July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nani ataangushiwa gogo CCM?

Mawaziri Wakuu wastaafu, Edward Lowassa (kushoto) na Fredrick Sumaye wakisalimiana kwenye mkutano wa CCM

Spread the love

NDANI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumedoda. Hakuna kinachosonga mbele. Mambo hayaendi. Kinachoonekana machoni mwa wengi, kutalamaki vituko na mtikisiko.

Mradi wa “Katiba Mpya,” ambao ungetumika kama mtaji mkuu wa kukiingiza chama hiki Ikulu kwa mara nyingine, tayari umegonga mwamba.

Kisa: Serikali na chama tawala, kushindwa kuwaunganisha waliokuwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, katika kutafuta sauti ya pamoja kwa maslahi ya taifa. Walitanguliza maslahi ya chama chao, jambo ambalo lilisababisha Katiba Mpya kukwama.

Ni kinyume na Jaji Joseph Sinde Warioba, aliyeongoza Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na tume yake kuwa na wajumbe wenye mitizamo tofauti kuhusu masuala yaliyopaswa kujadiliwa, aliweza kuyaunganisha makundi yote na hatimaye kutoka na msimamo wa pamoja.

Jaji Warioba, aliongoza tume iliyokuwa na mtazamo tofauti hasa upande wa Zanzibar. Kwa muda mrefu sasa, wananchi wa Zanzibar wameshikamana na kushinikiza kuwapo mfumo mpya wa Muungano.

Wamekuwa wakihoji mfumo wa serikali mbili kwa kusema umenyang’anya mamlaka Zanzibar, mamlaka ambayo ilipaswa kuwa nayo katika mambo kadhaa yakiwemo yasiyo ya Muungano.

Kwamba wamekuwa wakilalamika kuwa Muungano ulivyoanzishwa na unavyoendeshwa, umezorotesha umoja na mshikamno Visiwani na Tanganyika.

Hivyo basi, kama Katiba Mpya ingepita na kufanikiwa kumaliza matatizo ya Muungano, ingekuwa mtaji mkubwa kwa chama hiki kurejea madarakani katika uchaguzi mkuu wa mwishoni mwa mwaka huu. Kwa kweli, ungekuwa ufunguo muhimu wa kuingia ikulu.

Lakini kwa kuwa Katiba Mpya imekwama, kwa sababu ya CCM kulazimisha mambo, chama hiki hakiwezi kupata njia ya mkato kurejea ikulu.

Hatua ya Waziri Mkuu wa Jamhuri, Mizengo Pinda, kuwaghilibu Waislamu kuwa kitawapatia Mahakama ya Kadhi, jambo ambalo limeshindikana, nacho ni kigingi kingine ambacho kitaifanya CCM kupata wakati mgumu kujitetea.

Aidha, kitendo cha Muungano wa vyama vinne vilivyojipa jina la “UKAWA,” kuendelea kukaa kimya bila kumtaja mgombea wao wa urais, ni kiza jingine kwa CCM.

Hii ni kwa sababu, chama hiki kilijipanga kumshambulia na kumsawajisha mgombea wa UKAWA. Kilitaka kisimtangaze mgombe wake bila kutangazwa mgombea wa UKAWA. Ukimya wa UKAWA ni “msiba kwa CCM.”

Kila uchao, CCM kinapiga mahesabu ya nani awe mgombea wake wa urais. Awe mwenye kashfa au sifa nzuri? Awe mwenye mvuto au uvundo? Awe kutoka serikalini kulikoandamwa na rushwa, ufisadi, malalamiko na tuhuma za kushindwa kuwajibika au kutoka nje ya serikali ya Jakaya Kikwete? Kwa hakika, hali bado tete.

Kashfa za ufisadi ni doa kuu kwa chama hiki kuelekea Oktoba. Pamoja na serikali kuwasafisha watuhumiwa, mbele ya wananchi watuhumiwa hao ni wachafu na wasiofaa.

Mbaya zaidi, watuhumiwa hao ndio wenye nguvu hata ya kupenya kwenye urais. Kashfa za kifisadi zinazotajwa ni pamoja na Richmond, wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na katika akaunti ya Escrow. Wananchi wanazikumbuka na wanawakumbuka watuhumiwa.

Tumaini la CCM yetu ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), inayoongozwa na Jaji Damian Lubuva. Inategemewa kufanya mambo ili uchaguzi wa Oktoba uote mbawa. Lengo chama kipate muda wa kujipanga. Kipate ushindi.

Lakini, kwa jinsi upinzani ulivyong’amua mapema na kupigia kelele jambo hili na kwa yale yanayotokea nchi jirani ya Burundi, hakuna dalili za NEC kuiponya au kuipunguzia maumivu CCM. Kitaamua kuingia hivyo hivyo katika uchaguzi, litakalotokea, itakabiliana nalo hivyo hivyo.

Kwa msingi huo, nauona mwisho wa CCM umefika. Kilichobakia, chama changu kijiandae kisaikolojia kuondoka Ikulu.

error: Content is protected !!