May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwisho maombolezo ya Hayati Magufuli

Spread the love

 

LEO Jumanne, tarehe 6 Aprili 2021, ni siku ya mwisho ya maombolezo ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Dk. Magufuli (61), alifariki dunia saa 12:00 jioni, tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam.

Taarifa za kifo chake, zilitangazwa na aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa sasa ndiye Rais, baada ya kuapishwa.

Rais Samia alitangaza siku 21 za maombolezo na bendera zote kupepea nusu mlingoti ambapo siku hizo, zinamalizika leo Jumanne saa 5:59 usiku.

Mwili wa Hayati Magufuli, uliagwa na wakazi wa maeneo ya Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mwanza na Chato ambako kulifanyika maziko nyumbani kwao, Chato mkoani Geita, tarehe 26 Machi 2021.

Hadi anafikwa na mauti, Hayati Magufuli, alikuwa ameiongoza Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano na miezi minne.

Aliingia madarakani kwa mara ya kwanza tarehe 5 Novemba 2015, baada ya kutangazwa mshindi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), katika uchaguzi mkuu uliofanyika 25 Oktoba 2015.

Pia, Hayati Magufuli, alitangazwa mshindi na NEC, katika uchaguzi mkuu uliopita wa tarehe 28 Oktoba 2020 na akaapishwa 5 Novemba 2020, kumalizika ungwe ya mwisho wa miaka mitano, ambayo hata hivyo, hakuimaliza.

Hayati Magufuli ameacha Mjane, Janeth Magufuli ambaye alifunga naye ndoa takatifu Kanisa Katoliki la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1989.

Pia, ameacha watoto saba ambao ni; Suzana, Edna, Mbalu, Joseph, Jesca, Yuden na Jeremiah.

error: Content is protected !!