August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mzimu mauaji ya Mabina waibuka tena Mwanza

Marehemu Clement Mabina aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mwanza

Spread the love

MGOGORO wa ardhi katika mlima wa kijiji cha Kanyama kata ya Kisesa Wilaya ya Magu uliosababisha Clement Mabina aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mwanza kuuwawa na wananchi wenye hasira kali mwaka 2012 limeibuka upya, anaandika Moses Mseti.

Tayari baadhi ya wananchi wameanza ujenzi wa ofisi ya Serikali ya kijiji hicho.

Itakumbukwa kuwa Mabina aliuawa tarehe 15 Desemba mwaka 2013 baada ya kudaiwa  kuanza ujenzi katika mlima huo huku akidaiwa kuwarushia risasi na kuua mtu mmoja miongoni mwa wananchi walioenda kumuhoji juu ya ujenzi huo.

Baada ya kurusha risasi, wananchi walikimbiza na kumshambulia kwa mawe, marungu na mapanga na kumsababisha umauti papo hapo.

Katika muendelezo wa mgogoro huo wananchi wa kijiji hicho wamesema wamefikia hatua ya kuanza ujenzi baada ya kijiji hicho kukosa ofisi kwa muda mrefu.

Kwa kipindi kirefu kijiji hakina ofisi, tumeamua kujenga ili tuweze kupata huduma kiurahisi. Kijiji chetu kimenyanyaswa na viongozi wa Serikali kwa muda mrefu,” amesema Julius Kasuka mwananchi wa kijiji hicho.

Wananchi hao pia wameituhumu familia ya marehemu Mabina kutumia nguvu ya kifedha ili kuwakandamiza kitendo ambacho walidai hawapo tayari kuuachia mlima huo hata kama ni kwa kumwaga damu.

Wamedai kuwa wamekuwa wakidanganywa kwamba mlima huo umeuzwa na viongozi wa Serikali ya kijiji (iliyopita) jambo ambalo sio la kweli kwani vikao zaidi ya vitatu vilivyokuwa vikiitishwa wananchi walikataa kuuza mlima huo.

Wamedai kwamba, baada ya marehemu Mabina kuona wananchi wa kijiji hicho wamegoma kuuza mlima huo, alianza kuwalaghai kwa fedha baadhi ya wananchi na kuitisha kikao kilichohudhuriwa na watu 80.

“Kikao kilichoitishwa na Mabina na kinachodaiwa kuuza mlima kilikuwa na watu 80 lakini kikao cha pili cha kupinga kuuzwa kwa mlima kilihudhuliwa na watu 160, hatuwezi kukubali watu wachache kwa njaa zao wauze eneo letu,” amesema Betha Sata.

Wananchi hao walikuwa wakitoa madai hayo mbele ya Hadija Nyembo, Mkuu wa Wilaya ya Magu katika mkutano uliofanyika kijijini hapo.

Yohana Gervas ambaye ni mwenyekiti wa kijiji hicho amesema wananchi wameanza ujenzi huo baada ya kuona watu wachache wanataka kujimilikisha mlima huo huku wananchi wakiwa hawana eneo la kujenga ofisi ya kijiji.

“Viongozi wa Serikali ya kijiji waliopita ndio walisababisha tatizo hili kwasababu hata vielelezo vya kuuzwa kwa mlima huu havipo na wananchi wamegoma kuuachia mlima wao,” amesema Gervas.

Kwa upande wake Judith Mabina, mke wa marehemu Clement Mabina amemuomba mkuu wa wilaya hiyo kuchunguza mgogoro huo kwani wao wana imani kuwa ndiyo wamiliki halali wa mlima huo baada ya marehemu muwe wake kuununua kihalali.

“Naomba ufanyike uchunguzi kwanza kwani hata tukizungumza sasa hivi hatutamaliza. Hizi ni fitna tu na yalifanyika makubaliano ya kujenga visima vya maji baina ya wanakijiji na mnunuzi,” amesema.

DC Hadija Nyembo ameomba kupelekewa nyaraka zote zinazohusu mgogoro huo na pande zote za mvutano huo huku akiwataka Wananchi wanaofanya ujenzi katika mlima huo kusitisha mara moja mpaka pale ufumbuzi utakapopatikana.

“Watu wanasema hawakubali kutoka kwenye mlima huo na wanadai ni bora wakafie jela. Jela sio sehemu nzuri, sipendi mambo ya Burundi (nchi) yotekee Magu tena katika kijiji cha Kanyama ili kionekane kina watu wakorofi,” amesema Nyembo.

error: Content is protected !!