MWILI wa Hayati Rais wa awamu ya tano, John Pombe Magufuli (61), utazikwa Ijumaa ijayo ya tarehe 26 Machi 2021, badala ya Alhamisi, Chato mkoani Geita. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Pia, mwili huo, utapelekwa Zanzibar Jumanne tarehe 23 Machi 2021, ili kutoa fursa kwa wananchi wa visiwa hivyo, kuuaga na kisha kusafirishwa kwenda Mwanza watakaoaga kesho yake yaani Jumatano.
Awali, ratiba iliyokuwa imetangazwa jana Ijumaa tarehe 19 Machi 2021 na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alisema mwili wa Dk. Magufuli ungezikwa Alhamisi ya 25 Machi 2021, nyumbani kwao Chato mkoani Geita.
Katika ratiba hiyo, mkoa wa Dodoma ilikuwa imepangiwa siku mbili za kuuaga yaani Jumatatu na Jumanne lakini sasa, itakuwa siku moja ya Jumatatu 22 Machi 2021, ambapo utaagwa kitaifa na tayari Rais Samia ameitangaza kuwa siku ya mapumziko.
Pia, Rais Samia aliitangaza Alhamisi ya 25 Machi 2021, kuwa siku ya mapumziko ambayo angezikwa.
Hata hivyo, haijafahamika kama itaendelea kuwa ya mapumziko au itabadilishwa na kuwa Ijumaa ambayo ndio hasa, mwili wa Dk. Magufuli utahifadhiwa kwenye nyumba yake ya milele.
Dk. Magufuli (61), alifikwa na mauti saa 12 jioni ya Jumatano tarehe 17 Machi 2021, akiwa Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa mfumo wa umeme wa moyo.
Leo Jumamosi na kesho Jumapili, mwili wa Dk. Magufuli aliyehudumu nafasi ya urais kwa takribani miaka mitano na miezi mitano, utaagwa na wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam na maeneo jirani.
Leave a comment