Spread the love

 

KATIBU Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mzee Yusuph Makamba, amevitaka vyama vya upinzani nchini, vijitayarishe kuchuana na Rais Samia Suluhu Hassan, katika kinyang’anyiro cha urais wa Tanzania, kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025. Anariporti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Makamba ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, tarehe 1 Aprili 2022, jijini Dodoma, wakati akimuombea kura Abdulrahman Kinana, kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, wamteue kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara.

“Mama nilikusikia ukiongea na wanawake ukawambia hawakuchagua Rais mwanamke, Rais mwanamke watamchagua 2025…huyu mwanamke ni wewe. Nawaambia viongozi wa upinzani mko hapa, 2025 mgombea ni yule, kama kuna anayejiandaa huko akae tayari,” amesema Mzee Makamba.

Katibu Mkuu mstaafu huyo wa CCM, amesema katika kipindi cha uongozi wake akiwa Makamu wa Rais na sasa Rais wa Tanzania, Samia amefanya mambo mengi mazuri.

“Sisi Simba tuna kocha mzuri hawezi leo mtu akatuambia badilisheni kocha, hatutaki, Yanga wana kocha mzuri hata Simba anaogopa huu ubingwa nitaupata? Sasa Mama Samia alikuwa kocha msaidizi chini ya Magufuli, Mungu akamchukua tukamfanya kocha magoli yanaingia. 2025 mnaenda na nani tena?” amehoji Mzee Makamba.

Mwanasiasa huyo mkongwe nchini Tanzania, amesema Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), imefanya jambo sahihi kumteua Kinana kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, kwa kuwa atamsaidia Rais Samia kushinda kwenye uchaguzi huo.

Yusuph Makamba, Katibu Mkuu Mstaafu ww CCM

“Mimi nafurahi sana kwamba Kinana amependekezwa maana mnapokuwa na kocha mzuri lazima mumpe msaidizi mzuri, ili kocha akiumwa magoli yaingie, Kinana namjua, unapata kocha msaidizi mzuri. Ndugu zangu lazima mjue 2025 tuna ligi, sisi ndiyo mabingwa mama usiwe na wasiwasi,” amesema Mzee Makamba.

Samia alikabidhiwa mikoba ya Urais wa Tanzania, tarehe 19 Machi mwaka jana, kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, kilichotokea tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam.

Kiongozi huyo Mkuu wa nchi wa kwanza mwanamke Tanzania, alikuwa Makamu wa Rais kuanzia Novemba 2015 hadi Machi 2021.
Mzee Makamba amesema, Rais Samia alipoingia madarakni alimshukuru Mungu na kumuomba ampe uwezo wa kubeba majukumu yake mapya.

“Nikamuomba Mungu akujalie mabega makubwa ili uweze kuubeba mzigo huu. Namshukuru Mungu nyuki ameingia kwenye mzinga wa bibi tutalamba asali, sasa hivi watanzania wote tunalamba asali kwa maji yanayopatikana, mikopo inayopatikana ni asali,” amesema Mzee Makamba.

2 Responses

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *