May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mzee Mwinyi: Magufuli amefanya mambo yaliyotushinda watangulizi wake

Rais John Magufuli na Rais Ali Hassan Mwinyi

Spread the love

 

RAIS Mstaafu wa Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi amesema, Hayati Rais John Pombe Magufuli (61), atakumbukwa kwa utekelezaji wa masuala yaliyoshindwa kufanywa na watangulizi wake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Chato … (endelea).

Mzee Mwinyi amesema hayo mara baada ya kumalizika kwa mida takatifu ya kumwombea Dk. Magufuli, iliyofanyika Uwanja wa Mpira wa Magufuli, wilayani Chato mkoani Geita , leo Ijumaa tarehe 26 Machi 2021.

Dk. Magufuli alifariki dunia tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam na mwili wake kuzikwa kijijini kwao Chato mkoani humo.

Mzee Mwinyi amesema, Dk. Magufuli alifanikiwa kutekeleza maagizo ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ya makao makuu ya Tanzania kuwa mkoani Dodoma.

Mzee Mwinyi amesema, marais waliomtangulia Dk. Magufuli, walishindwa kutekeleza agizo hilo kwa zaidi ya miaka 40.

Marais hao ni; yeye mwenyewe (Mzee Mwinyi), Hayati Benjamin Willium Mkapa na Jakaya Mrisho Kikwete.

“Jambo la kwanza nalo ni kubwa ni pale alipofanya kijana huyu alipoamua kutekeleza maagizo ya baba yetu wa taifa marehemu Mzee Nyerere, kijana huyu ameweza na kuamua kuhamia Dodoma, na kutekeleza jambo hilo kwa miaka miwili ambalo sisi wengine tulichukua miaka 40 bado hatujatekeleza,” amesema Mzee Mwinyi.

Rais John Magufuli akizindua kitabu cha Rais Mstaafu, Hayati Benjamin Mkapa, wengine ni wastaafu, Jakaya Kikwete na Ali Hassan Mwinyi

Mchakato wa Serikali ya awamu ya tano kuhamia Dodoma, ulianzishwa 2016 kwa wizara na taasisi mbalimbali kuanza kuhamisha ofisi zao kutoka Dar es Salaam, kwenda mkoani humo.

Mbali na hilo, Mzee Mwinyi amesema Dk. Magufuli amefanya mambo mengi ya maendeleo nchini Tanzania, katika kipindi cha muda mfupi.

“Si hilo tu, ndugu yetu huyu amefanya mambo mengi sana, yenye maslahi ya Tanzania, amefanya mambo makubwa mazuri ya maana, ameyatekeleza,” amesema Mzee Mwinyi.

“Katika kipindi kifupi cha miaka mitano nchi yetu imepiga hatua sana hata kuushangaza ulimwengu kwa namna alivyoiletea maendeleo ya haraka nchi yake ya Tanzania,” amesema Mzee Mwinyi.

Akitaja mafanikio ya Dk. Magufuli katika uongozi wake, Mzee Mwinyi amesema, amefanikiwa kuunganisha nchi kwa barabara za lami.

“Amestawisha uwekezaji na biashara nchini kwa kurahisisha mawasiliano hata masoko makubwa ya kisasa yameanza kuchipuka kama uyoga katika nchi yetu,” amesema.

error: Content is protected !!