama chama hicho kwa madai kuwa wanaunga mkono juhudi za Rais Magufuli katika “kunyoosha nchi.”

MwanaHALISI Online imeona sehemu ya mkanda wa video uliowasilishwa Takukuru. Ndani ya mkanda huo, kunaonekana Mnyeti na Kazeri wakishawishi madaiwani kuondoka Chadema kwa ahadi za kupatiwa fedha na ajira serikalini.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuingia kwenye ofisi za Takukuru, Nassari amesema, “Pamoja na matatizo yaliyopo kwenye taasisi hii, ikiwamo chombo hiki kuwa mikononi mwa rais, bado ninaamini maneno ya mkurugenzi mkuu kuwa taasisi yake itafuatilia suala hili hadi mwisho,” ameeleza Nassari.

Hata hivyo, Nassari amesikitishwa na hatua ya Rais Magufuli ya kumuacha Mnyeti katika wadhifa wake.

Amesema, “pamoja na ushahidi wote huu, bado Mnyeti yuko ofisini kana kwamba hakuna kitu. Kibaya zaidi, Mnyeti amekuwa akijigamba kuwa yeye ni swahiba wa rais na hakuna chochote kitakachofanyika.”

Aliongeza, “wapo watu waliosema, ni ngumu ‘kesi ya Ngedere kumpelekea Nyani. Yawezekana ndio maana Mnyeti bado yuko ofisini. Ninamuomba rais Magufuli, sheria ni msumeno. Ichinje kwa kadri inavyotakiwa.”

Naye Kubenea akizungumza katika mkutano huo alisema, “huu ni ushindi mkubwa sana kwetu. Kwa mara ya kwanza tumefanikiwa kuiweka serikali kwenye kona.”

Amesema, ushahidi uliwasilishwa na Nassari haina chembe ya mashaka na kwamba sasa Takukuru wanakabiliwa na kibarua kizito cha kupeleke shauri hilo mahakamani.

Kubenea ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Tamisemi amesema, “nimeshirikishwa katika kukamilisha sehemu ya kazi hii ya kitume. Hivyo basi, nitahakikisha kazi hii haiendi bure.”

“Tayari Nassari na madiwani wake wamekamilisha kazi yao. Ni jukumu la Takukuru sasa kuchunguza na kuwasilisha ushahidi uliopo mahakamani ili haki iweze kutendeka,” amesisitiza.

Naye ameungana na Nassari kushangazwa na hatua ya kuwaona watuhumiwa bado wakiwa ofisini.

Alisema, “tulitegemea hawa watu wangekaa pembeni ili kupisha uchunguzi. Tulitegemea ama wangekuwa wamechukua likizo kwa hiari au wamelazimishwa.

“Hii ni kwa sababu, wanasheria wanasema, vyombo hivi vya umma kama Takukuru vinapaswa kutenda haki na kuiridhisha jamii kuwa haki siyo tu inaweza kutendeka, bali inaonekana kuwa inatendeka. Kitendo cha Mnyeti na mkurugezi wake kuendelea kuwa ofisini, kinatia mashaka dhamira hiyo.”

Mnyeti na Kazeri wanadaiwa kuwashawishi madiwani wa Chadema kukihama chama chao ahadi ya kupatiwa nafasi za ajira serikalini.

Tarehe 2 Oktoba mwaka huu, Nassari aliongozana na wabunge wenzake wawili wa Chadema, Mchungaji Peter Msigwa na  Godbless Lema, kuwasilisha ushahidi unaowatuhumu Mnyeti na Kazeri kufanya biashara ya ununuzi wa madiwani.

Msingwa ni mbunge wa Chadema katika jimbo la Iringa Mjini na Lema ni mbunge wa Chadema katika jimbo la Arusha Mjini. Wote wawili wameathirika na biashara ya ununuzi ya madiwani inayodaiwa kuendeshwa na viongozi wandamizi wa chama tawala.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Askofu Wolfang Rais mpya TEC, Padri Kitima aula tena

Spread the loveBARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetambulisha safu mpya za...

Habari MchanganyikoTangulizi

Padre anayetuhumiwa mauaji ya Asimwe, asimamishwa

Spread the loveKanisa Katoliki Jimbo la Bukoba limemsimamisha kutoa huduma za kichungaji...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali yaahidi kushirikiana na Prof. Ndakidemi kuhamasisha zao la kahawa

Spread the loveSerikali imeahidi kuungana na Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick...

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

IMF yaimwagia Tanzania trilioni 2.4 kukabili mabadiliko ya hali ya hewa

Spread the loveShirika la Kimataifa la Fedha (IMF) jana Alhamisi limesema bodi...

error: Content is protected !!