May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Naibu waziri Gekul aipa somo TCRA

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imeitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhakikisha inasimamia vyema mfumo wa mtandao, ili kuhakikisha maudhui mtandaoni yanasalia yenye manufaa kwa watumiaji wote. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul, alipotembelea makao makuu ya TCRA, jijini Dar es Salaam.

Gekul alisema, TCRA inapaswa kuhakikisha makosa ya uvunjifu wa sheria za mtandao yanapungua huku akiwataka watumiaji kutumia vyema huduma hizo ili kuchagiza ukuaji wa uchumi na kuepuka matumizi ya mitandao yanayokiuka sheria za nchi, kanuni na maadili.

Katika ziara hiyo, naibu waziri huyo alipata fursa ya kujifunza namna mamlaka hiyo inavyofanya kazi.

Alilitoa wito kwa vituo vya utangazaji wa redio na televisheni nchini kuhakikisha vinarusha maudhui yanayozingatia maadili ya kitaifa badala ya kuweka kipaumbele urushaji maudhui yasiyofaa yanayotweza na kubomoa maadili na utamaduni wa jamii.

“TCRA tunashirikiana nao kwa upande wa wizara yetu kuhakikisha maudhui ambayo yanapelekwa na vyombo vya habari kwa wananchi yanakuwa sahihi lakini pia yanaangalia maadili ya Taifa letu. Nitoe tu rai kwa jamii, tunapotumia mitandao hii tutumie kwa namna ya kujenga na si kubomoa” alisema Gekul.

Naibu waziri huyo alihimiza umuhimu wa kuzingatia sheria na kanuni kwenye sekta ya utangazaji wa Redio na Televisheni, kwa ajili ya Umoja, Mshikamano na Maendeleo ya Nchi.

Katika ziara hiyo, Gekul alipata fursa ya kupokea wasilisho juu ya utendaji kazi wa TCRA na kushauriana na menejimenti ya mamlaka hiyo juu ya masuala mtambuka yanayoangukia katika wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo.

Akizungumzia kamati ya maudhui ambayo hufanya kazi na TCRA, Naibu Waziri alibainisha wajumbe wa kamati hiyo watateuliwa hivi karibuni baada ya waliokuwa wakihudumu katika kamati hiyo muda wao wa utumishi kutamatika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Kuwe Bakari alibainisha katika mitandao ya kijamii zimo fursa nyingi za maendeleo kwa ajili ya wananchi na Taifa na kuwatolea wito wananchi kuzitumia vilivyo fursa hizo ili kujinufaisha kiuchumi badala ya kutumia mitandao isivyopasa kinyume na Sheria za nchi.

“Kwa hiyo tunapoingia kwenye (cyber space) mtandaoni, ambayo ina nafasi kubwa sana ya kutengeneza ajira unaweza ukapata fursa ya biashara au kazi nzuri tu ya kufanya ukiwa ndani ya mtandao, badala ya kuingiza, kutengeneza au kuzungusha maudhui ambayo hayafai kwa Jamii” alisisitiza Kuwe.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Gekul alitembelea kituo cha Makumbusho ya Mawasiliano, Dawati la Huduma kwa Wateja wa Huduma na Bidhaa za Mawasiliano na Kituo cha Kufuatilia Maudhui.

error: Content is protected !!