May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwili wa Magufuli wawasili Dodoma, wapelekwa Ikulu

Spread the love

 

MWILI wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli (61), umewasili Uwanja wa Ndege wa Dodoma, ukitokea mkoani Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Maelfu ya wananchi wamejitokezaa kwa wingi kuupokea mwili wa Dk. Magufuli ambaye kwenye utawala wake wa awamu ya tano, alifanikisha adhima ya kuihamishia Serikali mkoani Dodoma.

Ndege iliyoubeba mwili wa Dk. Magufuli, ilitoka Uwanja wa Ndege wa Jeshi wa Airwing majira ya saa 12 na dakika kadhaa na kutua Uwanja wa Ndege wa Dodoma saa 12:55 jioni, ukiwa umetumia takribani dakika 50.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliwaongoza wananchi na viongozi mbalimbali wa kisiasa, dini na kiserikali kuupokea mwili wa Dk. Magufuli.

Pia, Janeth ambaye ni Mjane wa Dk. Magufuli na familia nzima, ilikuwapo uwanjani hapo, kushuhudia jeneza lenye mwili wa mpendwa wao, likishushwa katika ndege ya Shirika la Ndege ya Tanzania (ATCL).

Viongozi wengine waliokuwapo ni; Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah.

Mara baada ya kuwasili, mwili huo wa Dk. Magufuli umepelekwa Ikulu ya Chamwino ambako utalala hadi kesho Jumatatu.

Kama ilivyokuwa kwa wananchi wa Dar es Salaam waliojipanga barabarani ulipokuwa ukipita, ndivyo imekuwa Dodoma ambapo wananchi wakijipanga kando ya barabara kuelekea Chamwino.

Ratiba inaonyesha kesho Jumatatu ambayo ni siku ya mapumziko, mwili wa Dk. Magufuli utapelekwa bungeni jijini Dodoma, ili kutoa fursa kwa wabunge kutoa heshima za mwisho.

Kisha mwili wake, utapelekwa Uwanja wa Jamhuri ambapo kutafanyika shughuli ya kumuaga kitaifa na Rais Samia Suluhu Hassan, atawaongoza Watanzania na wageni mbalimbali, kumuaga kiongozi huyo.

Mapema leo mchana Jumapili, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dk. Hassan Abbas alisema, marais kumi kutoka Afrika na jumuiya za kimataifa, mabalozi, asasi za kikanda zaidi ya 50 watashiriki.

Dk. Abbas amewataja Marais hao na nchi zao kwenye mabano ni; Uhuru Kenyatta (Kenya), Lazarus Chakwera (Malawi), Azali Assoumani (Comoro), Filipe Nyusi (Msumbiji) na Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe.

Wengine ni; Edgar Lungu (Zambia), Hage Geingob (Namibia), Mokgweetsi Masisi (Botswana), Felix Tshisekedi (Congo) na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini.

Mbali na marais hao, Dk. Abbas alisema Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Rais wa Angola, Joao Lourenco na Rais wa Burundi, Everist Ndiyashimiye, watawakilishwa katika shughuli hiyo.

Mwili wa Hayati Magufuli utaagwa kesho Dodoma, baada ya kuagwa mkoani Dar es Salaam kwa siku mbili, Jumamosi na Jumapili ambako kulishuhudia umati mkubwa uliojitokeza kutoa heshima za mwisho.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiaga mwili wa Hayati John Magufuli

Baada ya mwili wa Hayati Magufuli kuagwa Dodoma, keshokutwa yaani Jumanne, tarehe 23 Machi 2021, utaagwa na wananchi wa Zanzibar, kisha utasafirishwa kuelekea mkoani Mwanza, ambapo utaagwa Jumatano tarehe 24 Machi 2021.

Alhamisi itakuwa zamu na familia na wananchi wa Chato mkoani Geita na kesho yake yaani Ijumaa ya tarehe 26 Machi 2021, itakuwa siku ya kuhitimisha safari yake hapa duniani kwa maziko yatakayofanyika nyumbani kwao, Chato.

Dk. Magufuli, alifikwa na mauti saa 12:00 jioni ya Jumatano tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu.

Hadi anafikwa na mauti, alikuwa amewatumikia Watanzania kwa nafasi ya urais takribani miaka mitano na miezi mitano.

Kutokana na kifo hicho, Mama Samia, aliyekuwa makamu wa Rais, aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania.

error: Content is protected !!