August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mzimu wa Escrow wamtesa Tibaijuka

Spread the love

WASIWASI ndiyo akili. Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia Profesa Anna Kajumulo Tibaijuka, Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini, kukataa kupokea kiasi cha dola za kimarekani 100,000 (zaidi ya Sh. 200 milioni za kitanzania), alizopewa kama zawadi, anaandika Charles William.

Prof. Tibaijuka alilazimika kujiuzulu nafasi yake ya Waziri wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Januari mwaka jana kutokana na kupokea kiasi cha fedha Sh. 1.6 bilioni kutoka kwa mfanyabiashara James Rugemarila kinyume na maadili ya utumishi wa umma.

Alijiuzulu baada ya kupokea fedha hizo katika akunti yake binafsi, ingawa fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya Shule ya Sekondari Baobab, ambayo ni mali yake.

Prof. Tibaijuka pia alipokea fedha hizo kama zawadi pasipo kutoa taarifa kwa mamlaka za serikali, jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Maadili ya Utumishi wa Umma Na. 12 (e) (I) ya mwaka 1995.

Akizungumza na wanahabari jana, Tibaijuka amesema alikuwa nchini Marekani ambapo alienda kupokea tuzo ya heshima ya maendeleo endelevu ya mwana wa Mfalme Khalifa bin Khalifa wa Bahrain inayotolewa na Umoja wa Mataifa (UN) lakini alikataa kiasi cha fedha kinachoambatana na tuzo hiyo.

“Tuzo imetolewa kwa kuthamini mchango mchango wangu nilipokuwa nikifanya kazi UN, pamoja na kuambiwa kuwa nimepokea mgao wa fedha za Escrow lakini wazungu hawasikilizi majungu,” alisema.

Prof. Tibaijuka aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Makazi (UN-HABITAT), kabla ya kuamua kujitosa katika siasa za Tanzania kwa kugombea ubunge katika Jimbo la Muleba Kusini, mkoani Kagera mwaka 2010.

“Sikuzichukua zile fedha kwasababu kama mnavyojua katika nchi yetu yanaweza kuibuka mengine….ingawa niliwambia kuwa katika mkoa ninaotoka (Kagera) kuna tetemeko la ardhi limetokea, watajua wenyewe watafanya nini,” alisema Tibaijuka.

error: Content is protected !!