November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nape apiga ‘stop’ bei za bando kupanda

Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Tekinolojia

Spread the love

 

KAMPUNI za mawasiliano ya simu nchini zimetakiwa kutobadilisha bei za vifurushi hadi pale matokeo ya tathmini kuhusu gharama za utoaji huduma hiyo yatakapotolewa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Agizo hilo limetolewa leo Jumatatu, tarehe 21 Novemba 2022 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Nape amesema, matokeo ya tathmini hiyo inayoendelea, yatatolewa kati ya Desemba 2022 au Januari 2023.

“Kupitia TCRA tunafanya tathimini ambayo ya kawaida inafanyika kila baada ya miaka mitano, ilifanyika 2018 na sasa inafanyika 2022 na matumaini yetu Disemba itakamilika. Serikali inafanya mapitio ya gharama halisi ya utoaji hduuma za mawasiliano nchini na baada ya tathimini hiyo huwa inatolewa dira kama bei elekezi kwamba kutoka kiwango hiki na haki,” amesema Nape.

Nape amesema, 2018 ilifanyika tathimini ya gharama halisi ya utoaji huduma za mawasiliano nchini na ikapatikana bei elekezi kuanzisha Sh. 2.03 hadi 9.35.

Amesema, tathimini mpya ikifanyika bei za vifurushi itashuka kutokana na hatua mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuboresha huduma za mawasiliano, ikiwemo katika kodi.

“Ni matumaini kwamba tathimini itatupa muelekeo mzuri sababu kuna uwekezaji umefanyika, kuna hatua za kikodi tunachukua, kuna marekebisho kadhaa yanafanyika. Tathimini itatoa matokeo na matumaini yetu kwamba gharama zinaweza kushuka kwa kiasi fulani,” amesema Nape.

Katika hatua nyingine, Nape amesema Serikali italiimarisha baraza la Ushauri la Watumia Huduma za Mawasiliano la TCRA, ili litekeleze majukumu yake ya kudumisha mahusiano mazuri kati ya watoa huduma na watumia wa huduma za mawasiliano.

error: Content is protected !!