September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mzumbe, Ghent kukuza ujasiriamali

Spread the love

SERIKALI mkoani Morogoro imeahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Chuo Kikuu Mzumbe katika kuboresha shughuli za ujasiriamali ili kupunguza umaskini, anaandika Christina Haule.

Hayo yamesemwa leo kwenye chuo hicho na Lucas Mwasaka, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Morogoro wakati akipokea mwongozo wa matarajio ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi wa utawala bora kupitia tafiti, elimu, uwezeshaji na teknolojia katika kuboresha ujasiriamali unaofanywa na Chuo cha Mzumbe kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ubelgiji.

Mwasaka amesema kuwa, chuo hicho kimeonesha nia ya kuinua shughuli za ujasiriamali kwa kuchimbua wavuna asali, watumiaji wa mazao ya misitu na kuinua suala la elimu kwa vijana jambo ambalo linaleta maana halisi na dhana za Rais John Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu’ na Tanzania ya viwanda kwa kuboresha shughuli za ujasiriamali.

Profesa Auleria Kamuzola Mratibu, mkuu wa mradi huo amesema kuwa, awamu ya kwanza ya mradi huo wa miaka 12 ulioanzishwa mwaka 2012 inatarajia kukamilika mwaka 2018 ikiwa na mafanikio mbalimbali ikiwemo kusomesha vijana saba shahada ya uzamivu katika vyuo vya nchini Ubelgiji ili kuweza kuelimisha wajasiriamali na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Prof. Kamuzola amesema, baadhi ya tafiti walizofanya katika awamu ya kwanza ya mradi zinaonesha kuwa licha ya Tanzania kuwa na sera ya kutunza maji na sheria ya maji iliyokuwa na kipengele cha watu wanaokaa karibu na maji kutunza vyanzo hivyo kupitia uongozi wa vijiji, baadhi ya vijiji havina katiba inayoviwezesha kukaa vikao na kutatua changamoto zinazojitokeza.

Amesema kuwa mradi huo unatarajia kufika nchi nzima ambapo kwa tayari wameshatuma watafiti katika mikoa mingine ya Simiyu na Iringa wakiangalia masuala ya utunzaji maliasili na maji.

Prof. Koenraad Stroeken, mratibu wa mradi huo kutoka Chuo Kikuu cha Ghent, Ubelgiji amesema, lengo la umoja wao ni kutaka kuanzisha kitu kizuri kitakachowafanya Watanzania kuhisi mafanikio yatokanayo na wao wenyewe na sio kwa ajili ya mtu kwa kuboresha bidhaa zao za ujasiriamali walizoanzisha.

error: Content is protected !!