Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Nani aliyeomba kuzaliwa Tanzania?
Makala & Uchambuzi

Nani aliyeomba kuzaliwa Tanzania?

Spread the love

WAPENDWA sisi wote tumekutana katika nchi hii pasipo wenyewe kuridhia! Anaandika Mwalim Mkuu wa Walimu…(endelea).

Hakuna kati yetu aliyeomba azaliwe katika nchi hii ambayo sasa inaitwa Tanzania. Nani alimchagua mwenzake wakutane Tanzania?

Tumekutana katika nchi hii kama wengine walivyokutana. Au tumewakuta wenzetu au wenzetu wametukuta. Ndiyo kusema katika nchi hii na nchi nyingine duniani hakuna raia aliye na haki zaidi ya mwingine.

Hivyo haki sawa kwa wote ndiyo busara kuu kwa nchi zote. Nimesoma maneno yaliyoandikwa kwenye daladala moja kuwa, “Nimezaliwa bongo kwa bahati mbaya!”

Sijui alitaka azaliwe wapi lakini haya ni maneno ya mtu asiye na furaha na nchi yake. Leo tutafute sababu. Hakuna mahali unapoweza kupata.

Ni sisi wanadamu popote duniani ndiyo huikosea nchi! Maandiko yanasema baada ya kuumba vyote Mwenyezi Mungu alivitazama viumbe vyake na kuona kuwa, vyote ni vyema!

Sasa mtuambie enyi wacha Mungu, huu ubaya kati yetu uliumbwa na nani? Wapendwa haijapita miezi myingi tangu dunia itoke Winsor, Uingereza kushuhudia harusi ya kifahari ya mwana wa kifalme.

Mwanamfalme kumuoa yule mwanamke ilikuwa ni ufahari lakini yule mwanamke kuolewa na Mwanamfalme ilikuwa ni bahati. Kuwatofautisha wanadamu katika matabaka haiwezi kuwa ni kazi ya Mungu.

Kazi hii aliifanya mwanadamu na mpaka leo anaendelea kuifanya. Na sisi haijatupitia kando.

Hatuna fahamu kuwa duniani kote, kuna watu warefu kwasababu tu, kuna watu wafupi. Watu wanene wasingekuwapo kama wembamba wasingekuwapo.

Ndiyo maana kuna weupe kwasababu kuna weusi. Ni nani aliye zaidi kati ya hao? Badala yakusema sisi ni hatujui wanasema wale ni wapinzani.

Kama Kamusi Kuu ya Kiswahili inatafsiri mheshimiwa kuwa ni mtu maarufu maana yake ni kwamba, waheshimiwa wapo kwasababu malofa wapo.

Fikra, mwenendo wa maisha na mwelekeo wa wale waliokuwapo kabla yetu ndivyo vimetufanya tuwe hapa na tuwe hivi tulivyo.

Fikra zetu za sasa, mwenendo wetu wa maisha na mwelekeo tulionao sasa ndivyo vitakavyoifanya Tanzania ya kesho. Kabla ya Tanzania kuwapo Tanganyika ilikuwapo.

Vivyo hivyo kabla ya Tanganyika kuwapo nchi yetu ilikuwapo. Tulipozaliwa sisi wengine tulikuta wazee wetu wakimsalimia Mwene wao kwa kulala chini kifudifudi.

Aliyepigwapigwa mgongoni na mkono wa Mwene alihesabiwa kati ya watu wenye bahati. Ndiyo kusema waheshimiwa
tangu zamani walikuwapo.

Lakini hawa walikuwa ni waheshimiwa wakuzaliwa. Leo duniani tuna waheshimiwa wakutengenezwa na wengine wakujitengeneza wenyewe.

Na hawa ndiyo waharibufu wa amani ya dunia yetu kwa kuleta dhana ya ubwana na utwana. Tunawaheshimiwa mpaka
wakubeep!

Ndugu Julius Kambarage Nyerere, alikuwa mheshimiwa kwa kuzaliwa katika ukoo wakichifu. Mheshimiwa wa kuzaliwa hujiona ni mtumishi wa watu wake na yule wakujitengeneza hujiona ni mtukufu anayepaswa kutumikiwa.

Na hawa ndiyo tulionao hapa duniani. Na wengine wamefika mahali wamekubuhu kwa unafiki. Wote tunasema nani kama mama? Mama ni mpendwa kwa watoto wake wote.

Lakini hatusikii watoto wake wakisema, “shikamoo mama mpendwa”. Wakisema shikamoo mama, wote tunajua huyo mama ni mpendwa wao.

Wako viongozi ambao hata siku moja wanapomtaja rais, hawaishii kusema rais wetu. Lazima waweke neno, ‘mpendwa’. Kwakukosa fahamu wanadhani wanamtukuza, kumbe wanaamsha hisia za kiongozi kutopendwa.

Haileti maana hata kidogo! Nilimuuliza rafiki yangu Kazadi Nyembwe, kwanini viwanja vingi vya ndege hasa vya kiafrika vinapotajwa lazima liwekwe neno ‘International?’

Akanijibu kuwa, ni kwasababu viwanja hivyo vingi siyo international. Uwanja wa ndege wa London, kule Uingereza kwa mfano, au Marekani ule uliopo Washington DC siyo lazima useme international.

Ni international wenyewe kama wenyewe. Ndugu Julius Kambarage Nyerere Rais wa kwanza wa nchi hii hakuhitaji neno mpendwa ili awe mpendwa.

Wanaohitaji neno mpendwa ni wale ambao hawapendwi. Stahili ya maisha yake na namna alivyoongoza vilimtambulisha kama mpendwa.

Nina hakika Mwalimu Nyerere angeitwa rais wetu mpendwa angemkemea mpuuzi huyo na upuuzi wake, tangu siku ya kwanza.

Mpendwa siyo vazi avae kila mtu. Wapendwa usibweteke na sifa za hadharani usijeingia katika mtego wake na watu wakakudharau kwa hilo.

Kichwani mwake wewe siyo mpendwa hivyo anakujengea mazingira udhani unapendwa. Kiongozi jasiri ni katika
kutenda kwa kuwatumikia watu. Hivi vijisifa vya bei rahisi
vinampunguzia mtu hadhi yake.

Anayekukosoa hadharani kwa haki akimtanguliza Mungu huyu ndiye mpendwa kwako. Anakujenga na kukuimarisha. Nyerere alikuwa mpendwa wa watu wake. Na kwa kuwapenda
watu wake aliwaundia Azimio la Arusha.

Azimio ambalo manyang’au walikuja wakaliua baadaye. Ni ndani ya Azimio la Arusha peke yake ndiyo kuna wananchi wenye furaha ya kweli na amani ya kweli kwasababu wanaishi kwa upendo, umoja na mshikamano.

Nje ya Azimio la Arusha ni hofu na mateso. Ni wakati sasa wananchi wahamasike, wachague mgombea atakayewaahidi kuwarejeshea urithi wao walioachiwa na Baba wa Taifa, Azimio la Arusha!

Atakayejali ustawi wao, badala ya kuweka mbele sifa, fedha na uroho wa madaraka. Wapendwa tutaendelea kuisoma historia ya nchi yetu wiki ijayo.

Kwasasa tuutazame upuuzi huu. Piga, ua, galagaza…..wanaopinga tutawafunga jela”. Ni maneno ya kipuuzi yaliyotamkwa na mtu mpuuzi.

Kama hupaoni anapotamkia, utajua ni mpuuzi tu amekwishalewa ‘mataputapu yake’ yaani pombe za kienyeji.

Rais Nyerere alisema, “Ukipewa kazi ya watu lazima ujiheshimu. Huwezi kuishi kihunihuni! Kafanyie uhuni wako
huko!” (siyo bungeni).

Wapendwa huyu amethibitisha kuwa wanachojali ni maslahi yao! Mtetezi wa masikini ni uchaguzi mkuu ujao. Unganeni!

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!