January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwingine Usalama wa Taifa atia nia urais

Dk. Hassy Kitine

Spread the love

DAKTARI Hassy Bessen Kitine – Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), amekuwa kiongozi mwandamizi wa pili kutoka katika taasisi hiyo nyeti kutangaza nia ya kuomba uteuzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuwania urais Oktoba 25 mwaka huu. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Ni siku moja tangu mtangulizi wake katika idara hiyo, kati ya mwaka 1980 hadi 1983, Dk. Augustine Mahiga naye atangaze uamuzi kama huo jana na hivyo kuzua maswali mengi kwa wadadisi wa kisiasa.

Mbali na hao, pia wako makachero wengine waliowahi kufanya kazi katika idara hiyo, Mizengo Pinda (Waziri Mkuu) na Bernard Membe (Waziri wa Mambo ya Nje), ambao nao wameingia katika kinyang’anyiro hicho.

Dk. Kitine anakuwa mwana-CCM wa 28 kuingia katika kinyang’anyiro hicho cha kuomba uteuzi, akitanguliwa na Dk. John Magufuli, William Ngereja, Prof. Sospeter Muhongo, Amosi Siyatenzi, Mizengo Pinda, January Makamba, Balozi Amina Salum Ali, Luhanga Mpina, Dk. Hamis Kigwangalla, Edward Lowassa na Boniface Ndengo.

Wengine ni; Fredrick Sumaye, Mark Mwandosya, Lazaro Nyalandu, Dk. Mwele Malecela, Dk. Titus Kamani, Samuel Sitta, Balozi Ali Abeid Karume, Dk. Gharib Mohamed Bilal, Mwigulu Nchemba, Makongoro Nyerere, Steven Wasira, Godwin Mwapongo, Peter Nyalali, Bernard Membe, Leonce Mulenda na Mathias Chikawe.

Hata hivyo, mjadala mkali umejitokeza baada ya vigogo hao wakuu wastaafu wa TISS kutia nia na hivyo kuzua utata kwamba huenda kuna sababu maalum hasa kufuatia tetesi za usaliti ndani ya idara hiyo, baada ya baadhi ya vigogo wengine wastaafu kutajwa kuwaunga mkono baadhi ya makada wenye nguvu waliyomo kwenye kingang’anyiro.

Dk. Kitine, aliyewahi kuwa pia Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Mbunge wa Makete mkoani Iringa, ametangaza nia yake mkoa Dodoma katika ukumbi wa Royal Village Hotel mbele ya waandishi wa habari.

Staili yake ilikuwa ya kawaida kama alivyofanya Dk. Mahiga kwa kutoongozana na misafara ya wapambe wala kutangazwa moja kwa moja kwenye runinga na redio kama walivyofanya makada wenzao wengi waliotangaza nia.

Amesema “Baba wa Taifa alituambia, ukiwa na mtu anayekimbilia Ikulu hasa akigawa mapesa mpaka anatisha. Huyu mtu akienda Ikulu lazima azirudishe, wakati huko hakuna biashara.”

 “Wananchi ninawaomba sana. Wakiwapa fedha chukueni. Kwanza, hakuna mtu anayekataa fedha. Pili hizo fedha wameiba. Wamewaibia nyinyi wenyewe,” amesisitiza Kitine.

Pia , Dk. Kitine amesema “baadhi ya vyombo vya habari vimenunuliwa. Nilikuwa kiongozi wa Usalama wa Taifa. Ninajua mbinu wanazozitumia kuingia Ikulu.”

Aidha, amesema akipata ridhaa ya chama na akichaguliwa kuwa rais, kazi kubwa atakayoifanya ni kutekeleza Ilani ya CCM ambayo mpaka sasa haijatolewa huku akipendekeza sifa za mtu anayefaa kuwa rais ziingizwe kwenye Ilani hiyo.

Kitine ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa kwanza wa Utawala Bora wakati wa uongozi wa awamu ya tatu, amezitaja sifa hizo kuwa ni kiongozi mwenye awe na uwezo wa kuangalia usalama wa nchi; uwezo, utashi na hulka ya kuhakikisha ulinzi na usalama kwa familia, mali zao na mipaka ya nchi.

“Lazima awe muadilifu wa asili, mwenye uwezo na elimu ya kutosha. Awe na shauku na roho ya kuhakikisha kilimo sio tu kinasaidia katika maendeleo bali kiwe ni cha taaluma kwa ajili ya kuboresha maisha yetu,” ameeleza Kitine.

Sifa zingine amezitaja kuwa ni kuanzisha au kujua sera sahihi za maendeleo ya nchi katika sekta za kilimo, uvuvi, viwanda na biashara, utashi na uwezo wa kufanya maamuzi magumu, atakayeongoza nchi kwa sheria, mwenye hofu ya Mungu, mwenye upendo kwa watu wote na awe na uwezo wa kujua uchumi. 

“Nilikuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa. Ni kazi mbaya. Madaraka yake ni makubwa na mabaya. Anayekutisha ni Rais peke yake. Naifahamu Ikulu kuliko wagombea wote. Mkinipitisha kuwa Rais, nitawashughulikia mafisadi,” ameeleza Kitine.

error: Content is protected !!