August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nani kawahonga Mwakyembe, Masaju?

Spread the love

MWAKA 1955 wakati mama yangu amebeba mimba yangu kulitokea jambo kule mkoani Mara katika Wilaya ya Tarime, ambalo halisahauliki miongoni mwa Wanyamongo wa Tarafa ya Ingwe na Wanyabasi wa Tarafa ya Inchage, anaandika Nyaronyo Kicheere.

Mimi sikuwepo, nilikuwa sijazaliwa, kwa hiyo nimehadithiwa kwamba wakati huo, Wanyamongo walikuwa na Mtemi wao waliyemwamini aliyeitwa Kibisa Omseti na ambaye aliishi katikati ya Mlima Turuturu na Bonde la Mto Tigite.

Nimeambiwa kuwa mwaka huo Wanyabasi walivuka mpaka na kwenda kulima katika eneo liitwalo Kwimamu ambalo ni katikati ya Turuturu, Mto Tigite na Monanka lakini Kibisa Omseti aliwazuia Wanyamongo kupigana nao.

Kibisa alisema “tiga baleme neho nde,” akimaanisha “waache walime mie nipo.” Wanyamongo walimwelewa mzee Kibisa kwa kuwa walikuwa wakimwamini na kumwogopa kwa hiyo waliacha ugomvi wakisubiri kuona matokeo yake.

Taarifa zinasema Wanyabasi walilima na kulimaga, wakalima na kulimaga na hatimaye ulimpokwisha mwezi itabalalya na kuingia mwezi kimusi wakaanza kupanda ulezi na mtama. Katika kuulizia nimeambiwa Itabalalya ni Januari na Kimusi ni Februari.

Baada ya Wanyabasi kupanda mazao ndipo kilipowapata kisebusebu na kiroho papo. Tunaambiwa mzee Kibisa alikwenda katika mashamba yao na kuchomeka kijiti, hatuambiwi kilikuwa kijiti cha mti gani sababu si muhimu.

Kilichotokea baada ya Kibisa kuchomeka kijiti hicho kwenye mashamba ya Wanyabasi ndicho muhimu kwa sababu magugu fulani tunayoyaita Egetoha yaliota kwa nguvu na kufunika mazao yote. Wanyabasi wakapalilia na kurudia lakini wapi! Kwenye mavuno hawakuambulia hata punje!

Kibisa Omseti alijua anafanya nini tofauti na Waziri wetu wa Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, ambao wanamwachia rais wetu mpendwa na Mwenyekiti wa chama chetu anabwabwaja mikutanoni na kuumbuka.

Wanyamongo walikuwa na Kibisa Omseti anawalindia mali zao sijui siku hizi wanamtumia nani na sisi wanaCCM na Watanzania kwa ujumla tunao Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Sheria ndio wa kufanya kazi ya kutulindia mali zetu na viongozi wetu.

Na sisi hatujui watu hawa wawili wamehongwa na nani kiasi kwamba wameacha kazi yao muhimu ya kutumia katiba na sheria za nchi kuwalinda viongozi wetu na mali za taifa hili. Mimi siwaelewi kabisa Mwakyembe na Masaju inapotolewa hutuba yenye viashiria vya udikiteta.

Serikali iliyopo madarakani ni ya CCM, serikali hiyo inayolalamikiwa na vyama vya upinzani kuwa ina viashiria vya udikiteta halafu kiongozi wetu mpendwa wa CCM na serikali akitoa hotuba inasheheni kauli zinazoashiria udikiteta! Hili halikubaiki.

Yaani sisi tunakana kwamba Mwenyekiti wetu wa CCM siyo dikiteta na kwamba serikali yetu siyo ya kidikiteta. Lakini viongozi wetu wanaolipwa mishahara wawashauri watendaji serikalini wanaacha kufanya kazi hiyo, nasi tunaonekana tuna viashiria vya udikiteta.

Mtu unajiuliza kama iliwezekanaje Rais wetu mpendwa, John Magufuli, akatoa hotuba mbaya namna ile Zanzibar wakati wapo watu wenye elimu ya sheria walioajiriwa kumwongoza kiongozi wa nchi asitamke maneno yanayokinzana na katiba.

Ina maana Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Sheria hawakuiona ile hotuba ya rais kabla haijasomwa? Au ina maana Dk. Mwakyembe na Masaju hawamjui Mwandishi wa hotuba wa Rais ni nani nao wakamshauri? Mbona hawarekebishi kama alivyofanya Mzee Kibisa?

Au hawakumuuliza mwandishi huyo wa hotuba wa Rais kama siku hiyo Rais angezungumzia nini kwenye hotuba yake?  Kwanza huyo Mwandishi wa hotuba wa Rais ni nani huyo asiyejua jinsi ya kumsetiri kiongozi wake? Sasa sikiliza anavyovisema Rais wetu kwenye hotuba zake:

Kwanza kwamba Polisi wasiwe rafiki na raia. Rais wetu mpendwa alisema haya alipozungumzia vifo vya maskari polisi jijini Dar es Salaam. Hivi kweli Polisi wanaohubiri siku zote juu ya Polisi jamii na ulinzi shirikishi leo waachane na urafiki na raia?

Mwandishi wa hotuba wa Rais ndiye aliyeandika haya au Rais wetu aliteleza na kusema hivyo wakati maneno hayo hayapo kwenye hotuba? Na je Mwakyembe na Masaju wamefanya nini baada ya maneno haya kutamkwa na Rais wetu? Kwa nini wameachia tu!

Pili kwamba mtu anayezuia watu kuchota maji kisimani huko Zanzibar azamishwe kisimani! Hivi mtu akizamishwa kisimani atapona? Kama anayezamishwa kisimani haponi maana yake ni kwamba atakufa kwa kuuawa kwa kuzamishwa kisimani! Utawala wa sheria unaruhusu haya?

Au utawala wa sheria unataka mtu anayetuhumiwa akamatwe, ahojiwe, ashitakiwe, upelelezi ufanyike, ushahidi ukipatikana shauri liendeshwe mahakamani na akipatikana na hatia afungwe. Na kama kosa ni kubwa ndipo auawe kwa kunyongwa siyo kuzamishwa kisimani.

Tatu Raisi wetu mpendwa kanukuliwa akihutubia mikutanoni eti Polisi wakikamata magari yanayovunja sheria za barabarani wayakamate na kuyapeleka kituoni na kuyatoa matairi halafu eti wenyewe wakija kuulizia kesho yake waambiwe magari hayo yalikuja kituoni hivyo hivyo!

Hivi hiki ni nini kama si kuhamasisha uhasama kati ya raia na walinzi wao wa amani? Hii ni kauli ya namna gani kama siyo kauli ya kuchochea askari kuwadhulumu raia mali yao bila kuwapeleka kortini? Kauli ya kiongozi wa nchi inayochochea uhalifu inaachiwa hivi hivi bila kuondolewa? Kwenye hotuba!

Mbona Dk. Mwakyembe na Masaju hawafanyi chochote kurekebisha hali kama alivyofanya Kibisa wa Nyamongo! Sisi Wanyamongo tulisaidiwa na mwenzetu Kibisa Omseti ambaye aliwaachia wahalifu wakafanya uhalifu wao baadae akawaadhibu kwa kuchomeka kijiti mashamba yakaota egetoha/magugu badala ya ulezi .

Fikiria ninyi wenzangu eti Rais wetu mpendwa kahutubia wananchi na kusema Maalim Seif hapaswi kuandikiwa au kutiliwa saini nyaraka za kumwezesha kupata pensheni au kusafiri nje kwa sababu aliukataa mkono wa Rais wa Zanzibar, Dakitari Ali Mohamed Shein.

Jamani, Mwakyembe, Masaju na Mwandishi wa hotuba wa Rais hamkuliona hili kwenye hotuba mliondoe? Yaani Rais wetu hawezi kutofautisha kati ya Shein anayetoka chumbani kwa mama yetu Mwanamwema amejifunga kanga yake akienda bafuni kuoga na Rais wa Zanzibar?

Rais wa Zanzibar anaongozwa na katiba, sheria, kanuni na taratibu za Zanzibar na asipotekeleza chochote kwa mujibu wa sheria na katiba anashitakiwa. Rais wetu mpendwa Magufuli hajui hili kweli. Ali Mohamed Shein anaweza kugoma kusaini nyaraka lakini Rais wa Zanzibar hana ujanja, hawezi kugoma.

Mbona hotuba za Magufuli zina viashiria vya udikiteta halafu watu walioajiriwa kuhakikisha viashiria vya udikiteta havionekani wanaachia mambo tu matokeo yake Rais wetu mpendwa anaonekana dikiteta hata kama hana nia ya kuwa dikiteta?

Yaani nimefika mahali nashindwa kuorodhesha yote yanayofanya kiongozi wetu mpendwa John Pombe Magufuli aonekae dikiteta kama yale ya kusitisha siasa mpaka 2020 na kuwapoteza watu walioimba kwenye mkutano wa CCM kwamba wana imani na mtu fulani.

Sasa kiongozi wa nchi anaposema eti angewapoteza watu tena wanachama wenzake wa CCM ana maana gani? Watu wanaopotezwa wanakuwa hai? Watu wapotezwe kisa kuimba kuwa na imani na Lowassa? Au Lowassa ndiye kawahonga Mwakyembe na Masaju?

Hapana, hapana. Kuna mtu kawahonga Mwakyembe na Masaju ili wahakikishe hotuba ya Rais haisomwi na kuboreshwa na lengo ni kumharibia kiongozi wa nchi aonekane dikiteta.

Makala hii imetoka katika Gazeti la MwanaHALISI la tarehe 12Septemba mwaka huu.

 

 

error: Content is protected !!