October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Naibu waziri afariki dunia, Rais Samia amlilia

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa familia, Bunge na wananchi kufuatia kifo cha William Tate Ole Nasha. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Ole Nasha, aliyekuwa naibu waziri, ofisi ya waziri mkuu-uwekezaji, amefariki dunia jana usiku Jumatatu, tarehe 27 Septemba 2021, jijini Dodoma.

Ole Nasha ambaye ni mbunge wa Ngorongoro mkoani Arusha anakuwa mbunge wa tano kufariki dunia wa Bunge hili la 12 lililoanza Novemba 2020.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter jana Jumatatu usiku, Rais Samia ameomboleza kifo hicho akisema “Nasikitika kuwajulisha kuwa aliyekuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji Mhe. William Tate Ole Nasha amefariki dunia Jijini Dodoma.”

“Natoa pole kwa Spika Mhe. Job Ndugai, Wabunge, Familia na Wananchi wa Ngorongoro. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina.”

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Aidha, asubuhi ya leo Jumanne, Jaffar Haniu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu ametuma taarifa ya Rais Samia akizungumzia kifo hicho ambaye amemwelezea Ole Nasha kuwa alikuwa mchapakazi na hodari.

Amesema, katika sekta aliyokuwa mtumishi mwaminifu wa Serikali na pia ametoa mchango mkubwa katika ujenzi wa Taifa.

Rais Samia ametoa pole kwa Spika wa Bunge la Tanzania, Yustino Ndugai, wabunge, familia ya marehemu na wananchi wa Ngorongoro.

Ole Nasha aliwahi kuwa naibu waziri wa elimu, sayansi na teknolojia.

Wabunge wengine waliokwisha kufariki dunia na majimbo yao kwenye mabano ni, Elias Kwandikwa (Ushetu), Atashasta Nditiye (Muhambwe), Martha Umbulla (Viti Maalum) wote wa CCM na Khatibu Saidi Haji (Konde- ACT-Wazalendo).

error: Content is protected !!