Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Tangulizi Nape ataka utawala wa Rais Magufuli uchunguzwe
Tangulizi

Nape ataka utawala wa Rais Magufuli uchunguzwe

Spread the love

 

MBUNGE wa Mtama mkoani Lindi nchini Tanzania, Nape Nnauye ametaka uchunguzi maalumu ufanyike katika akaunti ya deni la Taifa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa awamu ta tano uliokuwa chini ya Rais John Pombe Magufuli. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Nape anayetokana na chama tawala- Chama Cha Mapinduzi (CCM), alitoa kauli hiyo jana Jumatatu, tarehe 9 Novemba 2021, bungeni jijini Dodoma, akichangia hotuba ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo uliowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba.

Mbunge huyo alisema katika kipindi cha miaka mitano hadi sita deni la Taifa limeongeza kwa kiwango kikubwa na uwazi haukuwapo, hivyo kutaka ufanyike ukaguzi wa akaunti ya deni hilo.

Alisema taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Waziri wa Fedha na Mipango na Kamati ya Bunge ya Bajeti, zinasema deni la Taifa limefikia Sh.64 trilioni na bado ni himilivu, ila anashangaa ongezeko la deni hilo katika kipindi cha serikali ya awamu ya tano.

“Naomba ufanyike ukaguzi kwenye akaunti ya deni la Taifa, katika kipindi cha awamu ya tano na ambapo uwazi haukuwapo, ili kujua kilikopwa nini, kilikwenda wapi, thamani yake nini, uhalisia wa miradi na thamani viwekwe mezani, ili kuiga mfano uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema.

Mbunge huyo alisema kuongezeka kwa deni la Taifa katika kipindi cha miaka sita, kunaifanya Serikali kulipa Sh.800 bilioni kila mwezi, hivyo kukwamisha shughuli zingine za kijamii.

Nape Nnauye, Mbunge wa Mtama (CCM)

“Mtakumbuka Serikali ya awamu ya tatu ilikopa dola bilioni 9 kwa miaka 10, awamu ya nne kwa miaka 10 dola bilioni 7 na Awamu ya Tano kwa miaka mitano hadi sita, dola bilioni 9, hili ni ongezeko kubwa sana, hivyo njia ya kubaini ukweli ni ukaguzi maalumu,” alisema.

Alisema bahati mbaya mkopo huo asilimia 40 ni mikopo ya kibiashara, ambayo moja ya sifa zao ni riba kubwa, lakini inalipwa kwa muda mfupi, hali ambayo inasababisha kila mwezi Serikali kulipa Sh bilioni 800 sawa na asilimia 44 ya makusanyo.

Alisema iwapo kasi itaendelea hivyo, ni wazi asilimia kubwa ya makusanyo itatumika kulipa madeni, hivyo kuathiri shughuli zingine za kutoa huduma.

Dk. Magufuli aliingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015 na kuhudumu hadi 17 Machi 2021, alipofariki dunia katika Hospitali ya Mzena, iliyopo Makumbusho jijini Dar es Salaam.

Mwili wake, ulizikwa nyumbani kwao Chato mkoani Geita tarehe 26 Machi 2021.

Aliyekuwa makamu wake wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliapishwa kuwa Rais tarehe 19 Machi 2021, kumalizia awamu ya tano ya kipindi cha pili iliyokuwa imeingia madarakani 5 Novemba 2020.

Katika mchango bungeni, Nape alisema pamoja na ukweli, kuwa namba zinaonesha deni linastahimilika, ila si vizuri kupuuza kwamba fedha zinazotumika kulipa madeni ni nyingi.

Alisema katika kuhakikisha hali hiyo haijitokezi, ni lazima mfumo aliokuja nao Rais Samia wa uwazi kuhusu anachokopa uwe endelevu, kwani kila mwananchi atapata welewa.

“Leo hii hata muuza mchicha anajua kuwa Serikali imekopa Sh.1.3 trilioni na zinakwenda kufanya nini, hivi ndivyo inavyotakiwa, ndiyo maana naomba ukaguzi ufanyike kwa kipindi cha awamu ya tano,” alisema.

Alisema iwapo mkopo wa Sh.1.3 trilioni umewekwa mezani itapendeza na mikopo hiyo ya kibiashara ikaguliwe, kwa kuwa Watanzania ndio walipa kodi.

Aidha, kuhusu kilimo alisema iwapo mpango unasema ni kujenga uchumi wa ushindani na shirikishi, alitarajia nguvu kubwa ielekezwe kwenye sekta yenye watu wengi ili kupata uhalisia.

Alisema hali ilivyo sasa, kilichowasilishwa hakina uhalisia, hivyo kuitaka Serikali kuja na mpango sahihi, kwani wabunge wengi wanawakilisha wakulima ambao ni asilimia 70 ya Watanzania.

Mbunge huyo alisema kilimo kinachangia asilimia 26 ya pato la Taifa, hivyo ni vema kuwepo miradi ya kielelezo ambayo itaonesha kuwekeza kwenye eneo hilo.

“Mapendekezo yangu, ni kuomba Serikali kuleta mpango unaogusa watu wengi, kwa kuweka fedha za kutekeleza angalau hekta 200,000 au 300,000 za mfano katika kilimo,” alisema.

Nape alisema pia anaomba kuwepo Mfuko wa Ruzuku kwenye mazao, ili siku Dunia ikitikisika kiuchumi nchi isiyumbe.

Mbunge huyo wa Mtama alikuwa Waziri kipindi cha Rais Magufuli kabla hajatumbuliwa na Rais huyo, baada ya sakata la aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuvamia kituo cha utangazaji cha Clouds.

Makonda alivania kituo hicho akiwa na askari wenye silaha usiku wa Machi 17, 2017, ambapo Nape akiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, aliunda Tume kuchunguza tukio hilo.

Lakini baada ya Tume yake kuwasilisha taarifa ikimbana Makonda huku akiahidi kuwasiliana na Mamlaka ya Uteuzi, Rais Magufuli alimtumbua na kubaki na ubunge.

Mara baada ya kutumbuliwa na kuibuka kwa kadhia mbalimbali za kisiasa ambazo hazikuwa nzuri, tarehe 10 Septemba 2019, Nape alikwenda Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam kumwomba radhi Rais Magufuli kwa yaliyokuwa yametokea.

Rais Magufuli alimsamehe na kumtaka kwenda kuendelea na majukumu yake pasina wasiwasi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

error: Content is protected !!