April 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mwili wa Hayati Magufuli kuzikwa leo, Rais Samia atoa shukrani

Spread the love

 

WAKATI mwili wa Hayati John Pombe Joseph Magufuli, ukizikwa leo Ijumaa tarehe 26 Machi 2021, nyumbani kwao, Chato mkoani Geita, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za shukrani kwa viongozi wa kimataifa, dini na wa kisiasa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Chato … (endelea).

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Rais Samia amewashukuru viongozi hao kutokana na mchango wao wa hali na mali katika msiba wa Hayati Rais Magufuli, tangu alipotangaza kifo chake tarehe 17 Machi 2021.

“Leo tunapompumzisha mpendwa wetu Hayati Rais Magufuli kwenye nyumba yake ya milele, kwa niaba yangu binafsi na niaba ya watu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kuwashukuru Watanzania wenzangu.”

“Viongozi wenzangu pamoja na viongozi wastaafu, viongozi wa nchi na mashirika mbalimbali ya kimataifa, viongozi wa dini, viongozi wa kisiasa, jumuiya ya kidiplomasia, vyombo vya habari, wasanii na kila aliyekuwa nasi bega kwa bega wakati huu mgumu kwa Taifa letu,” ameandika Rais Samia.

Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania

Mwili wa Hayati Rais Magufuli unazikwa leo, baada ya kuagwa katika mikoa mitano (Dar es Salaam, Dodoma, Unguja-Zanzibar, Mwanza na Geita ), kuanzia tarehe 20 hadi jana 25 Machi 2021.

Mapema leo asubuhi, mwili wa Dk. Magufuli umepelekwa kanisani kwa ibada fupi ambapo, familia ilipata fursa ya kuuaga mwili wa mpendwa wao kisha ukapelekwa Uwanja wa Mpira wa Chato kwa ajili ya misa takatifu.

Misa hiyo takatifu, inaongozwa na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Gervas Nyaisonga.

Katika shughuli ya mazishi ya kitaifa iliyofanyika tarehe 22 Machi 2021, makao makuu ya nchi jijini Dodoma, wakuu wa nchi tisa na viongozi wa jumuiya na taasisi mbalimbali za kimataifa walihudhuria.

Miongoni mwa wakuu wa nchi waliohudhuria ni, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta. Lazarus Chakwera (Malawi). Azali Assoumani (Comoro). Filipe Nyusi (Msumbiji). Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe).

Felix Tshisekedi Rais wa Congo

Wengine ni, Edgar Lungu (Zambia). Mokgweetsi Masisi (Botswana). Felix Tshisekedi (Congo). Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini).

Hayati Rais Magufuli alifariki dunia katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo.

Kufutia msiba huo mzito, Rais Samia amewaomba Watanzania kuendelea kuiombea roho ya Hayati Rais Magufuli, ili Mungu aipumzishe kwa amani.

“Tafadhali pokeeni shukrani zetu za dhati na muendelee kuiombea roho ya Hayati Dk. Magufuli ipumzike kwa amani na Mungu aendelee kuifariji familia yake,” ameomba Rais Samia.

Hayati Rais Magufuli amefariki dunia akiwa madarakani, takribani miezi mitano tangu alipoapishwa kuendelea na muhula wake wa mwisho wa uongozi katika Serikali ya Awamu ya Tano, tarehe 5 Novemba 2020.

Hayati Rais Magufuli aliapishwa kuendelea kuiongoza Tanzania, baada ya kushinda kiti cha Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Kwa mara ya kwanza Hayati Rais Magufuli, aliingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015, baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka huo.

Baada ya Hayati Rais Magufuli kufariki dunia, Mama Samia aliyekuwa makamu wake wa rais, aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania, Ikulu ya Dar es Salaam, tarehe 19 Machi 2021.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu kwa habari na taarifa mbalimbali

error: Content is protected !!