Wednesday , 29 March 2023
Home Kitengo Habari Kimataifa Mwili wa Mwai Kibaki huenda ukafukuliwa, kupimwa DNA
Kimataifa

Mwili wa Mwai Kibaki huenda ukafukuliwa, kupimwa DNA

Spread the love

MWILI wa aliyewahi kuwa Rais wa Kenya, Mwai Kibaki, huenda ukafukuliwa kwaajili ya kufanyiwa vipimo vya DNA endapo Mahakama Kuu nchini humo itakubaliana na ombi la watu wawili, Jacob Mwai na mwanamke mmoja anayefahamika kama JNL, wanaodai kuwa ni watoto wake. Vimeripoti vyombo vya habari nchini humo…(endelea). 

Kituo cha televisheni cha KTN kimeripoti kwa undani taarifa hiyo ya mahakamani ambapo watu hao wawili wameieleza mahakama kuwa wao ni watoto halali wa Kibaki hivyo wanastahili urithi wa mali alizoziacha.

Kibaki alifariki dunia mnamo mwaka 2022 na kuacha watoto wanne wanaotambulika ambao aliwazaa na mke wake wa ndoa Lucy Kibaki.

Watoa maombi katika kesi hiyo wametoa ombi hilo kwa Mahakama ya nchi humo baada ya kugonga mwamba kupata vipimo vya DNA kutoka kwa watoto wanne wa Kibaki ili kuona kama wana uhusiano wa kijenetiki.

Katika hati ya kiapo, JNL ameiambia Mahakama kuwa marehemu Mwai Kibaki na mama yake walikutana wakati wakiwa masomoni Uingereza miaka ya 1950.

Ameendelea kueleza kuwa uhusiano wa wazazi wake uliendelea hata waliporudi nchini na kwamba hata Kibaki aliwahi kumtembelea yeye na mama yake hospitalini alipozaliwa Desemba mwaka 1961 siku 16 kabla ya Kibaki kufunga ndoa na mke wake Mama Lucy Kibaki.

Hata hivyo mwanamke huyo mwenye miaka 62 amesema kuwa cheti chake cha kuzaliwa kina pengo katika sehemu ya jina la baba.
Anaongeza kuwa alisoma katika shule moja ya Hospital Hill na watoto wa marehemu Kibaki kwa miaka saba.

“Mbali na kuwa marafiki, tulijuana kwa karibu. Baadae pia tulisoma na Wanjiku (mwanawe Kibaki) nchini Marekani na tulikuwa marafiki,” ameeleza JNL katika hati yake ya kiapo.

Mwanamke huyo ameendelea kudai kuwa watoto wa kiume wa Kibaki ambao ni Jimmy, Kagai na Githinji pamoja na jamaa wengine wa Kibaki, wanamtambua kama ndugu yao lakini kikwazo kimekuwa kwa ndugu wa kike.
Kwa upande wake Jacob ambaye naye ana miaka 62 amedai kuwa kufanana kwake na Mwai Kibaki ni ishara tosha kwamba ana uhusiano na baba yake huyo.

Ameitaka mahakama kuchunguza kwa karibu kipara, uso, masikio, pua, shavu, mfupa wa shavu, fremu ya mwili na jinsi anavyotembea, “utakubali kuwa mimi na marehemu Kibaki ni mtu na baba yake,”

Hata hivyo watoto wa Kibaki wakiongozwa na Judith wamepinga mchakato wowote wa kupima DNA zao pamoja na ya baba yao.
Ameeleza kuwa kifo cha baba yao kilikuwa cha kitaifa na kimataifa na hivyo mahakama haipaswi kutoa amri ya kufukuliwa kwake.

Amedai kuwa hatua ya wawili hao kujitokeza baada ya kifo cha baba yake kudai urithi ni ya kutiliwa shaka na kwamba baba yao hakuwahi kuwatambulisha kwao hata mara moja.
Kesi ya kuamua hatima ya wawili hao inatarajiwa kusikilizwa tarehe 28 Februari 2023 mbele ya Jaji Eric Ogoa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Kimataifa

Nyumba ya babu yake Makamu wa Rais wa Marekani yatafutwa Zambia

Spread the love  KAMALA Harris, makamu wa rais wa Marekani, amepanga kutembelea...

Kimataifa

Benki ya Uswizi mbioni kuziwekea vikwazo akaunti za siri za Wachina

Spread the love  WAKATI Serikali na Benki ya Uswizi ikichukua hatua kali...

Kimataifa

Netanyau asitisha mipango yenye utata marekebisho mfumo wa sheria

Spread the love  WAZIRI Mkuu wa nchini Israel, Benjamin Netanyahu amesema atachelewesha...

Kimataifa

Raila ahutubia waandamanaji, mabomu yarindima

Spread the loveMSAFARA wa kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga...

error: Content is protected !!