July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Namuona Kikwete ndani ya Magufuli

Spread the love

PIGA picha. Vuta hisia na kumbukumbu. Unakumbuka nini katika wakati kama huu, miaka 10 iliyopita? Mimi nakumbuka machache, yaliyotangulia na yaliyofuata baadaye. Nyakati zinashindana na kupingana; lakini zinafanana, anaandika Ansbert Ngurumo.

Nakumbuka nyakati za kushangilia “ari mpya, nguvu mpya, kasi mpya.” Ni shangilio la kaulimbiu. Naoanisha hilo na hili la sasa: “Hapa Kazi Tu!”

Nakumbuka enzi za Rais Jakaya Kikwete kuitwa “chaguo la Mungu?” Wengine walimwita “Tumaini lililorejea.” Wapo waliomuita, “Mkombozi mpya wa Tanzania.”

Wakati wakimwita Kikwete mkombozi, mtangulizi wake, Rais Benjamin Mkapa, alipewa majina yote mabaya. Mbabe. Katili. Mwizi. Aliambiwa ameharibu nchi. Hakuwa mtu wa watu.

Naona kama tumerudi nyuma miaka 10. Chaguo la Mungu sasa linapewa sifa za kijambazi, na huyu mpya, John Magufuli anaitwa “mpenzi wa Mungu.”

Kikwete aliyeshangiliwa na kusifiwa, sasa anazomewa na watu wale wale waliomsifu na kumtukuza. Wapo wanaodiriki kusema amekuwa mbaya kuliko Mkapa.

Miaka 10 baada ya kuahidiwa “maisha bora kwa kila Mtanzania” yakashindikana, sasa watu wanazungumzia “Tanzania Mpya” ya Rais Magufuli.

“Tanzania yenye neema inawezekana” ya Kikwete imetoweka ghafla. Hatujiulizi wanakotoa kaulimbiu tamu zinazoteka wananchi kwa muda, halafu zikawatesa baadaye.

Watu wale wale, mambo yale yale. Hatujifunzi. Hatukui. Hatuendelei kwa sababu hatutumii fikra bali hisia. Ndiyo maana tunadanganywa kirahisi.

Namkumbuka, Gado, mchora katuni mmoja katika magazeti ya Nation, Kenya. Alichora waandishi wa Tanzania wakiwa wanalamba viatu vya Rais Kikwete.

Tafsiri yake ilikuwa pana. Ilikera watawala na waandishi. Lakini ujumbe ulikuwa umefika, kwamba vyombo vyetu vya habari, badala ya kumhoji rais, vilimtukuza.

Leo tukitazama nyuma, tunajivuna kwa kazi tuliyofanya kumdekeza na kumfikisha Kikwete hapo alipo leo?

Yupo wapi Kikwete “rafiki wa vyombo vya habari” aliyehitimisha miaka 10 ya utawala wake bila kuruhusu zitungwe sheria za kulinda taaluma ya habari, waandishi, wamiliki wa vyombo vya habari na watoa habari?

Kwa sababu ya “urafiki huo” wakosoaji kadhaa wa serikali – waandishi na wanaharakati wengine, waliumizwa, waliteswa, na wengine waliuawa. Tuligawanyika ilipofika zamu yetu kujadili mateso na dhuluma hizi. Tulilewa madaraka yasiyo yetu.

Hayo ndiyo malipo ya mapokezi ya shangwe tuliyompa. Miaka mitano ya kwanza ya “ari mpya, nguvu mpya na kazi mpya” ilizaa miaka mitano mingine ya “ari zaidi, nguvu zaidi, na kasi zaidi.” Tuliona lakini hatukutafakari. Hatukushtuka!

Rais Kikwete huyu tunayemzomea leo, tulimharibu wenyewe. Na sasa tunamzomea wenyewe. Ni malipo ya “urafiki wa mashaka.”

Alipoanza ziara za kushtukiza katika ofisi na idara za serikali, tuliona ni mapinduzi makubwa sana. Alipopeleka wateule wake katika semina elekezi, halafu akawahutubia mwanzo hadi mwisho, tulisifu ubunifu mpya wa utendaji.

Hatukuhoji Kikwete amepata wapi maarifa ya ghafla anayojaribu kupandikiza kwa wasaidizi wake. Hatukuhoji alipata wapi uadilifu wa ghafla uliotufanya tumuone tofauti na mfumo wake.

Tulidanganywa na tabasamu lake. Tulimezwa na nguvu yake ya kuteka na kutumia vyombo vya habari kuimba sifa zake.

Hata vichwa vya habari vilibadilika. “Kikwete, we acha tu! Haijawahi kutokea.” Tulivyo wasahaulifu, Rais Magufuli naye alipoanza ziara za kushtukiza, tukarejea kule kule.

Rais Magufuli alipofuta semina elekezi, tukamuona shujaa, wakati sisi ndio tulishangilia semina hizo zilipoasisiwa na Kikwete miaka 10 iliyopita.

Kama vile Rais Kikwete alivyojaribu kujijenga kwa kumbomoa Mkapa, huyu naye anajijenga kwa kumbomoa Kikwete.

Ndiyo “majipu” haya yanayotumbuliwa. Ni “majipu” ya Kikwete. Ni “majipu” tuliyosababisha wenyewe kwa kushangilia matendo, kauli na vituko vya Kikwete.

Ni “majipu” ya makofi na vifijo vyetu. “Majipu” haya yanayotumbulia ni salamu kutoka juu. Ni dhihaka isiyo kifani kwamba chaguo la Mungu linatumbuliwa majipu!

Tunaponzwa na ukasuku wa “kuimbaimba” kaulimbiu za watawala.

Rais Magufuli wa leo hatofautiani na Rais Kikwete wa Machi 2006. Wote wanajua jinsi ya kucheza na hisia za wananchi.

Huyu anazungumza lugha ya wananchi waliokata tamaa. Anatoa matumaini mapya kwa wananchi maskini wanaokerwa na utajiri wa wengine, na walioaminishwa kwamba utajiri huo, kama usingekuwa mikononi mwa hao wachache, ungekuwa kwa maskini hao.

Wananchi wanashangilia jinsi anavyotumbua majipu kwa sababu aliyetanguliwa aliyalea. Lakini naye anasahau kwamba anajenga msingi wa yeye kutumbuliwa baadaye.

Kikwete tuliyemlea, aliyelewa sifa zetu, akafanya atakavyo, ameacha shida zinasotesa wananchi. Wanasema amewaachia shida. Wanalia. Rais Magufuli anatumbua majipu yake, yeye “anatumbua raha” alizojiandalia kwa miaka 10 mfululizo.

Na wakati wananchi wanashangilia utumbuaji wa majipu unaofanywa na rais, hawana muda wa kutafakari, ni akina nani wanateuliwa kuziba nafasi za wanaotumbuliwa.

Je, tunawajua na kuwaamini wanaoingizwa kuzina nafasi za waliotumbuliwa majipu? Mbona wengi wao ni watu waliokuwa karibu sana na Magufuli huko alikotoka? Mbona na huko kuna majipu mengi waliyosababisha kabla ya kuondolewa?

Yawezekana utumbuaji huu wa majipu ni fursa ya Magufuli kuchomoa watu wa Rais Kikwete na kuchomeka watu wake kwenye serikali?

Rais Magufuli si “rafiki wa vyombo vya habari” lakini ana uhusiano mzuri na baadhi yetu, na ameanza kujifunza jinsi ya kuishi na vyombo vya habari na waandishi ili wasimtumbue jipu.

Anajaribu kujenga kundi la watetezi wake. Ameshapata genge la washangiliaji. Anajaribu kugawa makundi ya wakosoaji. Nia yake ni moja. Aachwe apumue. Afanye atakalo. Tutajadiliana baada ya miaka mitano.

Na kwa wengine, Rais Magufuli hachekicheki kama Kikwete. Anafura. Anachukia. Anaamuru.

Mtu mmoja amesema, “kama mliumizwa na rais anayetabasamu, kwa huyu mtauawa wengi. Punguzeni makali. Huyu ni mkali.”

Sikiliza kauli na ahadi zake mbele ya majaji na mahakimu. Rejea hotuba yake bungeni kuhusu mustakabali wa katiba mpya. Jikumbushe hotuba yake ya Singida kuhusu vyama vya siasa.

Hakika, hii siyo Tanzania tunayotaka kujenga. Nchi ya waoga. Nchi ya wanafiki. Nchi ya kujipendekeza. Nchi ya kukubali bila kuhoji. Nchi itakayoangamia kwa ukimya wetu.

error: Content is protected !!