July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Namungo, Ihefu hakuna mbabe, Mbeya City, Kagera Sugar sare

Spread the love

 

MICHEZO miwili ya Ligi Kuu imemalizika kwa michezo yote miwili kutoka bila mbabe na kila timu kuondoka na pointi moja. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Ligi hiyo imeendelea hii leo mara baada ya kusimama kwa wiki tatu kupisha michezo ya kimataifa na maombelezo ya siku 21 kufuatia kifo cha Hayati John Magufuli aliyekuwa Rais wa Tanzania.

Katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya, wenyeji wa mchezo huo, Mbeya City walimaliza mchezo huo bila kufungana dhidi ya Kagera Sugar, huku Namungo FC wakitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Ihefu FC.

Kwenye mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, Ihefu walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa kiungo wake, Raphael Daudi kwenye dakika ya 23 na kufanya mchezo huo kwenda mapumziko kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili cha mchezo mwenyeji Namungo FC walirejea mchezoni na kufanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia kwa Ibrahim Mkoko dakika 61 na kufanya mchezo huo kumalizika kwa bao 1-1.

Kwa matokeo hayo ya michezo yote miwili Mbeya City wameendelea kusalia nafasi ya 16 wakiwa na pointi 21, Kagera Sugar wakiwa nafasi ya 13 na pointi 21.

Namungo wao baada ya kutoka sare wapo kwenye nafasi ya 10, wakiwa na pointi 28, huku Ihefu wakiwa nafasi ya 17 wakiwa na pointi 21 sawa na Mbeya City.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa michezo mitatu kuchezwa ambapo Biashara United itashuka dimbani dhidi ya Polisi Tanzania, JKT Tanzania dhidi ya Mwadui FC ambao wapo mkiani kwenye msimamo huo na mchezo wa mwisho utakuwa kati ya Azam FC dhidi ya Mtibwa Sugar.

error: Content is protected !!