Tuesday , 5 December 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Mwingine aondoka Chadema, aelekea NCCR- Mageuzi
Habari za SiasaTangulizi

Mwingine aondoka Chadema, aelekea NCCR- Mageuzi

Ndiholeye Zuberi Kifu, aliyekuwa Mratibu wa Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo vikuu nchini (CHASO), kupitia Chama cha Dekomrasia na Maendeleo (Chadema).
Spread the love

NDIHOLEYE Zuberi Kifu, Mratibu wa Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo vikuu nchini (CHASO), kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani Kilimanjaro, amejiondoa kwenye chama hicho. Anaripoti Mwandishi Wetu kutoka Dodoma…(endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili, mjini Dodoma, Ndiholeye ambaye ni mwanafamilia ya aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), Kifu Gulam Hussen Kifu amesema, ameondoka Chadema, baada ya kujiridhisha kuwa chama hicho, siyo tena mali ya umma.

Amesema, “…katika kipindi cha miaka mitano niliyokuwa ndani ya Chadema, nimekutana na mambo makubwa sana. Kule ndani kuna ubaguzi na upendeleo, usiyo na kipimo.

“Kinyume na inavyohubiriwa huku nje, ndani ya Chadema, hakuna demokrasia. Hakuna uwazi na hakuna haki.”

Kifu ambaye alikuwa Mratibu wa CHASO mkoani Kilimanjaro hadi mwishoni mwa mwaka jana anasema,
pamoja na kupitishwa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), mkoa wa Kigoma, bado hakuweza kushinda kutokana na kuwekewa hila na mizengwe na baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi huo.

“Niliyokutana nayo kwenye uchaguzi huo, siyo rahisi kuyaeleza hapa; bali itoshe tu kusema kwamba, nawashauri vijana wenzangu walioko Chadema, wasijaribu hata kutamani nafasi za uongozi wa juu ndani ya chama hiki,” anaeleza Kifu.

Anasema, hii ni kwa sababu, nafasi zote za juu ndani ya Chadema, zilikuwa tayari zina wenyewe na kwamba kinachofanyika wakati wa mkutano mkuu, ni maagizo ili watu walioko nje waone kuwa chama hiki kinaendesha mambo yake kwa uwazi na kinafuata demokrasia.

Kifu anatoa mfano wa nafasi ya mwenyekiti wa taifa, ambako Freeman Mbowe, alitangazwa mshindi.

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, ushindi wa Mbowe kwenye uchaguzi huo, ulishandaliwa, na ndiyo maana yeyote aliyejaribu kuitaka nafasi hiyo, alisakamwa, kutengwa na hata kupachikwa majina mabaya ya usaliti.

“Hata lile kundi la vijana lililojitangaza kumchukulia fomu Mbowe na kuhubiri kwa sauti kubwa, ‘Mwamba Tuvushe,’ lilikuwa limeandaliwa rasmi na washirika wa Mbowe, ambao baadhi yao wakiwa wajumbe wa Kamati Kuu,” anasisitiza.

Anasema, siyo kweli hata kidogo, kwamba watu wote waliofanya kazi ya kumnadi Mbowe, walifanya hivyo kwa mapenzi yao na bila kulipwa ujira wowote.

Anasema, upo ushahidi wa kutosha kuwa baadhi ya wapambe wake, walilipwa ujira wa fedha na wengine waliahidiwa vyeo, ikiwamo ubunge wa viti maalum, ukurugenzi na ukatibu wa kanda.

Akiongea kwa kujiamini, Kifu anasema, “tunahubiri demokrasia na tunashinikiza kuwapo kwa Tume Huru ya Uchaguzi, ni jambo jema sana. Lakini tujitazame na sisi wenyewe. Je, tunayoTume huru ya kusimamia chaguzi zetu,” anahoji.

Anasema, jibu ni hapana. Ndani ya Chadema, Kifu anaeleza, watu wamekuwa wakivunja Katiba, Kanuni na taratibu za uchaguzi, bila aibu na hadharani.

“Tumeshuhudia watu wakiondolewa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi, bila kuelezwa sababu za kufanya hivyo. Tumeshuhudia rushwa. Tumeshuhudia upendeleo na tumeona uvunjaji wa Katiba ya Chama ya mwaka 2006, Toleo la 2016, pamoja na Kanuni zake,” anaeleza.

Anasema, Ibara ya 7.2 ya Katiba ya Chadema, inaeleza kwamba, vikao vya uteuzi vinatakiwa kuwafahamisha wale wote ambao hawatapendekezwa, sababu za kutopendekezwa na kwamba, rufani zote lazima ziwasilishwe na kuamuliwa kabla au wakati wa uteuzi wa mwisho, ili kwenda na ratiba ya uchaguzi.

Lakini Kamati ya Uchaguzi ya Chadema, haikutoa nafasi kwa wagombea walioenguliwa kuelezwa sababu za kuenguliwa kwao, wala haikutoa nafasi kwa wasioridhika na mwenendo wa uchaguzi, kuwasilisha rufaa zao, jambo ambalo ni kinyume na Katiba.

Anasema, “matendo haya makubwa ya uvunjifu wa Katiba ya Chama, Kanuni na taratibu zake, yaliyofanyika kipindi cha uchaguzi mkuu na yanayoendelea kufanyika sasa, yamenifanya mimi kuona kuwa uwezekano wa Chadema kuwa mbadala wa CCM, ni sawa na ndoto za mchana.

“Ndani ya Chadema, hakuna usawa wa kijinsia. Mfano mzuri, ni mimi mwenyewe niliyekuwa miongoni mwa wanawake wachache waliojitokeza kugombea, lakini nikapigwa vita na wanaume kwa sababu zao binafsi.

“Katika viongozi wote wakuu wa taifa 6 wa chama – mwenyekiti wa taifa, makamu wake wawili, katibu mkuu na manaibu wake wawili – hakuna mwanamke hata mmoja. Ndani ya Kanda, kati ya makatibu 10 wanaounda kada, hakuna mwanamke hata mmoja.

“Katika kanda zote 10, mwenyekiti wa kanda ambaye ni mwanamke, ni mmoja tu; huku nafasi za wakurugenzi zote za makao makuu, zikishikiliwa na wanaume.”

Akizungumzia nafasi za viti Maalum vya udiwani na ubunge, Kifu anadai zinatolewa siyo kwa vigezo ambavyo vinaelezwa, bali ni kwa upendeleo, unaotegemea sana, kwamba nani anayekubeba kwenye uongozi wa chama.

“Wanawake wenyewe, hususani waliotangulia na kujijengea nguvu kubwa za kiuchumi, wamehodhi nafasi hizo na siyo rahisi kuwapisha wengine. Wapo waliokaa miaka 20, wengine 15, wegine 10 na bado wanaendelea kujipanga katika uchaguzi ujao, bila kujali uwezo wao,” anasisitiza.

Kifu anasema, baadhi ya wanawake wanatafuta uongozi ndani ya Chadema si kwa sababu ya kutaka kukijenga chama na kukitumikia, bali ni kujiwekea mazingira mazuri ya Viti Maalum na ndio maana uchaguzi wa Bawacha ulitawaliwa na mizengwe.

Anasema, “…watu wote waliotaka kugombea nafasi ya mwenyekiti wa Bawacha taifa, walifanyiwa mizengwe na hata wabunge wanawake wenye uwezo hupigwa vita na viongozi wenyewe wa Bawacha.”

Anasema, “baada ya kutafakari mambo haya yote na mengine, ambayo yamezalisha malalamiko mengi ndani ya Chadema; na baada ya kujiridhisha kuwa viongozi wakuu wa chama hiki, wevimba kichwa kutokana na mafanikio yaliyotokana na ukuaji wa chama, nimeamua kwa moyo mkunjufu kuondoka Chadema na kujiunga na NCCR- Mageuzi, chama ambacho nimeona kimejiekeza katika Itikadi yake ya kulinda na kutetea utu wa mwanadamu.”

Anakiasa Chadema, kuacha kujikweza na kujiona kimefika kwa kuwa chama chochote cha siasa huwa kinazaliwa, kinaishi na kinakufa.

mwisho

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Dk. Biteko: Viongozi tuache alama nzuri katika utendaji wetu

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari za SiasaTangulizi

Chanzo maporomoko yaliyoua 65 Hanang, chatajwa

Spread the loveSERIKALI imesema kumeguka kwa sehemu ya Mlima Hanang ambao ilikuwa...

Habari za Siasa

Baba yake Ole Sabaya ashinda Uenyekiti CCM – Arusha

Spread the loveLoy Thomas Sabaya ambaye ni Baba wa aliyekuwa Mkuu wa...

Habari za Siasa

Serikali yaagiza uchunguzi chanzo maporomoko Hanang

Spread the loveSERIKALI imeagiza uchunguzi ufanyike ili kubaini chanzo cha maporomoko ya...

error: Content is protected !!