May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mzee Mwinyi: Rais Samia ameanza vizuri, tumsaidie

Spread the love

 

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa awamu ya Pili wa nchi hiyo, Ali Hassan Mwinyi huku akimpongeza kwa kuanza utumishi wake vizuri. Anaripoti Hamis Mguta…(endelea).

Mazungumzo hayo, yamefanyika leo Jumatatu, tarehe 12 Aprili 2021, nyumbani kwa Rais Samia, jijini Dar es Salaam, ambapo Mzee Mwinyi, alimtembelea.

Mara baada ya mazungumzo hayo, Mzee Mwinyi amempongeza Rais Samia kwa kuanza vizuri majukumu yake ya kuongoza nchi.

Samia, aliyekuwa makamu wa Rais wa Tanzania, aliapishwa kuwa Rais tarehe 19 Machi 2021, akichukuwa nafasi ya Dk. John Pombe Magufuli, aliyefariki dunia 17 Machi 2021.

Dk. Magufuli alifikwa na mauti katika Hospitali ya Mzena, mkoani Dar es Salaam na mwili wake ukazikwa nyumbani kwao, Chato mkoani Geita.

Mzee Mwinyi amesema, amefika nyumbani kwa Rais Samia kumjulia hali, kumtia moyo na kumhakikishia kuwa yeye na wazee wenzake wapo tayari kutoa ushirikiano na kumsaidia wakati wowote watakapohitajika kufanya hivyo.

“Mama ameanza vizuri, ingekuwa ni nyimbo ningesema once more!!!, ameanza vizuri kabisa na kila mmoja ana furaha, kila raia unayemsikia anasema mama ameanza vizuri,” amesema Mzee Mwinyi aliyeongoza nchi kuanzia 1985-1995

“Tuliyekuwa nae tulikuwa na Rais mzuri sana, mzoefu wa mambo ya kiserikali, ametufanyia kazi nzuri sana, sasa kaacha mambo haya ghafla kamuachia mwenzie,” amesema

Mzee Mwinyi amesema, “sasa mama naye mwanadamu, atakuwa na yake na vile vile kuna mambo ambayo yameanzwa na mtu mwingine ambayo watu wanayataka wanayapenda, wanamshikilia Mama tunayataka haya tunayataka!!, tulieni tutayatekeleza haya, sasa hilo linafurahisha.”

Kiongozi huyo mstaafu, amewataka Watanzania kumuunga mkono Rais Samia, kwa kuacha balaa, ugomvi na fitina badala yake wawe na umoja, mshikamano na kufanya juhudi za kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

error: Content is protected !!