May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mzindakaya kuzikwa Alhamisi Rukwa

Hayati Dk. Chrisant Mzindakaya

Spread the love

 

MWILI wa mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, Hayati Dk. Chrisant Mzindakaya (79), unatarajiwa kuzikwa Alhamisi tarehe 10 Juni 2021, nyumbani kwake Sumbawanga mkoani Rukwa. Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumanne, tarehe 8 Juni 2021 na Msemaji wa Familia wa Mzindakaya, Kapteni Mstaafu, Zeno Nkoswe, akitangaza ratiba ya mazishi hayo, mkoani Rukwa.

Mzindakaya alifariki dunia Jumatatu, tarehe 7 Juni 2021, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alikokuwa anapatiwa matibabu kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Nkoswe amesema, kesho tarehe 9 Juni 2021, mwili wa Mzindakaya utasafirishwa kutoka Dar es Salaam, kuelekea mkoani Songwe kwa ndege, kisha utasafirishwa kwa gari kuelekea mkoani Rukwa, kwa ajili ya taratibu za mazishi.

“Maiti inategemewa kuja kesho kwa ndege, kutoka Dar es Saalam mpaka Songwe na kutoka Songwe maiti italetwa kwa barabara kuja Sumbawanga. Tunategemea kesho jioni maiti ya marehemu Mzindakaya inaweza ikawa imeingia hapa Sumbawanga,” amesema Nkoswe.

Msemaji huyo wa familia ya Mzindakaya, amesema baada ya mwili huo kuingia nyumbani kwake, Alhamisi itafanyika ibada ya mazishi.

“Baada ya mwili kuingia nyumbani kwake, pengine kesho kutwa tutafanya ibada na tutafanya mazishi nyumbani kwake hapa tulipo,” amesema Nkoswe.

Mzindakaya alikuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 40, katika nyakati tofauti, kupitia majimbo ya mkoani Rukwa.(Ufipa Kusini, Sumbawanga Mjini, Nkasi na Kalambo).

Mwanasiasa huyo alizaliwa tarehe 31 Desemba 1940, mkoani Rukwa.

error: Content is protected !!