April 11, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mwinyi amteua Maalim Seif makamu wa kwanza wa Rais

Maalim Seif Sharif Hamad, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo

Spread the love

RAIS wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi amemteua Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Rais Mwinyi alifanya uteuzi huo jana Jumapili tarehe 6 Desemba 2020 kwa kutumia matakwa ya Kifungu cha 9(3) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Kifungu hicho kinasema “Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa na Umoja wa Kitaifa na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na lengo la kufikia demokrasia.”

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee ilieleza, uteuzi huo wa Maalim Seif mwenye miaka 77 umeanza jana Jumapili.

Rais Mwinyi alifanya uteuzi huo, ikiwa ni saa chache zimepita tangu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu kuzungumza na waandishi wa habari kutoa maazimio ya kikao cha kamati kuu kilichojadili suala hilo la kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar

Kikao hicho, kilikubali kwenda kushiriki katika Serikali hiyo pamoja na madiwani, wabunge na wawakilishi walioshinda katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 27 na 28 Oktoba 2020, kwenda katika vyombo vya uwakilishi kuanza majukumu yao.

Maalim Seif aliyezaliwa 22 Oktoba 1943, anarejea tena kwenye nafasi hiyo kwa mara ya pili baada ya ile ya mwaka 2010-2015 kuhudumu akiwa Chama Cha Wananchi (CUF) na Rais wa wakati huo alikuwa Dk. Ali Mohamed Shein.

error: Content is protected !!