January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Mwalimu Nyerere’ atoa mapendekezo ya kudumisha Amani

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad akifunga mkutano wa kujadili amani na utulivu nchini

Spread the love

VIONGOZI waliokutana katika mkutano wa mashauriano kuhusu amani na utulivu wa nchi, wametoa mapendekezo ya nini kifanyike kudumisha amani na umoja wa taifa. Anaandika Pendo Omary …(endelea).

Mkutano huo ulifanyika jana na leo jijini Dar es Salaam ambapo waandaaji ni Taasisi ya Mwalimu Nyerere, huku wahudhuriaji wakiwa ni wazee, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani na viongozi wastaafu wa serikali.

Hatua hiyo inakuja baada ya kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani nchini hali ambayo inaweza kuzua machafuko muda wowote.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Joseph Butiku ameyasoma mapendekezo hayo kuwa ni;-

 1. Viongozi na jamii itambue kuwa misingi ya Amani na umoja ni haki na usawa.
 2. Utawala wa sheria uzingatiwe na usimamiwe na viongozi na wananchi wote na adhabu zitolewe kwa watakaokiuka.
 3. Wananchi wanapaswa kujifunza na kuelewa misingi ya amani na kuitumia kusimamia uongozi na utendaji wao na kujisimamia wao wenyewe.
 4. Maliasili itambulike ni ya watanzania wote na itatumiwa kwa mipango mizuri ili iwasaidie wote. Wageni wanaotaka kutumia rasilimali zetu watafanya hivyo bila kuvunja misingi hiyo.
 5. Vyama vya siasa ndivyo vyenye wajibu wa kwanza wa kutoa viongozi na kuweka sera zinazozingatia usawa na haki na vitambue kwamba ni vyombo vya wananchi wote na vitahakikisha mipango yao, sera zao haziwagawi wananchi wala kusababisha fujo na kuvunjiana heshima kwa namna yoyote ile.
 6. Mataifa ya kigeni na wageni wote wanaotoka katika mataifa hayo kama wawekezaji au kwa shughuli nyingine inabidi wazingatie misingi ya haki na usawa na uhuru na heshima na wasiruhusiwe kujiingiza katika mipango yenye muelekeo wa kuwanyang’anya watanzania mali zao, bali wawe shirikishi na wazingatie misingi ya ubia kwa mujibu wa sharia. Serikali inaombwa na kuhimizwa kusimamia jambo hili kwa makini.
 7. Ushauri kwa uongozi; imedhihirika kwamba viongozi wetu wakuu wamepungukiwa kwa kiwango kikubwa uwezo wa kuaminiana, kuheshimiana, kupendana na kufanya kazi kwa pamoja (collective responsibility). Upungufu huu umekuwa na athari kubwa kwa uongozi wa pamoja na kwa kiasi kikubwa umechangia kuathiri misingi ya amani na umoja na kwa hiyo amani kwa ujumla.
 8. Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, usicheleweshwe bali ufanyike kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi na kwa muda uliopangwa. Aidha ihakikishwe kuwa unakuwa uchaguzi wa amani, haki na ulio huru.
 9. Tunathamini na kupongeza uamuzi uliotolewa na serikali wa kuahirisha Kura ya Maoni kuhusu Katiba inayopendekezwa na tunashauri Tume ya Taifa ya Uchaguzi iendelee kufanya maandalizi yanayotakiwa ili kura ya maoni ifanyike kwa wakati muafaka.
 10. Uhuru wa dini uheshimiwe. Migogoro ya kidini inapojitokeza ishughurikiwe na viongozi wa dini na waumini wao.
 11. Kwa mujibu wa Katiba na Sheria wananchi ndio wenye kauli ya mwisho katika mambo ya utawala wa  nchi yao. Maoni, mawazo na hisia zao zisikilizwe na kuzingatiwa kwa makini ili kuepuka kujiingiza katika maamuzi na matendo yanayoweza kuvunja amani ya nchi.
error: Content is protected !!