January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mwili wa Dk. Kigoda kuwasili kesho

Spread the love

MWILI wa marehemu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk. Abdallah Omar Kigoda unatarajiwa kuwasili nchini kesho saa 9 mchana. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Dk. Kigoda alifariki dunia jana saa 10 jioni katika Hospitali ya Appolo, jijini New Delhi, India, ambako alipelekwa miezi miwili iliyopita kupata matibabu.

Mzee Masimba, mtu wa karibu na familia ya marehemu, ameiambia MwanaHALISI Online, kwamba ratiba ya awali mwili ukishafika utapelekwa nyumbani kwake mtaa wa Mindu, eneo la Upanga, Dar es Salaam.

Siku ya Alhamisi, mwili huo utapelekwa uwanja wa Karimjee, kwa ajiliu ya kuagwa, shughuli ambayo ikishakamilika, itaruhusu safari ya kuupeleka mwili nyumbani kwao marehemu Handeni Mjini, mkoani Tanga, kwa ajili ya mazishi.

Shughuli ya kuaga mwili wake, inatarajiwa kuratibiwa na Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, ambako alitumikia kama mbunge kwa vipindi vinne mfululizo.

Baada ya uchaguzi wa 1995 alipoingia bungeni kwa mara ya kwanza, Dk. Kigoda aliteuliwa Waziri wa Mipango na Ubinafsishaji chini ya Rais Benjamin Mkapa na moja ya majukumu yake makubwa kuwa kusimamia sera ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma.

Baada ya uchaguzi wa 2010, aliendelea kuwa mbunge pasina kuteuliwa uwaziri hadi yalipofanyika mabadiliko ya baraza la mawaziri mwaka 2013 akichukua nafasi ya Dk. Cyril Chami aliyeondolewa kwa kashfa ya ukaguzi wa magari yanayoingia nchini kutoka Japan.

Dk. Kigoda (62) ni mmoja wa wanasiasa wakongwe waliokulia ndani ya chama hicho tangu akiwa amejiunga na TANU mwaka 1966 kupitia Umoja wa Vijana wa Chama hicho (TANU Youth League).

Kifo chake kimesababisha kampeni za ubunge Handeni Mjini kuahirishwa ili kusubiri ratiba mpya ambayo CCM itaruhusiwa kuteua mgombea mwingine.

Huyo ni mgombea wa nne kufariki na kusababisha uchaguzi kusogezwa mbele baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25. Kabla, wagombea waliofariki walikuwa wa majimbo ya Lushoto (Mohamed Mtoi wa Chadema), Ulanga (Celina Kombani wa CCM) na Arusha Mjini (Estomi Malla (ACT-Wazalendo).

Dk. Kigoda alizaliwa 25 Novemba 1953; Alipata elimu ya msingi Shule ya Msingi Chanika na kuhitimu Shule ya Msingi Mswaki mwaka 1965.

Kidato cha kwanza hadi cha nne Shule ya Sekondari ya Tanga alikohitimu mwaka 1969; Kidato cha Sita katika Sekondari ya Mzumbe, mjini Morogoro alikohitimu mwaka 1971.

Amesomea uchumi hadi ngazi ya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Vanderbilt kilichoko Jimbo la Tennesse, nchini Marekani alikohitimu mwaka 1980.

error: Content is protected !!