August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nani anawatisha viongozi wa dini na wanaharakati?

Spread the love

UTAWALA wa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli unadaiwa kuwatia hofu viongozi wa dini, wanaharakati na asasi za kiraia waliokuwa na ujasiri wa kuikosoa serikali katika tawala za awamu zilizopita, anaandika Pendo Omary.

Madai haya yanaibuka kufuatia viongozi wa dini na wanaharakati kukaa kimya katika kipindi hiki ambacho kamata kamata na ufunguaji wa mashtaka dhidi ya watu wanaooneka kukosoa mwenendo wa serikali ya awamu ya tano ukipamba moto.

Kabla ya utawala wa awamu hii ilikuwa ni kawaida kwa asasi za kiraia kama Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na viongozi wa dini mbalimbali kujitokeza kuikemea serikali kila mara mambo yanapoenda ndivyo sivyo.

Akitoa maoni yake kuhusu hali ya sasa ya nchi na uhuru wa kutoa maoni kwa wananchi, Yericko Nyerere mkazi wa Kigamboni Dar es Salaam ameeleza kushangazwa na ukimya wa makundi hayo katika kipindi hiki.

“Wako wapi ma‘sheikh’ waliokuwa wakilisemea taifa na watu wake mambo yaendapo mrama? Wapo wapi makasisi waliokuwa wakilisemea taifa na watu wake pindi mambo yaendapo mrama?

“Wapo wapi wanaharakati wa utaifa na makerubi wenye kulisemea taifa pindi mambo yaendapo mrama. Nani atuokoe?” amehoji Yericko

Naye Asha Amiri, mkazi wa jijini Dar es Salaam pia amesema; “hata viongozi wa dini na wanaharakati kwa sasa wanaiogopa serikali hii. Lakini pia wanahofia hata taasisi zao kufugwa na serikali na ukimya wao unajenga hofu zaidi miongoni mwa jamii.”

Serikali ya awamu ya tano imekuwa ikilaumiwa kuminya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni binafsi kama ilivyo matakwa ya Katiba ya Tanzania ibara ya 18 (a-c).

Uhuru wa kutoa maoni umekuwa ukiminywa katika vikao vya Bunge la Jamuhuri ya Muungano, mikutano ya hadhara na hata mitandao ya kijamii ambapo wengi wamekuwa wakikamatwa kwa madai ya kukiuka sheria ya makosa ya mtandao.

error: Content is protected !!